KELVINA JOHN
Mwanamke aliyeacha Jeshi kwa ajili ya sanaa
WAHENGA walikuwa na semi zao ambazo zilikuwa na maana sana. Kati ya hizo, upo ule wa ‘Umdhaniaye ndiye kumbe siye’, huu unastahili kabisa kupigiwa mfano kwa Kelvina John.
Je, unajua kwa nini mwandishi wa makala haya anatolea mfano wa usemi huo kwa Kelvina? Hiyo ni kutokana na kuamua kuvua gwanda za Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) kwa ajili ya kujikita katika kucheza filamu, fani ambayo anaendeshea maisha yake kwa sasa.
Katika mahojiano, Kelvina alisema uamuzi wake huo ulitokana na uthubutu wake kwa sababu kazi hiyo ya kuwa muigizaji na mtengeneza (Prodyuza) filamu alikuwa akiipenda tangu utoto.
“Maisha ni kujaribu, inakupasa mtu kujaribu na hasa kwa kile unachokipenda na hakika utafanikiwa kwa sababu utakifanya kwa ufanisi wa hali ya juu, ndivyo ilivyojitokeza kwangu na kufikia uamuzi wa kuachana na kazi ya Jeshi na kujikita katika filamu.
“Ingawa nilipata wakati mgumu kuanzia katika Jeshi, lakini namshukuru Mungu hivi sasa nafanya kile ambacho nafsi yangu inapenda na naweza kuendesha maisha yangu kutokana na kazi hii ya kuandaa na kucheza filamu,” ndivyo alivyoanza kuzungumza Kelvina.
Kwa wasiomfahamu vema, Kelvina John ni muandaaji wa filamu (Prodyuza) ambaye alianza kujikita katika fani hiyo mwaka 2000 kwa kuandaa filamu yake ya kwanza kabisa ambayo aliamua kuiita Mtazamo.
Ingawa pia na yeye ni muigizaji, lakini anapenda zaidi kufanya kazi ya uandaaji, kazi ambayo hapa nchini imekuwa ikifanywa zaidi na wanaume na ndiyo maana upo uwezekano mkubwa kabisa akawa ni mwanamke pekee aliyeamua kujiiingiza katika fani hiyo ya uandaaji.
Pengine ujasiri huo umetokana na kuwa mwajiriwa wa Jeshi la Wananchi (JWTZ) ambaye alihitimu mafunzo na kupewa namba ya kazi 2712MTM na kupangiwa kazi katika kikosi namba 312 KJ Lugalo, kabla ya kuamua kuvua gwanda na kujikita katika filamu.
Katika mahojiano yake na Mtanzania, Kelvina alisema aliamua kuachana na kazi hiyo ya jeshi aliyoifanya kwa uadilifu ili akafanye kazi ya kuandaa na kuigiza filamu kwa sababu ni kitu kilichokuwa moyoni mwake tangu utoto.
“Ki ukweli katika maisha kila mmoja ana jambo ambalo anapenda, kwa sababu siku zote mimi nilikuwa naipenda fani hii, hata nilipokuwa jeshini nilihisi kama bado moyoni mwangu kuna jambo napungukiwa.
“Kwa sababu sikutaka kuidhulumu nafsi, niliamua ‘kusarender’ kazi ya jeshi na kuamua kujikita zaidi katika kuandaa filamu sambamba na kuigiza, kazi ninayoifanya hadi leo inayoniingizia kipato na kufanya nitatue matatizo yangu,” alisema.
Alisema aliamua kujitoa Jeshini mwaka 2003 baada ya kuona kazi yake ya kwanza aliyoandaa mwenyewe ambayo aliiita Mtazamo ikifanya vizuri, hivyo kuona ipo haja kutumia muda zaidi katika fani hiyo.
Kwa sababu inafahamika kazi hiyo ya Jeshi ni ‘bize’ sana kama angeendelea kuifanya, basi asingekuwa na muda wa kutosha kuandaa filamu zake, ndipo alipoamua kujivua gamba.
Mpaka sasa amefanikiwa kuandaa filamu tano, ikiwamo ambayo iko katika mchakato wa mwisho wa maandalizi ambayo inaitwa Leave or Die. Ni filamu ya action iliyowashirikisha mastaa kibao wa fani hiyo na kati yao mbali ya yeye mwenyewe, yupo Anti Fifi, Winter, Shilole na wengine.
Nyingine ambazo Kelvina amekwishatoa ni ile ya Penzi la Baba, Machozi na The Dadaz, ambayo aliitoa mwaka juzi. Aliwataka wanawake kuwa na uthubutu wa maamuzi ya mambo yao ili kufikia ndoto wanazohitaji, kwani hakuna lisiloshindikana endapo utakuwa na nia.
“Naomba wanawake wenzangu waache kubweteka, mimi unavyoniona dada yangu, naendesha maisha yangu kwa kazi hii, kwani imeniwezesha kuwapeleka watoto wangu wawili shule ambao Mungu amenijaalia.
“Na sasa nimeanza ujenzi wa kibanda cha kuishi huko jijini Mwanza, ambako ndiko ninapotokea, hivyo wale wenye mtazamo hasi juu ya kazi hii waachane nao kabisa,” alisema.
Akizungumzia maisha binafsi nje ya shughuli hizo za uandaaji wa filamu pamoja na kuvua kwake gwanda za Jeshi, Kelvina anasema yeye ni mama wa watoto wa kike wawili aliobahatika kuwapata kati ya miaka minane iliyopita.
Hata hivyo, ilimlazimu kuachana na mumewe ambaye naye alitaka kumtia kiwingu kutokana na kutokubaliana naye kujihusisha na kazi hizo za uandaaji filamu, jambo ambalo hakukubaliana nalo ingawa awali alifanya hivyo.
“Kwa kweli hii ni sehemu ya changamoto katika maisha, namshukuru sana Mungu kuendelea kunipa ujasiri, hasa baada ya kupitia wakati mgumu na kufikia uamuzi wa kuachana na mume wangu ambaye hakuridhia nifanye kazi hii,” alisema.
Kwa sasa anaishi Mbezi jijini Dar es Salaam na ni mtoto wa kwanza katika familia yao ya watoto wanne, huku akiwa ndiye mtoto wa kike pekee. Akizungumzia ushirikiano anaoupata katika familia, alisema hakuna, kwa sababu hawafurahii fani aliyojikita.
“Baba yangu hataki hata kidogo nifanye kazi hii, yeye alitamani sana niwe ‘Air Hostess’ kwani ndiyo fani aliyonipeleka kusoma kabla ya mimi kuikacha na kujiingiza katika Jeshi, ingawa hakuvutiwa nayo sana, lakini aliipenda baada ya kusikia nimehitimu mafunzo na kuajiriwa.
“Nilikuja kumtibua tena nilipoamua kuvua gwanda na kujikita katika filamu. Simlaumu sana kwa sababu najua yeye, familia, ndugu na jamaa bado wana mtazamo hasi wa kazi ninayoifanya, lakini nataka niwaonyeshe kwamba sivyo wanavyofikiria.
“Ndio maana nahitaji kufanya mambo makubwa katika fani hii yatakayonifanya niwe msanii mkubwa ninayetambulika ndani na nje ya nchi na hapo nafikiri wataelewa nini nafanya na sasa nimeishaanza kuwaonyesha, hasa nilipofanikisha kumiliki kampuni yangu ya ‘Production’ ya kazi za filamu inayoitwa KJ Production,” alisema.
Kila kazi inakabiliwa na changamoto mbalimbali. Je, unajua fani hii ya filamu inakabiliwa na changamoto gani?
“Changamoto kubwa tunazokabiliana nazo katika fani hii hapa kwetu ni kama tatu hivi: Sehemu za kuigizia, wasanii wengi ni wasumbufu, hasa baada ya kulewa sifa, hivyo kitu unachotakiwa kufanya siku mbili inaweza kuchukua hata wiki, soko la kazi zetu na tatizo la wizi wa kazi ni kubwa mno, tunaomba Chama cha Hakimiliki (COSOTA) kisimame imara, wasanii tunaumizwa sana hatufaidiki vilivyo,” alisema.
Ushauri wake kwa Serikali, watambue vema umoja wao waliounda unaoitwa Tanzania Films Federation (TAFF) na kuupa nguvu uweze kufanya kazi ipasavyo pengine utasaidia kuzuia wimbi la wizi wa kazi zao.
Lakini kwa upande wa wasanii wenzake, aliomba kujenga tabia ya kuheshimiana, kushirikiana na kuifanya kazi hiyo kwa ufanisi kwa maendeleo yao binafsi na Taifa kwa ujumla. Huyo ndiyo Kelvina John.
xxxxxxMWISHO
No comments:
Post a Comment