Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
HALI ndani ya Chama cha Mapinduzi CCM, inazidi kuwa mbaya, kutokana na baadhi ya wanachama na viongozi wake, kushindwa kuwekana sawa katika kipindi hiki kigumu. Wapo wapo tu. Kila mmoja anajifanya yeye ni zaidi ya mwenzake.
Wenaonyeshana nani ana sauti zaidi ya mwenzake. Hali hii ni mbaya mno. Maana, wakati wao wakiendelea kulumbana, wapinzani wao wanaitumia nafasi hiyo kujinufaisha, maana siku zote adui yako muombee njaa.
Ndio maana nasema CCM inauliwa na mengi, hivyo ipo haja ya kila mfuasi wa chama hicho, hasa vijana kukaa na kuliangalia hilo kwa mapana. Hatuwezi kuwa na maisha bora kama chama kinachoongoza nchi kinakuwa legelege, ama kinachotawaliwa na migogoro ya kimaslahi kila siku ya Mungu.
Mambo ya aina hiyo, yanasababisha msuaguano hata kwenye baraza la Mawaziri, kwenye ofisi mbalimbali kuwa chungu. Mfano, malumbano ya kimaslahi ya baadhi ya mawaziri wetu, hayawezi kutegua kitendawili cha maisha bora kwa kila Mtanzania. Hali hii ni mbaya mno. Angalia.
Licha ya Waziri Mkuu wa zamani aliyejiuzulu, Edward Lowassa, kutoa wazo la kujenga shule za Kata, lakini leo shule hizo ni kama mtu aliyevaa shati huku sehemu zake za siri zikiwa wazi. Unategemea nini hapo? Mtu gani anaweza kusifia shati zuri lililovaliwa, zaidi ya kucheka kila anapotupa macho yake na kugundua kwamba anayemuangalia hajajistiri?
Hakuna wa kuziendelesha shule hizo, maana anajua fika ni mtaji mkubwa wa kisiasa wa waziri huyo, ambaye kwa hakika bado yupo kwenye kikaango na makundi hasimu ndani ya CCM. Wenyewe wanasema vita ya Urais 2015. Kila mmoja anamsurubu mwenzake kwa faida yake. Pamoja na hayo, Watanzania, hawawezi kukosoa hata yale wenye faida nayo.
Hili la shule za kata, ni kubwa linaloweza kuboresha maisha ya Watanzania, kwa kuhakikisha kwamba watoto wao wanakwenda shule. Ni kwenye shule za kata tu. Nasema hivyo maana wengi wao hawawezi kumudu gharama za shule za binafsi zinazohitaji fedha nyingi.
Wakati hayo yakiendelea, shule za kata zinakabiriwa na changamoto nyingi, ikiwamo uhaba wa walimu, maabara na hata vifaa vingine vya kufundishia watoto wetu. Hapo huwezi kutarajia matokeo mazuri katika shule za kata, zenye maana kubwa na kizazi cha Tanzania, yenye kasumba za kila aina.
Tembelea katika kata, wilaya na mikoa mbalimbali ya Tanzania uone mambo. Hawana upendo. Ubinafsi, umimi ni matokeo ambayo hakika yananiweka CCM mahali pagumu. Haya lazima yasemwe kama kweli tunahitaji kujifanyia marekebisho kwa ajili ya kujiandaa na uchaguzi Mkuu ujao.
Kadri miaka inavyozidi kwenda mbele, ndivyo uchaguzi unavyozidi kuwa mgumu. Idadi kubwa ya vijana wanaona CCM tena sio mahali pao ndio maana wameingia zaidi kwenye vyama vya upinzani. Tena wamevaa upinzani kiasi cha kuwaona wenzao kinyaa, kisa wamebaki kwenye chama tawala.
Hutoa maneno ya kejeli na dharau za aina nyingi, wakiamini chama hicho sio sehemu sahihi na mkombozi wa wanyonge. Tuwaache na mtazamo wao. Lakini, kama wana CCM wenyewe hawatakuwa tayari kwa mabadiliko ama maono ya mbali, hakika hawawezi kufanya lolote katika mabadiliko haya.
Chama kitaanguka, maana wao wenyewe wamekubali kife. Tena wapo watakaotembea kifua mbele, wakijisifia kukiangusha kabla ya kuhamia upande mwingine wakipokelewa kwa shangwe kwa kukamilisha kazi waliyotumwa.
Huo ndio ukweli wa mambo. Kama sio ukweli, basi upo mbali na uongo. Upo wapi ukweli halisi wa muanzilishi wa Chama cha Kijamii (CCJ)? Je, sio kweli kama wengi waliokuwa ndani ya CCM ndio waanzilishi wake? Kama ni kweli, hao unategemea wana mapenzi mema na chama chao, kiasi cha kukiombea mema?
Unafiki wa aina hiyo ndio sumu. Niliwahi kusema katika makala zangu huko nyuma, hasa lile la mfanyabiashara maarufu, Mustafa Sabodo, kumwaga fedha zake kwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), huku akijifanya ni mwana CCM damu.
Wapo walioniunga mkono na walionitukana ama kuniparua kadri walivyoweza wao hawakukosena. Nakubali kukosolewa kama name ninavyowakosoa wenzangu, maana huo ndio uungwana unaotakiwa katika Dunia ya leo. Yale makundi yasiyokuwa na tija ndani ya chama yakomeshwe, ili kama ni kulia tulie wote.
Na wale ambao wamekosa mapenzi mema na chama chao, ni wakati wao kuondoka, ili wachache wanaobakia wakijenge chama chao. Waswahili wamesema akheri ya ndege mmoja mkonono kuliko ndege kumi mtini.
Kujisifia una wanachama wengi, wakati ni wanafiki, ni wafitina, wazandiki, huko ni kutwanga maji kwenye kinu. Mengi yanasemwa, ila yanamezewa tu. Wapo ambao wametembea kwa furaha mara baada ya Sioi Sumari kukosa
Ubunge katika Uchaguzi Mdogo wa Arumeru Mashariki. Bado hao utawaita ni wana CCM? Kwalipi? Mapenzi yao kwa chama yapo vipi? Hao hao ndio wanaofanya mambo kinyume, wakitoa siri ya chama hadharani kwa ajili ya kujenga mtandao kwa watu, bado nao ni wana CCM?
Inauma sana. Chama sasa kimebaki kama mti mkavu ambao umeliwa ndani na kubaki magome tu. Ni dahiri utaanguka. Kama sio leo basi kesho. Kitu gani cha kuufanya usianguke? Mbona umeshakwisha kwa kuliwa na mchwa watu, usiku na mchana?
Kulisema ama kuliona hili bado kunahitaji elimu ya Chuo Kikuu? Nani anayefurahishwa na hali inayoendelea ndani ya chama? CCM leo imebaki kidogo tu kuanguka. Na wale wenye mapenzi mema ndio watakaoumia, maana wenzao, wale wanafiki watahamia kwenye vyama vyao walivyoanzisha, ama vilivyoanzishwa na wale wanaofanana nao.
Wamebaki wana CCM usoni wakivaa skafu na kofia, wakati mioyoni mwao ni wapinzani wa kutupwa, ndio maana hawapendi kuona wanapatana, wanafanya kazi pamoja. Ni roho ngumu tu, ila hata leo hii, Mwenyekiti wao, Jakaya Kikwete, ambaye pia ni Rais wa Jamhuli ya Muungano wa Tanzania, angeinua mikono juu na kusema ameshindwa.
Anashindwa kufanya hivyo, akikumbuka imani kubwa kwa Watanzania juu yake, hivyo anajipa moyo wa kuendelea na mapambano. Hii ndio Tanzania ya leo. Hii ndiyo CCM ya Muasisi wa Taifa letu, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na kizazi kipya cha leo.
Mbele za watu wanasema kidumu chama cha Mapinduzi, wakati vichochoroni wanasema watajuta kutufahamu. Katika hili, waungwana wamekubali kuiua CCM, wakiona kupo watakapokimbilia. Tukutane wiki ijayo.
kambimbwana@yahoo.com
No comments:
Post a Comment