https://tpc.googlesyndication.com/simgad/8045142562622600543


Recent Post

Thursday, April 09, 2015

Mwendokasi watajwa chanzo cha ajali iliyoua 10 na kujeruhi 35 Handeni, Tanga

Na Mwandishi Wetu,Tanga
AJALI iliyoangamiza roho za watu 10 katika kijiji cha Mbweni Mkata, wilayani Handeni, mkoani Tanga, umetajwa kuwa chanzo cha ajali hiyo iliyohusisha gari ya Ratco na Ngorika zilizogongana baada ya gari ndogo aina ya Passo nayo kugongana na Ratco.
 Hali ilivyoonekana katika ajali ya magari matatu ambayo ni Ratco, Ngorika na gari ndogo ya Passo
Mkuu wa Kikosi cha Usalama barabarani mkoani Tanga, Abdi Issango, aliuambia mtandao wa Handeni Kwetu kuwa mwendo kasi ndio uliosababisha ajali hiyo na kusababisha vifo vya watu 10, wakiwamo madereva wawili na abiria wao nane.

Ajali hiyo ilitokea leo saa tano asubuhi ambapo awali Ratco iligongana na Passo ambapo pia ikajumlisha na basi la Ngorika lililokuwa linatoka Dar es Salaam kuelekea Arusha.

Majeruhi 35 katika ajali hiyo wamepelekwa katika Hospitali ya wilaya Korogwe (Magunga), Handeni na ile ya Mkata kwa ajili ya kuwapatia matibabu majeruhi hao.

Wanafunzi wanaosoma China wa Tanzania wachaguana

Viongozi Wapya waliochaguliwa katika Mkutano Mkuu wakiwa katika picha ya pamoja ikiwa ni kumbukumbu ya Uchaguzi huo.
Viongozi Wapya waliochaguliwa katika Mkutano Mkuu wakiwa katika picha ya pamoja ikiwa ni kumbukumbu ya Uchaguzi huo.
Wanafunzi wa Kitanzania wanaosoma Beijing China wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kumalizika kwa Mkutano Mkuu wa Jumuiya hiyo na kuwapata Viongozi wapya baada ya kuchagulia kwa kuongoza Jumuiya hiyo kwa mwaka 2015/2016.

Watatu wa Dar es Salaam, Songea na Bukoba wajishindia mamilioni kutoka Bayport Financial Services

Meneja Utawala wa Bayport Financial Services aliyezibwa macho, Evalyine Hall, akichagua koponi ya mmoja wa washindi wa Kopa Bayport kwa njia ya mtandao wa www.kopabayport.co.tz, inayoendeshwa na taasisi hiyo ambapo washindi watatu ambao ni Hyasint Mbunda (Songea), Phaustine Mbilinyi (Dar es Salaam) na Allen Bishubo (Bukoba), walipatikana na kila mmoja kushinda Sh Milioni moja. Kushoto ni Meneja Masoko na Mawasiliano wa Bayport, Ngula Cheyo na kushoto ni Msimamizi wa Michezo ya Kubahatisha, Humud Abdulhussein. Picha na Mpiga Picha Wetu.
 
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
WASHINDI watatu waliokopa fedha kwa njia ya Mtandao wa Taasisi ya Kifedha ya Bayport Financial Services, wamejishindia Sh Milioni moja kila mmoja, kutokana na shindano hilo lililoanzishwa maalum kwa ajili ya wateja wao waliomua kuutumia mtandao wao wa www.kopabayport.co.tz kupata huduma mbalimbali.

Washindi hao wamepatikana kutoka kwenye droo ya mwezi wa Aprili, iliyoendeshwa na Bayport Financial Services kwa kusimamiwa na Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania.

Meneja Utawala wa Bayport Financial Services Evelyine Hall katikati akisoma koponi ya mmoja wa washindi wa Kopa Bayport kwa njia ya Mtandao inayoondeshwa na taasisi hiyo ya kifedha. Kulia kwake ni Msimamizi wa Michezo ya Kubatisha Tanzania, Humud Abdulhussein na kushoto ni Ngula Cheyo, Meneja Masoko na Mawasiliano wa taasisi hiyo ya Bayport Financial Services.

Akizungumza katika droo hiyo, Meneja Masoko na Mawasiliano wa Bayport Financial Services, Ngula Cheyo, alisema kwamba washindi hao watatu wamepatikana baada ya kuamua kukopa kwa njia ya mtandao wao waliyouzindua mwezi uliopita.
Ngula Cheyo (katikati) ambaye ni Meneja Masoko na Mawasiliano wa taasisi ya kifedha ya Bayport Financial Services akizungumza jambo katika droo ya kutafutwa washindi watatu wa bahati nasibu inayoandaliwa na taasisi hiyo ambao kila mmoja alishinda Sh Milioni moja.

“Tuliamua kuanzisha huduma ya kukopa kwa njia ya mitandao tukiamini ni huduma rahisi inayoweza kuwafanya Watanzania wote wafurahie kwa pamoja na kukuza uchumi wetu, hivyo tukaona tufike mbali zaidi kwa kuchezesha droo yetu ya kuwapatia Sh Milioni moja washindi watatu kila mwezi.

Wednesday, April 08, 2015

Zakhem FCna FFU SC kusaka Bingwa wa jumla michuano ya Ligi ya Mkoa Dar es Salaam

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
Baada ya kumalizika kwa michuano ya ligi ya mkoa wa Dar es salaam na kupata timu tatu zitakazouwakilisha mkoa katika michuano ya ligi ya mabingwa ya mikoa ya TFF,kesho Alhamis Aprili 09/2015,katika uwanja wa Karume jijini kutakuwa na mchezo wa fainali ya kumpata Bingwa wa jumla wa michuano ya ligi ya mkoa.
Msemaji wa DRFA Omary Katanga, pichani
Msemaji wa Chama cha Soka Mkoa Dar es Salaam (DRFA), Omary Katanga, alisema kwamba timu zitakazoumana katika fainali hiyo ni ZAKHEM FC dhidi ya FFU SC,ambazo zitashuka dimbani majira ya saa kumi jioni zikishuhudiwa na umati wa mashabiki waliokuwa wakiyafuatilia mashindano hayo tangu yalipoanza kutimua vumbi.

Kwa mujibu wa kamati ya mashindano ya chama cha soka mkoa wa Dar es salaam DRFA,timu zilizofanikiwa kuuwakilisha mkoa katika michuano ya ligi ya maabingwa ni pamoja na ZAKHEM FC,FFU SC na CHANGANYIKENI SC.

Mwenyekiti wa DRFA, Almas Kasongo,ameipongeza kamati hiyo ya mashindano kwa kusimamia vizuri uendeshaji wa ligi tangu ilipoanza.

Kuziona Twiga Stars na She-Polopolo ni Sh 2000 tu

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini TFF limetangaza viingilio vya mchezo kati ya timu ya Taifa ya Tanzania ya Wanawake (Twiga Stars) dhidi ya timu ya Taifa ya Zambia (She-Polopolo) kiingilio cha juu sh.5,000 kwa VIP na sh. 2,000 kwa majukwaa yaliobakia, mechi hiyo itachezwa ijumaa jioni saa 10 kwenye dimba la Uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.

Twiga Stars chini ya kocha mkuu Rogasian Kaijage imeendelea kujifua katika hosteli za TFF zilizopo Karume, kuhakikisha inaibuka na ushindi katika mchezo huo wa kuwnaia kufuzu kwa Michezo ya Afrika nchini Congo- Brazzavile mwezi Septemba mwaka huu.

Katika mchezo wa awali uliofanyika wiki tatu zilizopita jijini Lusaka nchini Zambia, Twiga Stars iliibuka na ushindi wa mabao 4-2 dhidi ya wenyeji Zambia, hivyo katika mchezo wa ijumaa kuhitaji ushindi wa aina yoyote tu ili kuweza kufuzu kwa fainali hizo.

TFF inawaomba wapenzi, wadau na washabiki wa mpira wa miguu nchini, kujitokeza kwa wingi siku ya ijumaa jioni uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam kuja kuwapa sapoti Twiga Stars watakapokuwa wanapeperusha bendera ya Taifa.

Wakati huo huo, timu ya Taifa ya Wanawake ya Zambia (She-Polopolo) inatarajiwa kuwasili usiku wa saa 7.25 kuamkia alhmisi kwa shirika la Ndege la Ethiopia wakiwa na msafara wa wachezaji 18 na viongozi saba na watafikia katika hoteli ya Tansoma iliyopo eneo la Gerezani Kariakoo.

Msafara wa Zambia (She-Polopolo) unaongozwa na mkuu wa msafara Lenny Khuwa, kocha mkuu Albert Kachinga, kocha msaidizi Kape Saili, kocha wa magolikipa Yona Phiri, daktari wa timu James Nyimbili, mchua misuli Conerlia Chazura, na meneja wa timu ni Besa Chibwe.

Wachezaji wanaotarajiwa kuwasili ni Rachel Nachula, Annie Kibanji, Chiko Nkhoma, Osala Kaleo, Joana Benai, Meya Banda (Nahodha), Misozi CR Chisamu, Jane Nshika Chalwe, Milika Limwanya, Mary Wilombe, Grace Chanda, Barbra Banda, Memory Mwaseba, Hazel Natasha Nali, Martha Tembo, Mary Mwakapila na Ireen Lungu.

Kesho jioni She-Polopolo wanatarajiwa kufanya mazoezi katika uwanja wa Taifa, uwanja ambao ndio utakaotumika kw amchezo huo.

Waamuzi wa mchezo huo kutoka nchini Uganda wanatarajiwa kuwasili leo mchana ambao ni  Ms Anna Akoyi , Ms Nakkito Nkumbi , Ms Jane  Mutonyi, na Ms Nabikko Ssemambo, Kamishina wa mchezo  Ms Nomsa Jacobeth Mhalangu kutoka nchini Afrika Kusini anatarajiwa kuwasili leo jioni.

TFF yammwagia sifa Leodgar Tenga

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini TFF Jamal Malinzi, amempongeza Bw Leodgar Tenga kwa kuchaguliwa kuendelea kuwa mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu barani Afrika (CAF).

Aidha Rais Malinzi ametuma salamu za pongezi kwa wajumbe  waliochaguliwa kuwa wajumbe wapya wa Shirikisho la Mpira wa Miguu baranai Afrika (CAF) na Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani FIFA.

Katika salamu hizo na nakala zake kutumwa kwa Rais wa CAF Bw. Issa Haytou na Rais wa FIFA Bw. Blatter, Malinzi amewatakia kila la kheri katika majukumu hayo mapya,na  kwa ajili ya maendeleo ya mpira wa miguu duniani.

Tenga amechaguliwa nafasi hiyo baada ya kuwa mgombea pekee kutoka kanda ya Afrika Mashariki aliyejitokeza kuwania nafasi hiyo na kuungwa mkono na nchi zote wanachama wa CECAFA.

Angalia picha mbalimbali za Hitma ya kumuombea marehemu Mzee Abeid Amani Karume

Mama Fatma Karume akiwasili katika viwanja vya Afisdi Kuu ya CCM Kisiwandui kwa ajili ya kuhudhguria Hitma na dua ya kumuombea Marehemu Mzee Abeid Amani Karume, iliofanyika leo Mjini Zanzibar.
Rais Mstaaf wa Zanzibar Dk Amani Abeid Karume akiwaili katika viwanja vya Afisi Kuu ya CCM kuhudhuria hitma ya Baba yake Marehemu Mzee Abeid Amani Karume, iliofanyika leo Mjini Zanzibar.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, akiwasili katika viwanja vya Afisi Kuu ya CCM na kupokelewa kwa na Askari wa JWTZ , akihudhuria Hitma ya Marehemu Mzee Abeid Amani Karume. Afisi Kuu.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Ali Mohamed Shein, akisalimiana na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Ndg Vuai Ali Vuai alipowasili katika viwanja vya Afisi Kuu ya CCM Kisiwandui Zanzibar kuhudhuria Hitma na Dua ya kumuombea Marehemu Mzee Abeid Amani Karume iliofanyika leo.

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania yamlilia Dr Mohamed Mhita

Hayati Dkt. Mohamed Mitha Mekuru Genzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania Dkt. Agnes Kijazi anasikitika kutangaza kifo cha aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu (mstaafu) Dkt. Mohamed Mhita kilichotokea siku ya Jumatatu tarehe 06 Aprili 2015 katika hospitali ya Agakhan jijini Dar es Salaam. 

Marehemu Dr Mohamed Mhita enzi za uhai wake, aliyesimama, aliyetarajiwa kuzikwa leo jioni wilayai Handeni, mkoani Tanga

Dkt. Mhita alikuwa Mkurugenzi Mkuu wa iliyokuwa Idara Kuu ya Hali ya Hewa kwa kipindi cha miaka 8 kuanzia 1992 hadi 1999 na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania kwa kipindi cha miaka 9 kuanzia 1999 hadi 2008. 

Dr. Mhita kwa kushirikiana na uongozi wa iliyokuwa idara Kuu ya Hali ya Hewa alishiriki katika kuishauri Serikali kuhusu kuanzishwa kwa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania kutoka iliyokuwa Idara Kuu ya Hali ya Hewa.

Pamoja na nafasi ya Mkurugenzi Mkuu pia alikuwa Mwakilishi wa kudumu wa Tanzania katika Shirika la Hali ya Hewa Duniani kuanzia mwaka 1992 hadi 2008. Alichaguliwa kuwa Mjumbe katika Baraza Kuu la Shirika la Hali ya Hewa Dunia kuanzia mwaka 1995 hadi 2007.
Alichaguliwa kushika nafasi ya Rais wa Jumuiya ya Hali ya Hewa katika Bara la Afrika (RA 1) kuanzia mwaka 1998 hadi 2007. Dkt Mhita alikuwa Rais wa ‘Tanzania Meteorological Society’ sambamba na nafasi nyingine nyingi mbalimbali alizoshika ndani na nje ya nchi. 

Akielezea baadhi ya mambo makubwa yatakayomfanya Dkt. Mhita aendelee kukumbukwa, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini Dkt. Agnes Kijazi alisema ‘Dkt. 

Mhita atakumbukwa kwa mchango wake mkubwa katika kuendeleza sayansi ya hali ya hewa hapa nchini, katika Bara la Afrika na Duniani kwa ujumla hususani katika ushiriki wake wa kuianzisha Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini kwa kuandaa dira (vision) na dhamira (mission) ya Mamlaka kwa kipindi cha miaka kumi na tano (15) kuanzia mwaka 2000 hadi 2015’.

Dkt. Mohamed Mhita ni mmoja kati ya wanasayansi waliokuwa zao la chuo kikuu cha Stolkholm, Sweden ambako alitunukiwa shahada ya hali ya hewa (BSc. Met) mwaka 1977. Kuanzia mwaka 1981 hadi 1984 alikuwa mafunzoni katika chuo Kikuu cha Reading, Uingereza ambako alitunikiwa shahada ya uzamivu (PhD). 

Hapa nchini alipata mafunzo ya Sekondari katika shule za Tanga na Kamrimjee zote zikiwa mkoani Tanga. Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania inajumuika na familia, ndugu, jamaa na marafiki katika kuomboleza msiba huu. Innalilah Wainnailaih Rajiun. 

Imetolewa na Monica Mutoni
Afisa Mahusiano wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania


LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...