Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
NYOTA wa muziki wa kizazi kipya maarufu kama Bongo Fleva aliyepatia makali yake katika taasisi ya kukuza na kulea ya vipaji ya Tanzania House of Talents (THT), Mwasiti Almas, amesema kwamba mwaka huu wa 2013 lazima apate mtoto, ingawa hakumtaja mtu ambaye yupo tayari kuzaa naye, akisema kuwa itabaki kuwa siri yake.
Mwasiti aliyasema hayo, wakati akizungumza na wasanii wenzake bila kujua kuwa mahali apokuwapo kulikuwa na chanzo chetu cha habari, ambapo hata hivyo aliwasihi maswahiba wake kuificha siri hiyo hadi itakapokuwa tayari.
Mwasiti anayetamba na wimbo wake wa 'Mapito', ameonekana kuwa moto wa kuotea mbali kutokana na kufanya kazi ya maana na kutishia usalama wa wasanii wenzake wa kike wanaotamba katika tasnia hiyo ya muziki wa kizazi kipya.
“Hakika mwaka huu lazima nizae maana nimeshapanga hivyo na nitashukuru kama Mungu atakubali dua yangu hii nikiamini kuwa ni hatua kubwa zaidi kwa maisha yangu.
“Nimekuwa nikijipanga na kutamani suala hili litimie katika kipindi cha mwaka huu, hivyo nitashukuru mno kwa hatua hii,” alisema Mwasiti.
Nyimbo nyingine zilizowahi kuimbwa na Mwasiti ni pamoja na Kisa Pombe, ambapo pia lengo lake lingine kwa mwaka huu ni kuifungua rasmi ofisi yao ya wasanii wanaotokea mkoani Kigoma, huku yeye akiwa kiongozi wao.
No comments:
Post a Comment