FIESTA 2012 DODOMA NA MOROGORO
Linah Sanga, akifanya mambo
Shetta akifanya mambo jukwaaani.
Na Kambi Mbwana, Dar
es Salaam
MASHABIKI wa muziki wa mkoani Dodoma, Septemba 14, walipata burudani za
aina yake katika Uwanja wa Jamhuri, lilipofanyika tamasha la Fiesta 2012,
lilioanza kutimua vumbi mapema mwezi uliopita, mkoani Kilimanjaro.
Mbali na Dodoma, tamasha hilo pia liliendelea katika Uwanja wa Jamhuri mjini
Morogoro, Jumapili ya Septemba 16, huku mashabiki wao wakibaki na hara mtindo
mmoja kutokana na tamasha hilo.
Wasanii ambao walitoa burudani katika tamasha la Dodoma na
Morogoro ni pamoja na Recho, Dayna, Linah, Mwana FA, Godzilla, Shetta, Stamina,
AT, Juma Nature, Diamond, Rich Mavoco na Ben Pol.
Mbali na wasanii hao wanaokubalika hapa nchini, pia wasanii
wachanga kama kawaida walianza kutoa burudani katika uwanja huo wa Jamhuri Dodoma, ikiwa ni utangulizi wa tamasha hilo na kiu ya kuibua wasanii wapya.
Burudani hizo zilianza jioni kwa wasanii wachanga kupanda
jukwaani kutangaza vipaji vyao katika tamasha linaloingiza watu wengi kwa
wakati mmoja, jambo ambalo linasababisha uwanja kujaa pande zote.
Kila msanii mchanga wa Morogoro na Dodoma, walikuwa na shauku ya kufanya vyema
kwa kuimba nyimbo moja nzuri, ikiwa ni dalili njema ya kutangaza cheche zao kwa
wadau wao katika uwanja huo.
Mara baada ya kumaliza kwa taratibu za burudani za wasanii
wachanga, moto ulianza kwa kuwapa nafasi washindi watatu wa Super Nyota, wakiongozwa
na Young Killer, mwimbaji mdogo mwenye makali ya kutisha.
Wasanii hao wamewekwa katika tamasha hilo
kama sehemu ya kuonyesha cheche zao, baada ya kupatikana katika shindano la
kusaka vipaji, ikiwa pia ni utangulizi wa ufunguzi wa tamasha hilo la Fiesta.
Baada ya kumaliza kwa wasanii hao watatu wa Super Nyota,
msanii aliyeibukia mkoani Morogoro na wimbo wake ‘Mafungu ya Nyanya’, Mwanaisha
Said, maarufu kwa jina la ‘Dayna’ alipanda jukwaani akifanya vitu vya aina
yake.
Dayna kwanza aliwatanguliza madansa wake walioingia jukwaani
kwa mbwembwe za aina yake, wakicheza na kujipanga kishujaa na kupandisha
Bendera ya Taifa ya Tanzania,
wakifuatiwa na kupiga wimbo wa Taifa.
Wakati wanakatisha kuimba wimbo huo, Dayna alipanda
jukwaani, akisababisha shangwe kwa mashabiki wengi uwanjani hapo, wakifurahia
alivyojipanga katika shoo yake kwenye tamasha hilo.
Alipomaliza kuimba nyimbo zake, ukiwamo ule wa Mafungu ya
Nyanya, Nivute Kwako na nyinginezo, mwanadada huyo alishuka na kupanda jukwaani
kwa msichana kutoka Tanzania House of Talents (THT), Reyker, akifuatiwa na
Rehema Sundi pamoja na Recho, anayetamba na wimbo wake wa Kizunguzungu, Upepo
na huu wa Nashukuru Umerudi unaofanya vizuri kwa sasa.
Recho anatamba katika chati za muziki kutokana na umahiri
wake wa kushambulia jukwaa, huku akitokea kwenye taasisi hiyo ya kulea na
kukuza muziki ya THT, iliyoibua wasanii wengi wenye uwezo wa kutisha.
Mara baada ya mwanadada huyo kumaliza kuimba, alimuachia
Ommy Dimpozi kuendelea kushusha burudani. Hata hivyo, Ommy ni kama
alipanda kwa mkosi, maana umeme ulisumbua kwa dakika kadhaa.
Cha kushangaza ni kwamba, licha ya umeme kusumbua uwanjani
hapo kwa dakika kadhaa, lakini Ommy aliendelea kushangiliwa na wadau kuimba kama kawaida, hivyo kuonyesha kuwa msanii huyo
anakubalika kupita kiasi.
Kitendo cha kumaliza kuimba kwa mkali huyo aliyeacha
historia mkoani Dodoma,
alipanda jukwaani Rich Mavoco, akifuatiwa na Stamina, msanii aliyetingisha
uwanja mzima kwenye shoo hiyo.
Wasanii wengine waliofuata kutoa burudani katika tamasha hilo ni Shetta, Ben Pol,
Linah, Mwana FA, aliyesindikizwa na AY, ambaye hata hivyo hakuwa kwenye ratiba
ya kupanda jukwaani kutoa burudani.
Msanii ambaye pia atakumbukwa ni AT aliyepanda jukwaani mara
baada ya kushuka wakali wa Hip Hop na R&B Ben Poli, yeye alipanda jukwaani
na kuwashawishi mashabiki wamsikilize na kucheza nyimbo zake.
Wengi katika shoo kubwa kama hizo hushindwa kuwafanya watu
wacheze, hasa hawa wa mduara kama AT, anayetokea mjini Zanzibar.
Shoo ya Dodoma
ilimalizwa na Juma Nature usiku wa manane, baada ya kumaliza wakali wote,
akiwamo Godzilla, mkali mwenye maskani yake mitaa ya Salasala.
Utaratibu kama huo ulionekana pia katika mji wa Morogoro,
ambapo mashabiki wengi walionekana kupagawa kabla ya shoo hiyo wakiwachekea
wasanii na kujipanga kwa ajili ya kuingia kwenye shoo hiyo.
Hata hivyo, mashabiki walipoingia kwenye uwanja huo wa
Jamhuri mjini Morogoro, walikuwa wazito sana
kucheza na kupagawa kama ilivyokuwa kwa wakazi na mashabiki wa mkoani Dodoma.
Fiesta inaandaaliwa na Kampuni ya Prime Time Promotion
pamoja na Clouds Media Group, likifanyika kila mwaka. Kwa mwaka huu, Fiesta
ilianza kutimua vumbi katika mji wa Moshi, mkoani Kilimanjaro.
Katika kila mkoa wanapofanya shoo hiyo, kunatanguliwa na
kazi za kijamii, ikiwamo kutembelea vituo vya watoto yatima na kuwapa misaada
ya aina mbalimbali pamoja na kupata fursa ya kubadilishana nao mawazo.
Kwa mkoa wa Dodoma, wasanii
na waandaaji wa tamasha hilo walitembelea kituo
cha watoto yatima kinachojulikana kama Kijiji
Cha Matumaini, kilichoanzishwa rasmi mwaka 2002.
Usiku wa shoo hiyo ulifunguliwa na Mkuu wa Mkoa, Rehema
Nchimbi, wakati ile ya Morogoro ilihudhuliwa pia na Mkuu wa Mkoa wake, Joel
Bendera, ambapo pia wakuu hao husisitiza suala la amani kwa tamasha hilo.
Mikoa iliyofuata kwa burudani hiyo ni pamoja na Tanga,
Musoma mkoani Mara, Shinyanga, Mwanza, Dodoma,
Morogoro, huku wiki hii likipangwa kufanyika jana Ijumaa katika mkoa wa Mbeya,
wakati kesho Jumapili tamasha hilo
pia litafanyika mkoani Iringa, Uwanja wa Samora.
0712 053949
0753 806087
Mwisho
No comments:
Post a Comment