Pages

Pages

Friday, January 25, 2013

Mganga Mkuu zahanati ya Saunyi Kilindi akamatwa akiiba dawa



Mkuu wa Wilaya Kilindi, Selemani Liwowa

Na Rahimu Kambi, Kilindi
Mganga Mkuu wa Zahanati ya Kata ya Saunyi, Tarafa ya Mgela, wilayani Kilindi mkoani Tanga, Rashid Mhande, anasakwa na porisi baada ya kufumwa akiiba dawa zenye thamani ya zaidi ya Sh Milioni tano.

Tukio hilo lilitokea juzi, baada ya Mhande kufumwa akiiba dawa kwa kutumia toroli la Zahanati hiyo, kabla ya kuzihamishia kwenye pikipiki yake kwa ajili ya kuzipeleka anakojua yeye.

Akizungumza jana usiku, Mkuu wa Wilaya ya Kilindi, mkoani Tanga, Selemani Liwowa, alisema kwamba hadi sasa mganga huyo hajulikani alipo, huku akiagiza asakwe popote alipo ili afikishwe kwenye vyombo vya dola.

Alisema hospitali hiyo imekuwa na malalamiko mengi kutoka kwa wananchi wakisema mara kadhaa wanaambiwa hakuna dawa, jambo linalowapa wasiwasi mkubwa.

“Tunashukuru kubainika kwa mganga huyo aliyekuwa anaiba dawa katika zahanati ya Saunyi, jambo ambalo hakika limetusikitisha mno kwa watumishi kama hawa.

“Baada ya kubainika, baadhi ya wananchi walianza kumpiga, hivyo kufanikiwa kukimbia, ambapo alipofika polisi alisingizia amepigwa na wafugaji, hivyo kupewa matibabu Makao Makuu ya wilaya, hata hivyo alipoona atagundulika janja yake kutoka kwa wananchi na serikali, aliamua kutoroka kusipojulikana," alisema Liwowa.

Kwa mujibu wa Liwowa, ameagiza porisi wamsake mhalifu huyo ili sheria zichukuwe mkondo wake kwa watumishi wanaohujumu Taifa na kuiletea aibu serikali kwa vitendo vyao visivyokuwa vya kiungwana.

No comments:

Post a Comment