Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
MZUNGUUKO wa pili wa
Ligi Kuu ya Vodacom (VPL), kuwania
ubingwa wa Tanzania Bara unaanza kesho (Januari 26 mwaka huu) kwa raundi ya 14
ambapo timu 12 kati ya 14 za ligi hiyo zitakuwa uwanjani.
Mabingwa watetezi Simba watakuwa wenyeji wa African Lyon katika mechi itakayochezwa saa 10 jioni kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Hiyo itakuwa mechi ya kwanza kwa kikosi cha Simba tangu kiliporejea kutoka Oman kwenye ziara ya mafunzo.
Mwamuzi wa kimataifa
Israel Mujuni ndiye atakayechezesha mechi hiyo ambapo African Lyon inatarajiwa
kuongozwa na Kocha Charles Otieno baada ya kusitisha kibarua cha Pablo Velez
kutoka Argentina kutokana na kufanya vibaya katika mzunguko wa kwanza.
Uwanja wa Manungu ulioko
Turiani mkoani Morogoro wenye uwezo wa kumeza watazamaji 8,000 ndiyo
utakaohimili vishindo vya mechi kati ya Polisi Morogoro na wenyeji Mtibwa
Sugar. Polisi Morogoro ambayo ni ya mwisho katika msimamo wa VPL ililazimisha
suluhu katika mechi ya mzunguko wa kwanza.
Coastal Union ambayo
kwenye dirisha dogo imesajili wachezaji sita akiwemo Mzimbabwe Tinashe
Machemedze itaoneshana kazi na wana-Tanga wenzao Mgambo Shooting kwenye Uwanja
wa Mkwakwani, jijini Tanga.
Timu zinazo katikati ya
msimamo wa ligi, Ruvu Shooting na JKT Ruvu zitapimana ubavu kwenye Uwanja wa
Mabatini ulioko Mlandizi mkoani Pwani ambapo sheria 17 zinazotawala mpira wa
miguu zitakuwa chini ya usimamizi wa refa Dominic Nyamisana kutoka Dodoma.
Wawakilishi wa Tanzania
kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho, Azam baada ya mechi za kirafiki nchini
Kenya wanarejea kwenye Ligi Kuu ya Vodacom kwa kuikaribisha Kagera Sugar ya
Kocha Abdallah Kibaden kwenye Uwanja wa Chamazi.
Ni mechi ya kulipa kisasi kwa Kagera Sugar baada ya kulala
bao 1-0 katika mechi ya mzunguko wa kwanza iliyochezwa Septemba 15 mwaka jana
Uwanja wa Kaitaba, mjini Bukoba.
Maafande wa Oljoro JKT
wanaanza kuchanga upya karata zao katika mzunguko wa pili kwa kuikaribisha Toto
Africans ya Mwanza kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sheikh Kaluta Amri Abeid,
jijini Arusha.
No comments:
Post a Comment