https://tpc.googlesyndication.com/simgad/8045142562622600543


Recent Post

Saturday, March 21, 2015

Makamu wa Rais Dkt Mohamed Bilal ashiriki matembezi ya hisani ya kuchangia ujenzi wa Kanisa la Mt Dominic Savio wilayani Temeke

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akipokea zawadi ya picha yake iliyochorwa na Msanii, Florian Ludovic (hayupo pichani) kutoka kwa Mwenyekiti wa Kamati ya maandalizi ya matembezi hayo, Paroko wa Parokia ya Chang’ombe, Benedict Mushi, wakati wa hafla fupi ya matembezi ya hisani ya kuchangia ujenzi wa Kanisa la Kigango cha Mt. Dominic Savio, lililopo Temeke Mikoroshini,  matembezi hayo yamefanyika leo Machi 21, 2015 asubuhi kuanzia Chang’ombe Polisi hadi Temeke Mikoroshini, jijini Dar es Salaam.  Picha hiyo iliuzwa kwa mnada kiasi cha Sh. Milioni 2.5.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akishiriki na kuongoza matembezi ya Hisani kwa ajili ya kuchangia ujenzi wa Kanisa la Kigango cha Mt. Dominic Savio, lililopo Temeke Mikoroshini. Matembezi hayo yamefanyika leo Machi 21, 2015 asubuhi kuanzia Chang’ombe Polisi hadi Temeke Mikoroshini, jijini Dar es Salaam.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akimpongeza Mzee Thomas Wambura Kyangombe (miaka 99) baada ya kushiriki matembezi hayo ya hisani ya kuchangia ujenzi wa Kanisa la Kigango cha Mt. Dominic Savio, lililopo Temeke Mikoroshini. matembezi hayo yamefanyika leo Machi 21, 2015 asubuhi kuanzia Chang’ombe Polisi hadi Temeke Mikoroshini, jijini Dar es Salaam. 

Bondia wa Tanzania, Class Mawe apoteza pambano lake nchini Namibia

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
BONDIA Ibrahim  Class Mawe pichani mwenye rekodi ya namba moja nchini Tanzania na namba 216 kwa Dunia  amepoteza mpambano wake wa kwanza nchini Namibia kwa kupigwa kwa pointi na bondia Julius Indongo mwenye rekodi ya Namibia ni namba moja na duniani ni namba 76 kwa ubora.
Mpambano huo uliofanyika Machi 20 katika Ukumbi wa jijini Windhoek Country Club Resort, Windhoek, Namibia ulianza kwa kasi ya ajabu ambapo bondia Class alimkalisha chini Indongo na kuhesabiwa na mpambano kuendelea kwa mashambulizi ya zamu kwa zamu kila upande hata hivyo mpaka mwisho wa mchezo Class alipoteza mpambano huo kwa pointi

Mpambano huo ni wa pili kwa Class kucheza nje ya nchi baada ya ule wa kwanza kupigana nchini Zambia mwaka jana na kurudi na ubingwa wa WPBF Africa kabla ya kuchaguliwa kwenda kupigana nchini Namibia. Pia Class alimdunda bondia Cosmas Cheka na kunyakuwa mkanda wa U.B.O Africa na kumfanya amiliki mikanda miwili ya Africa.

Mpambano huo anaupoteza baada ya miaka mitano iliyopita kuwapiga mabondia mbalimbali Class anaenolewa na jopo la makocha linalongozwa na Habibu Kinyogoli 'Masta' Kondo Nassoro pamoja na kocha wa kimataifa wa mchezo wa masumbwi nchini Rajabu Mhamila 'Super D' ambaye umpa ushauli anapokuwa uringoni jinsi ya kukabiliana na mpinzani anaecheza nae

Friday, March 20, 2015

Timu ya Taifa ya mpira wa ufukweni yawasili salama nchini Misri

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Timu ya Taifa ya soka la Ufukweni (Beach Soccer) imewasili salama jijini Cairo nchini Misri tayari kwa mchezo wa marudiano dhidi ya wenyeji kuwania kufuzu kwa fainali za mataifa Afrika zitakazofanyika Visiwa vya Shelisheli.

Taarifa iliyotumwa katika vyombo vya habari na Msemaji wa Shirikisho la Soka nchini (TFF), Baraka Kizuguto, ilisema kuwa msafara wa timu ya soka la Ufukweni ulipokelewa na maofisa wa Ubalozi wa Tanzania waliopo nchini Misri,  pamoja na viongozi wa chama cha soka nchini Misri (EFA).

Leo jioni kikosi kinatarajia kufanya mazoezi mepesi, kabla ya kesho kufanya mazoezi ya mwisho katika uwanja utakaofanyika mchezo siku ya jumapili.

Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini TFF linaitakia kila la kheri timu ya soka la ufukweni katika mchezo wake wa marudiano siku ya jumapili dhidi ya Misri.

Katika hatua nyingine, fainali ya kumsaka Bingwa wa Ligi Daraja la Pili (SDL) inatarajiwa kufanyika siku ya jumapili katika uwanja wa Karume jijini Dar es salaam siku ya jumatatu Machi 23 mwaka huu kuanzia saa 10 kamili jioni.

Mchezo huo wa fainali utazikutanisha timu za Mbao FC ya Mwanza dhidi ya Kiluvya United FC ya Pwani, ambapo mshindi wa mchezo ndio atakua Bingwa mpya wa Ligi Daraja la Pili.

Jumla ya timu nne tayari zimeshapanda Ligi Daraja la Kwanza (FDL) kutoka Ligi Daraja la Pili (SDL) ambazo ni Kiluvya United ya Pwani, Mji Njombe ya Njombe, Mbao ya Mwanza na Mji Mkuu (CDA) ya Dodoma.

Thursday, March 19, 2015

Makamu wa Rais Dkt Bilal afungua mkutano wa washirika wa majenzi ya kijani Afrika Mashariki, jijini Arusha

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akihutubia wakati akifungua rasmi Mkutano mkuu wa kwanza wa Washirika Majenzi ya Kijani wa Afrika Mashariki, uliofanyika leo Machi 19, 2015 kwenye Hoteli ya Ngurdoto jijini Arusha.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akimkabidhi Tuzo, Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii, PSPF, Adam Mayingu, wakati wa ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa kwanza wa Washirika Majenzi ya Kijani wa Afrika Mashariki, uliofanyika leo Machi 19, 2015 kwenye Hoteli ya Ngurdoto jijini Arusha.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akimkabidhi Tuzo, Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Nehemiah Mchechu, wakati wa ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa kwanza wa Washirika Majenzi ya Kijani wa Afrika Mashariki, uliofanyika leo Machi 19, 2015 kwenye Hoteli ya Ngurdoto jijini Arusha.

Mdiwani wa Lindi Mjini wajifunza wilayani Bagamoyo

Diwani wa Kata ya Nachingwe, Lindi Mjini, Omary Chitanda (katikati) akiuliza swali kwa mtaalamu wa mradi huo
Diwani wa Kata ya Nachingwe, Lindi Mjini, Omary Chitanda (katikati) akiuliza swali kwa mtaalamu wa mradi huo.
*Taasisi ya Miradi na Maendeleo ya Miundombinu (UTT-PID) ilianza kazi zake Julai 1, 2013. Taasisi hii ilirithi kazi za miradi zilizokuwa zinafanywa na Taasisi mama yaani UTT.

Andrew Chale, aliyekuwa Bagamoyo
Baadhi ya Madiwani wa Manispaa ya Lindi Machi 17, wametembelea miradi mbali mbali ya UTT-PID iliyopo Dar es Salaam ikiwemo ule wa Bagamoyo wa New Mapinga Satellite.
Madiwani hao waliweza kujifunza mambo mbalimbali dhidi ya mradi huo ulivyoandaliwa na kufanya kazi na namna ulivyopangiliwa kwa ustadi mkubwa.

Katika ziara hiyo inayotarajia kumalizika Machi 19, mwaka huu. Madiwani hao wakiongozwa na Mstahiki Meya wa Manispaaa ya Lindi, Frank Magali alipongea juhudi za UTT-PID kwa kufanikisha ziara hiyo kwani wamejifunza mengi na pindi watakaporejea Lindi, watakuwa mfano wa kuigwa.

“Kule kwetu Lindi pia tuna mradi uliopo katika hatua mbaali mbali na UTT-PID tayari wamesha pima baadhi ya viwanja katika mfumo kama huu wa kisasa tunaojifunza hapa hivyo itatusaidia sana kwa sasa” alisema Meya Magali.
Diwani wa Kata ya Nachingwea, Manispaa ya Lindi, Omari Chitanda akielezea namna alivyojifunza kwenye mradi huo kwa wandishi wa habari (hawapo pichani)
Diwani wa Kata ya Nachingwea, Manispaa ya Lindi, Omari Chitanda akielezea namna alivyojifunza kwenye mradi huo kwa wandishi wa habari (hawapo pichani).

Kwa upande wake, Diwani wa Nachingwea, Omari Chitanda alieleza kuwa, wamepata kuielewa vyema UTT-PID na naamna ya ufanyaji wake wa kazi.

Said Uwezo na Julius Kisarawe kuvaana Machi 28 Ukumbi wa CCM Tandale

Na Mwandishi Wetu
Mabondia Julius Kisarawe kutoka 'Ndame Club' na Saidi Uwezo kutoka 'Mzazi GYM' watapanda uringoni march 28 kugombania ubingwa wa taifa wa kg 54 katika ukumbi wa manyara park uliopo CCM Tandale Manzese mpambano uho wa raundi kumi wenye upinzani wa hali ya juu utasindikizwa na mabondia mbalimbali kutoka katika kambi tofauti
ambapo bondia Ibrahimu Tamba atapambana na George Dimoso na Vicent Mbilinyo kutoka kwa 'Super D.

Boxing Coach' atapambana na Yusufu Mkari na kasimu Gamboo atakabiliana na Mustafa Dotto na Mohamed Kibanga atapambana na Bakari Dunda wakati Karim Mura  atamkabili Eddy Baguo siku hiyo kutakuwa na uzwaji wa DVD za ngumi  mabingwa wa Dunia akiwemo Manny Paquaio, Floyd Maywether, Roy Jones,Miguel Cotto,Linox Lewis, David Haye,Mohamed Ali na wengine wengi DVD hizo zilizoandaliwa kwa ubora wa hali ya juu zitakuwa zikiuzwa kwenye mpambano huo na Kocha wa Kimataifa wa mchezo huo. Rajabu Mhamila ‘Super D’, alisema kuwa kutakuwa na DVD ili kuweza kuwauzia mashabiki kwa ajili ya kujifunza Kanuni na Sheria za mchezo huo.
--

Semina ya madaktari kuhusu magonjwa ya ngozi yafanyika Dar es Salaam

 Mmoja wa waratibu wa Semina ya madaktari kuhusu magonjwa ya ngozi, Jesinta Mboneko, akimkaribisha mmoja wa washiriki hiyo, Muuguzi katika hospitali ya Mbezi Medical Clinic inayojishughulisha na magonjwa hayo, Sarah Nyabhenda, kwenye ukumbi wa semina hiyo katika hoteli ya Protea Cortyard, Upanga jijini Dar es Salaam, jana jioni.
 Baadhi ya washiriki wakianza kuingia kwenye semina hiyo
 Mkuu wa Idara Chuo Kikuu cha Tiba Muhimbili (MUHAS), Dk. Denis Russa akiwakaribisha washiriki kwa ajili ya kuanza rasmi semina hiyo. Picha zote na Bashir Nkoromo.

Rais Jakaya Kikwete atua Burundi kwa ziara ya kikazi ya siku mbili, pia kuhutubia EAC

Na Mwandishi Wetu, Burundi
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete jioni ya Jumatano, Machi 18, 2015 amewasili nchini Burundi kwa ziara ya kikazi ya siku mbili nchini humo. 
 Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akipokea Maua kutoka kwa watoto waliokuja kumlaki katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Bujumbura ambapo alianza ziara ya kikazi ya siku mbili.
 Rais wa Burundi Pierre Nkurunzinza akimkaribisha Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Bujumbura leo jioni.Rais Kikwete yupo nchini Burundi kwa ziara ya kikazi ya siku mbili ambapo anatarajiwa kulihutubia Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa mji mkuu wa Burundi wa Bujumbura, Rais Kikwete amepokelewa na Rais wa Burundi Mheshimiwa Pierre Nkurunzinza na pamoja na mamia kwa mamia ya wananchi wa Burundi. 
Rais Kikwete ambaye amewasili Burundi akitokea Dodoma ambako alikuwa katika ziara ya kikazi pia leo Machi 19, 2015, atahutubia Bunge la Nchi Wanachama wa Afrika Mashariki (EALA) katika nafasi yake ya Uenyekiti wa Mkutano wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuia ya Afrika Mashariki (EAC) katika hotuba ya The State of the East African Community Address.

Wednesday, March 18, 2015

Mgambo Shooting yaiumbua Simba kwa kuwachapa 2-0, Yanga SC yaichapa Kagera Sugar bao 2-1 Taifa

Na Mwandishi Wetu, Tanga
TIMU ya Mgambo Shooting yenye maskani yake Kabuku, wilayani Handeni, mkoani Tanga, leo imeiadhibu timu ya Simba kwa kuwafunga bao 2-0. Katika mchezo wa Ligi ya Tanzania Bara, uliochezwa kwenye Uwanja wa Mkwakwani, jijini Tanga.

Mabao ya Mgambo yalifungwa na Ally Nassoro dakika ya 44 kipindi cha kwanza, akiunganisha pasi ya Fully Maganga na kuibua shangwe kwa mashabiki wao, huku likiwanyong’onyesha wale wa Simba, waliokuwa na hamu ya timu yao kuibuka na ushindi.

Bao la pili lilifungwa na Malimi Busungu dakika ya 66 kufuatia kipa wa Simba, Ivo Mapunda kumchezea madhambi Fully Maganga ndani ya eneo la hatari na mwamuzi Amon Paul kuamuru ipigwe penati iliyozaa bao hilo la pili hivyo kuzamisha jahazi la timu hiyo ya Simba.

Kwa ushindi huo, Mgambo sasa imefikisha pointi 23, huku ikitakiwa kufanya bidii katika kujinusuru ili wagosi hao wa Kaya wasiweze kushuka daraja katika Ligi iliyokuwa na ushindani wa aina yake kutokana na timu zote kupania kufanya vizuri.

Kufungwa kwa timu hiyo ya Simba kumeondoa furaha yote ya kuwafunga watani zao wa jadi Yanga SC, waliyoupata hivi karibuni. Wakati Simba ikipata kipigo hicho, wenzao Yanga wameibuka na ushindi wa bao 2-1 dhidi ya Kagera Sugar, mchezo utakaopigwa katika Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.




DC asema ujenzi wa maabara shule za kata wilayani Kilindi mambo mazuri

Na Mwandishi Wetu, Kilindi
MKUU wa Wilaya Kilindi, DC Selemani Liwowa, amesema kwamba wilaya yake ipo katika hatua nzuri juu ya ukamilishaji wa suala la ujenzi wa maabara, tangu walivyoanza mchakato huo mwaka jana.

Mkuu wa Wilaya ya Kilindi, Selemani Liwowa, pichani.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi wilayani Kilindi, DC Liwowa alisema kwamba shule nyingi zimeshakamilika kwa kiwango cha asilimia 100, huku zile zilizosalia zikiwa katika hatua ya mwisho za (finishing), jambo linalotia moyo.

Alisema kwamba akiwa kama DC wa Kilindi alihakikisha kwamba agizo la Rais Jakaya Kikwete juu ya ujenzi wa maabara linafanikiwa kwa vitendo, hivyo kuanza kulisimamia kwa nguvu zote kwa kushirikiana na watendaji, watumishi na wananchi wote.

“Kidogo sisi tunaendelea vizuri na ujenzi wetu wa maabara ambapo shule nyingi zimefikia hatua nzuri na nyingine zilizosalia zimeshakamilika kwa asilimia zote kutokana na nguvu kazi na ushirikiano wa watu wote katika wilaya yetu.

“Naamini kwa hatua hii ile dhana ya ujenzi wa maabara itakuwa na mashiko kwa kuhakikisha kwamba shule za kata zilizosalia ambazo ujenzi wake haujakamilika unafanyika nguvu na jitihada kubwa kukamilisha mchakato huu muhimu,” alisema.

Licha ya mabadiliko kadhaa katika wilaya mbalimbali kwa wakuu wake wa wilaya kuhamishwa, DC Liwowa ni kati ya wale waliobakizwa kwenye vituo vyao vya kazi, jambo linalomfanya aendelee na program zake alizokuwa akizifanya kwenye wilaya ya Kilindi.

Mbunge alia na unyanyapaa kwa walemavu wa ngozi

Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Al-Shaymaa Kwegyir, akizungumza na wanazuoni wa Chuo Kikuu cha Kumbukumbu cha Hubert Kairuki hawapo pichanai, katika kongamano la kujadili nini kifanyike kutokomeza mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi (albino) lililofanyika jana chuoni hapo. Kushoto ni Makamu Mkuu wa Chuo hicho Keto Mshigeni na Kulia ni Kokushubika Kairuki. 
 
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
MBUNGE wa Viti Maalum ambaye pia ni mlemavu wa ngozi (albino),  Al -Shaimaa Kweigyir, amekemea vikali unyanyapaa unaofanywa na baadhi ya Watanzania juu ya jamii yenye ulemavu wa ngozi na kusema kwamba inawafanya watu hao waishi kwa unyonge.

Mbunge huyo aliyasema hayo jana katika kongamano la kujadili nini kifanyike ili kutokomeza mauaji na vitendo vya ukatili wanavyofanyiwa walemavu wa ngozi llilofanyika katika Chuo Kikuu cha Kumbukumbu cha Hubert Kairuki na kuhudhuriwa na watu mbalimbali, wakiwamo wanazuoni.
Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Al-Shaymaa Kwegyir, katikati akiwa kwenye kongamano la wanazuoni wa Chuo Kikuu cha Kumbukumbu cha Hubert Kairuki kujadili nini kifanyike kutokomeza mauaji ya albino. Kushoto ni Makamu Mkuu wa Chuo hicho Keto Mshigeni na Kulia ni Kokushubika Kairuki.

Akizungumzia unyanyapaa huo, Shaimar alisema kwamba bado baadhi ya wana jamii wamekuwa wakiendeleza vitendo vya unyanyapaa vinavyofanywa na watu ambao wamekuwa na mtizamo hasi juu ya watu wenye ulemavu wa ngozi.

Alisema kwamba jamii ikielimika na kutambua haki sawa kama walivyokuwa nazo wao juu ya ndugu zao albino, hata mauaji yatapungua kama sio kwisha kabisa, hususan kwa kuhakikisha kwamba wanawalinda na kuwathamini wakati wote.

MGODI UNAOTEMBEA:Wametulia, lengo lao Handeni imwage damu kwa migogoro ya ardhi

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
NASHAWISHIKA kusema kwamba baadhi ya viongozi na watendaji wa serikali katika wilaya ya Handeni, mkoani Tanga, hawanazo kichwani. Na kama wanazo, basi wamegubikwa na maslahi zaidi. Wameshindwa kusimamia mambo yenye tija kwa wananchi na wakazi wao wilayani Handeni.

Mmoja wa wakulima wadogo walioporwa mashamba yao katika moja ya vijiji vya wilaya ya Handeni, Hausi Zuberi pichani.

Ndio hawanazo. Maana yapo mapungufu ya wazi ambayo kwa mtu mwenye akili hawezi kuyaacha yashamiri. Mtu mwenye nazo kichwani, atayafanyia kazi matatizo yanayowahusu watu, ukizingatia kwamba ndio kusudio la uwapo wake kwenye nafasi nyeti za serikali, kama ardhi, maji, afya, kilimo na mengineyo muhimu.

Baadhi ya mambo hayo hayahitaji hata elimu ya kidato  cha nne kubaini mapungufu. Ni kutokana na hilo, nadiriki kusema viongozi wa serikali wamenyamaza, wakiwa na lengo la kuona Handeni inamwaga damu kutokana na migogoro ya ardhi.

Katika kila kijiji cha wilaya ya Handeni kina migogoro mikubwa ya ardhi. Hali hiyo inatia hofu. Migogoro hiyo ni ile inayohusisha wakulima na wafugaji, wakulima wadogo na wafanyabiashara waliopewa jina la madalali wa ardhi, ama mipaka inayohusisha vijiji, bila kusahau wilaya kwa wilaya katika baadhi ya maeneo.

Na migogoro hiyo imekuwa kero kiasi cha kuwafanya wananchi wakose imani na viongozi na watendaji wa serikali katika maeneo yao. Wanafanya hivyo kwa sababu kero zao hazitatuliwi.
Kilio cha wananchi kimeendelea kuwa cha samaki, machozi yanakwenda na maji. Hii n hatari. Tulipofikia ni kubaya na wakati wowote wananchi wataanza kupigana.

Watamwaga damu kama wanavyomwaga damu katika maeneo mengine ya nchi. Ajabu, licha ya wakulima na wananchi kulalamikia suala hilo, lakini hawasikilizwi. Watendaji wa serikali wamebakia kuwatumikia wenye nazo. Wanachumia tumbo.

Chaguo lao kwanza ni wafugaji wakiamini kuwa watalipwa fedha au rushwa ya wanyama, kama vile ng’ombe, mbuzi na kondoo. Ama wale wakulima wakubwa wenye nazo. 

Hao ni rahisi kwenda Polisi na kupata askari wa kuongozana nao eneo la tukio kwa ajili ya kuwaogopesha wananchi.

Hakuna haki anayeipata mlalahoi. Katika vijiji 112 vya wilaya ya Handeni hakuna kilichokuwa na ahueni. Huko watendaji wa vijiji baaadhi yao wamekuwa madalali wa kuuza ardhi. Na wenyeviti wengi wamefikia kughushi mihutsari inayogawa ardhi kwa wafanyabiashara bila kuangalia sheria ya ardhi.

Tuesday, March 17, 2015

Bondia Francis Cheka abadilishiwa adhabu, sasa kutumikia kifungo cha nje badala ya miaka mitatu jela

Na Mwandishi Wetu, Morogoro
BONDIA maarufu wa uzito wa juu Tanzania, Francis Cheka, pichani, amepata ahueni baada ya kubadilishiwa kifungo kutoka kifungo cha miaka mitatu jela hadi kutumikia kifungo cha nje.

Taarifa kutoka mkoani Morogoro zinasema sasa bondia huyo atatakiwa kufanya kazi katika taasisi za kiserikali kwa muda atakapokuwa anatumikia kifungo  cha nje, akitokea gerezani.

Cheka alihukumiwa kwenda jela kwa miaka mitatu baada ya kukutwa na hatia ya kumpiga meneja wa baa yake Bahati Kabanda, mkoani Morogoro kwa madai kuwa ya kutoridhishwa na mahesabu kwenye biashara yake hiyo.


LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...