Pages

Pages

Thursday, September 12, 2013

Temeke na Mjini Magharibi kumenyana kesho nusu fainali Copa Coca-cola kwa wachezaji chini ya miaka 15


Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
Temeke na Mjini Magharibi zinapambana kesho (Septemba 13 mwaka huu) katika mechi ya nusu fainali ya michuano ya Copa Coca-Cola kwa vijana wenye umri chini ya miaka 15 itakayofanyika Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, jijini Dar es Salaam.

Boniface Wambura, Msemaji wa TFF
Msemaji wa Shirikisho la Soka nchini TFF, Boniface Wambura, alisema kuwa timu hizo zimetinga hatua hiyo baada ya kushinda mechi zao za robo fainali ya michuano hiyo zilizochezwa leo (Septemba 12 mwaka huu) asubuhi kwenye uwanja huo huo.


Wakati Temeke imetinga hatua hiyo baada ya kuilaza bao 1-0 Iringa lililofungwa dakika ya 18 na Ramadhan Mohamed, Mjini Magharibi imeing’oa Mtwara kwa ushindi wa bao 1-0.


Robo fainali nyingine zinachezwa leo (Septemba 12 mwaka huu) jioni kwa Kilimanjaro kuvaana na mabingwa watetezi Morogoro huku Arusha ikioneshana kazi na Ilala.


Katika hatua nyingine, Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limetoa Hati ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC) kwa Watanzania wawili kucheza mpira wa miguu nchini Afrika Kusini.


Wachezaji hao; Robert Kobelo na Mohamed Ibrahim wamepewa hati hizo baada ya kuombewa na Chama cha Mpira wa Miguu Afrika Kusini (SAFA) kama wachezaji wa ridhaa ili wajiunge na klabu ya Cacau United ambayo timu yake inacheza Ligi Daraja la Pili katika Wilaya ya Cacau.


Naye mchezaji Said Maulid aliyejiunga na Ashanti United akitokea nchini Angola msimu huu amepata ITC ambayo sasa inamwezesha kuchezea timu hiyo katika mechi za Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) inayoingia mzunguko wake wa tatu keshokutwa (Septemba 14 mwaka huu).


Aidha, Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Eliud Mvella amejiondoa kwenye mchakato wa uchaguzi uliopangwa kufanyika Oktoba 27 mwaka huu.

Mvella amemwandikia barua Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF, Hamidu Mbwezeleni akielezea uamuzi wake huo pamoja na mambo mengine umetokana na kile alichodai kuwa Kamati hiyo haikumtendea haki kwa kumwondoa.


Mbwezeleni amekiri kupokea barua hiyo, na kuongeza kuwa licha ya uamuzi huo wa Mvella aliyekuwa ameomba kuwania ujumbe wa Kamati ya Utendaji kupitia Kanda Namba Saba ya mikoa ya Iringa na Mbeya, bado suala lake litasikilizwa na Kamati ya Maadili ya TFF kwa ajili ya hatua zaidi.


Kamati ya Mbwezeleni ilimuondoa Mvella katika kinyang’anyiro hicho kwa kushindwa kuheshimu Kanuni za Uwajibikaji wa Pamoja (collective responsibility) baada ya kushiriki kufanya uamuzi ndani ya Kamati ya Utendaji ya TFF bila ya kutaka msimamo wake wa kupinga uwekwe kwenye muhtasari na baadaye kuupinga uamuzi huo akiwa kwenye uongozi wa mkoa.


Pia TFF imesema kuwa mechi za nyumbani za timu ya Kanembwa JKT ya Kigoma iliyoko Ligi Daraja la Kwanza (FDL) sasa zitachezwa katika Uwanja wa Kawawa badala ya ule wa Lake Tanganyika.


Uamuzi wa kuhamishia mechi hizo Uwanja wa Kawawa ulioko Ujiji umetokana na Uwanja wa Lake Tanganyika kutumiwa na Serikali katika Operesheni Ondoa Wahamiaji Haramu inayoendelea nchini kwa sasa. Uwanja huo hivi sasa unatumika kuhifadhi wahamiaji hao.

No comments:

Post a Comment