WAZIRI MKUU Mizengo Pinda
pichani, ameahidi kutoa Sh. milioni 10 ili kuwasaidia vijana wanaoishi kwenye kijiji cha
vijana cha Tulu ambao wameamua kujitegemea kwa uzalishaji kupitia kilimo,
matumizi ya misitu na ufugaji.
Alitoa ahadi hiyo jana
jioni (Alhamisi, Agosti 29, 2013) wakati akizungumza katika mkutano wa hadhara
na vijana wa kijiji hicho pamoja na wakazi wa vijiji jirani vya Tumbili na
Lufwisi wilayani Sikonge mkoani Tabora.
Kijiji cha Vijana cha
Tulu ambacho wenyewe wanakiita Pathfinders Green City (Jiji la Watafuta Njia)
kilianzishwa Aprili 2013 kikiwa ni msitu mtupu baada ya kupewa ekari 280 kutoka
vijiji jirani vya Tumbili na Lufwisi. Kilianzishwa kikiwa na vijana 68 kutoka
katika kata zote 17 za Wilaya ya Sikonge. Hivi sasa kijiji kina vijana 87
wakiwamo wasichana 22 na wavulana 65 wenye umri wa kati ya miaka 18 na 24.










