JUMATANO ya wiki hii nilikuwa miongoni mwa wadau wa sanaa waliohudhuria kikao cha Kamati ya Huduma za Kudumu ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania , kilichoongozwa na Mwenyekiti wake Jenista Mhagama.
Kikao hicho kilichohuduriwa pia na wasanii wa aina mbalimbali, kilifanyika katika viungwa vya Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), kikiwa na maana kubwa ya kujadili masuala mbalimbali ya sanaa na wasanii nchini.
Waandishi wa habari wakiserebuka.
Kikao hicho kilikuja wakati muafaka. Wakati ambao kwa miaka kadhaa sasa, bado wasanii wamekuwa wakiishi maisha ya kubahatisha huku wengine wakiindelea kuishi maisha mazuri kwa kupitia migongo ya wasanii.
Mengi yalisemwa. Wasanii wengi walichangia pamoja na wajumbe ambao ndio wabunge na wageni waarikwa. Inasikitisha sana . Kwani kwa kiasi kikubwa, matatizo mengi yalihjitokeza, huku chanzo chake kikiwa ni BASATA na ndugu zao COSOTA.
Hata hao wezi wanaodaiwa kuwapo, ilionekana dhahiri wanabebwa na wakubwa wao, ukizingatia kuwa BASATA ina uwezo wa kuwa wakali kwa ajili ya kuwakomboa watoto wao, yani wasanii ambao kwa Tanzania wanaishi kama omba omba.
Licha ya kuwa na vipaji vya hali ya juu, lakini wanachopata ni sifuri. Ni kutokana na hilo , nadiliki kusema kuwa ipo haja ya Serikali, kupitia Wizara yake ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, ili kuokoa maisha ya wasanii.
Kuvunjwa huko kunatokana na taasisi hizo kushindwa kufanya kazi zake kama inavyotakiwa, licha ya kupewa memo na wasimamizi wa sanaa kwa ujumla. Ndio, ingawa kwa COSOTA wao wanaweza kuyumba na msimamo wa Serikali, yani kuripoti kwa Wizara tofauti, kama ile ya Viwanda na Biashara pamoja na Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo.
Pamoja na hayo, bado hainifanyi niamini kuwa COSOTA na BASATA wanaweza kukomboa maisha ya wasanii wetu. Kwa sasa uwezo huo hawana. Maana kwa miaka kadhaa wamekuwa wakifanya kazi kwa kuleana zaidi badala ya kusimama kwenye ukweli.
Angalia, ukweli huu umedhihirika zaidi, maana viongozi hao wa COSOTA waliweza kuingia mitini, japo walijua kuwa walitembelewa na Serikali yao , iliyowekwa madarakani kihalali, huku ikiongozwa na watu makini.
Jamani, hakuna haja ya kulumbana. Hapa hakuna haja ya kuogopana. Kwanini BASATA waachwe na ndugu zao COSOTA? Kwa wale waliokwenda katika mjadala huo watakubaliana na mimi. Malalamiko mengi yalielekezwa kwao.
Usimamizi wao ni mdogo zaidi. Kuingizwa katika biashara za kujinyoji hiyo ndio kazi yao , hata kama wanajua hazina umuhimu kwa Watanzania. Kwa mfano, BASATA kuingizwa kwenye tuzo za Kilimanjaro Music Award huo ni umbumbumbu.
Tuzo hizo zinayumba. Hazina maana. Wasanii bora wanaachwa na wale wabaya wanapata tuzo. Sasa kwanini washiriki? Hawaoni ni kuwayumbisha Watanzania? Haya ni maswali ambayo majibu yake ni rahisi, endapo viongozi watajivua gamba.
Hayo yatakwisha kama viongozi hao watakubali kuwajibika. Moja ya sera ya uongozi bora ni kusimama kwenye ukweli kwa ajili ya manufaa ya watu wako. Inapotokea mambo yanakwenda tofauti, huo ni wizi.
Tuuseme hadharani, maana vikao kama hivyo havitakuwa na maana kama yanayojadiliwa yanaachwa na wale wezi kiuendelea kula raha. Inasikitisha mno. COSOTA wao kushiriki kwenye kampeni za mtu mmoja kuna nini ndani yake?
Wasanii kuendelea kuibiwa wakati wao wapo inaonyesha wameshindwa kazi. Kuyasema haya ni lazima kwa faida ya kizazi cha sanaa. Kuna haja gani msanii kuimba pasi kupata chochote cha maana?
Kwanini maisha yake ya sanaa asiyatumie kwenye kilimo? Nadhani hili la kuvunjwa kwa mabaraza hayo na kupewa kazi watu wengi wengine kutachangia kwa kiasi kikubwa kuibua ari ya utendaji kwa wasanii na wasimamizi wao.
Ikumbukwe kwamba sanaa ni kazi na inaweza kuleta utajiri mkubwa kwa Taifa. Nchi za wenzetu wao wanafanikiwa kwa kupitia ulingo huo wa sanaa. Ndio, maana nasema katika majumuisho ya kikao hicho, ipo haja ya viongozi waliopo wa BASATA na ndugu zao COSOTA wawekwe pembeni kama wameshindwa wenyewe kuwajibika.
Huu sio wakati wa kuoneana haya. Tusimame kwenye ukweli na hapana shaka, Jenista Mhagama, mwenyekiti wa kamati hiyo ya Huduma za Jamii pamoja na Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo watapata dawa hiyo kwa manufaa ya Taifa.
Mungu ibariki Tanzania
Mungu wabariki wasanii wetu
0712 053949
0753 806087
No comments:
Post a Comment