https://tpc.googlesyndication.com/simgad/8045142562622600543


Recent Post

Monday, April 06, 2015

Dayna Nyange kuachia wimbo mpya uitwao 'Nitulize', akiimba na Nay wa Mitego

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
MWMBAJI wa kike wa muziki wa kizazi kipya Mwanaisha Said ‘Dayna’ Jumatano anaachia wimbo wake mpya unaokwenda kwa jina la ‘Nitulize’, akiimba kwa ushirikano mkubwa na Nay wa Mitego.
Dayna na Nay wa Mitego wanavyoonekana katika kava ya wimbo mpya uitwao Nitulize ulioimbwa na Dayna akimshirikisha Nay wa Mitego.

Wimbo huo unatarajiwa kuwa na mvuto wa aina yake kwa wadau na mashabiki wa muziki wa Bongo Fleva unaozidi kutesa katika sehemu mbalimbali za Tanzania na nje ya nchi kwa ujumla. Akizungumza na Mtandao wa Handeni Kwetu, Dayna alisema kuwa wimbo huo mpya umetengenezwa na mtayarishaji wake T Touch kutoka Studio za Free National Sound.

Alisema wimbo huo utakuwa moto wa kuotea mbali kutokana na aina ya uimbaji uliochanganya sauti mbili za Dayna na Nay wa Mitego, moja ya wasanii wanaofanya makubwa katika tasnia hiyo. “Huu ni wimbo wa aina yake kutokana na jinsi nilivyotulia katika uimbaji wangu na nilivyoweza kutuliza akili yangu, huku nikifurahishwa zaidi na Nay wa Mitego alivyoweza kuimba.

“Naomba mashabiki wangu wakae mkao wa kula baada ya kuachia kibao change hiki keshokutwa Jumatano katika vituo mbalimbali vya radio, ukiwa ni mwendelezo wa kuonyesha makali yangu,” alisema.
Dayna aliwahi kutesa na nyimbo kadhaa ikiwamo ile ya Mafungu ya Nyanya, Nivute Kwako, Fimbo ya Mapenzi, ambazo kwa pamoja ziliweza kumtangaza vyema katika tasnia ya muziki wa kizazi kipya.


SIWEZI KVUMILIA:Uchaguzi huo, walau watapa jezi na mipira

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
UKIFANYA utafiti kidogo tu namna vijana wanaojihusisha na mambo ya kimichezo wanavyoangaliwa, utabaini kuwa leo hii wameanza kuonekana umuhimu wao. Baadhi yao katika maeneo mbalimbali wameanza kupokea vijizawadi vya jezi au mipira.

Hata hivyo, vijana hao wameanza kupata zawadi hizo kwa sababu ni mwaka wa Uchaguzi Mkuu. Wanaotoa zawadi hizo wanasukumwa na dhamira zao za kutaka kugombea nafasi mbalimbali za uongozi, iwe ni ubunge au udiwani.

Haya ni matatizo makubwa. Ni matatizo kwa sababu umuhimu wa vijana hao unaonekana kila mwaka wa uchaguzi. Ingawa tunatambua umuhimu wa michezo, lakini wadau wamekuwa kimya wakisubiria mwaka wa uchaguzi tu ndio wajitolee.

Hakika Siwezi kuvumilia kuona siasa zinapewa nafasi kila wakati hata kwa mambo yasiyostahili kutokana na umuhimu wake. Na wakati mwingine natamani kuwaambia vijana hao wasisumbuke na watu hao wanaojikosha katika mwaka wa uchaguzi.

Bali wajiweke mikakati ya kuona vipaji vyao vinawika hata kama asipotoa mpira mmoja au jezi mwanasiasa asiyekuwa na dhamira ya kukomboa vijana wanaokufa njaa licha ya kusheheni vipaji vya kucheza soka katika mikoa mbalimbali.

Hii inakera na kustaajabisha mno. Tanzania imebarikiwa kuwa na vijana wenye vipaji vya kila aina kama vile ngumi, riadha, mpira wa miguu na mingineyo. Hata hivyo hatuna mipango ya kuwaendeleza wenye vipaji hivyo. Tumeendelea kuwa wanasiasa.

Mtu anajiwekeza visenti vyake akijua fika anapotoa jezi seti mbili au tatu basi ataungwa mkono na makundi ya vijana. Hii haikubaliki. Na lazima wadau hao, wakiwamo hao wanasiasa kutafuta nafuu ya maisha kwa wanamichezo wao. Waweke mikakati endelevu kabla ya uchaguzi na hata baada ya uchaguzi ili faida zao zionekane dhahiri.

Tuacheni kufanya siasa hata pasipotakiwa. Lazima tufahamu michezo ni ajira. Makundi ya watu wasiokuwa na ajira wanaweza kuishi vyema kama wataibuliwa na kuendelezwa kutokana na vipaji vyao vya michezo, iwe ni riadha au mpira wa miguu.

Huo ndio ukweli. Ni wakati huu makundi hayo yakawa makini kupokea wanasiasa hao wanaoanza kuwaona leo kwa kuwapa jezi za bei rahisi ili wawachague na bada ya hapo huwakimbia kwa kipindi cha miaka mitano, huku wakiishi bila kujua kesho yao.

Badala yake watumie nguvu zao na maarifa yao kufanya mazoezi kwa bidii, pamoja na kutumia fursa zozote wazipatazo, ikiwamo kutafuta timu zenye dira ili waonyeshe vipaji vyao kwa ajili ya kuwakomboa kimaisha na kiuchumi.

Kinyume cha hapo, vijizawadi vya jezi au mpira vitaendelea kuwapatia maisha duni, maana licha ya kuwachagua watu hao, lakini wanashindwa walau kuanzisha ligi yenye thamani ya Sh 10 tu kwa mwaka ili kuhakikisha kuwa wanakuwa na Ligi yenye nguvu na ushindani kwa ajili ya kuwapatia mwangaza makundi ya vijana wanaoamini soka au michezo ndio ajira zao.
Tuone wiki ijayo.

0712053949

Sunday, April 05, 2015

Mwenyekiti wa Chama cha siasa cha NRA, Mheshimiwa Rashid Mtuta, afariki Dunia

MWENYEKITI wa Chama cha siasa cha NRA, Rashid Mtuta, amefariki Dunia ghafla usiku wa kuamikia April 5, 2015 katika Hospitali ya wilaya ya Temeke, jijini Dar es Salaam. 

Enzi za uhai wa mheshimiwa Rashid Mtuta, aliyesimama akichangia Bungeni Dodoma mwaka jana, katika vikao vya Bunge la Katiba. Picha kwa hisani ya Mitandao.

Kwa mujibu wa taarifa fupi iliyotolewa na Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho, Hassan Kisabya, ilisema kuwa mipango ya mazishi inafanyika nyumbani kwa marehemu Kilungule, Mbagala, jijini Dar es Salaam. 

Marehemu aliwahi kufaanya shughuli nyingi za ujenzi wa Taifa, ikiwa ni pamoja na kuwa Mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba (BMK), lililofanyika mwaka jana.

Saturday, April 04, 2015

Jamal Malinzi akutana na Makamu wa Rais wa FIFA

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini TFF jana ijumaa ilipokea ugeni wa makamu wa Rais wa FIFA ambaye pia ni mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu nchini Jordan, HRH Prince Ali Bin Al Hussein pichani.

Jioni Prince Ali Bin AliHussein na ujumbe wake walifanya mazungumzo na Rais wa Shrikisho la Mpira wa Miguu nchini TFF Jamal Malinzi  katika hoteli ya Kilimanjaro Kempsinki (Hyatt) iliyopo jijini Dar es salaam.

Katika mazungumzo hayo, zaidi waligusia maeneo kadhaa ya ushirikiano kati ya TFF na Chama cha Mpirwa wa Miguu nchini Jordan (JFA), hasa katika maeneo ya maendeleo ya mpira wa vijana, makocha na waamuzi.

HRH Prince Ali Bin Al Hussein ambaye ni mgombea wa nafasi ya urais FIFA mwaka huu, ameondoka leo mchana kurudi nyumbani kwake Jordan.
  

TFF yawalilia mashabiki wa Simba waliofariki ajalini mkoani Morogoro

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini TFF Jamal Malinzi, ametuma salamu za rambi rambi kwa Rais wa klabu ya Simba SC Bw. Evans Aveva kufuatia vifo vya mashabiki wa klabu hiyo, viliyotokea jana katika ajali ya barabarani eneo la Makunganya mkoani Morogoro.

Katika salamu zake Rais Malinzi amesema, TFF imezipokea kwa masikitiko taarifa hizo za ajali na kwa niaba ya familia ya mpira wa miguu nchini, wanawapa pole wafiwa wote na mwenyezi Mungu awape nguvu majeruhi waweze kupata nafuu na kupona kwa uharaka zaidi.

Aidha Rais  Malinzi ameagiza michezo yote ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania itakayochezwa  wikiendi hii nchini, kusimama kwa dakika moja ili kuwakumbuka mashabiki waliopoteza maisha katika ajali hiyo.

Friday, April 03, 2015

Mashabiki watano wa Simba SC wafariki ajalini Morogoro

MAJONZI. Klabu ya Simba imepata pigo baada ya kudaiwa kuwa mashabiki wake watano wamefariki Dunia kufuatia ajali waliyopata katika eneo kati ya Mkambala na Mdaula mkoani Morogoro wakati wanaelekea Shinyanga.
Habari kutoka kwenye vyanzo vyetu vya habari zinasema kwamba ajali hiyo ni baada ya gari walilokuwa wakisafiria kutumbukia mtaroni. Taarifa zaidi zitaendelea kutafutwa juu ya chanzo cha ajali hiyo. Pichani ni gar hilo hilo lililotumbukia mtaroni.

Bloggers watoa tamko zito kwa rais Jakaya Mrisho Kikwete kufuatia sheria mpya ya makosa ya mitandao

Mtandao wa waandishi kupitia mitandao nchini, Tanzania Bloggers Network (TBN) tunamuomba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. Jakaya Mrisho Kikwete kutumia mamlaka yake vyema kwa kutokupitisha muswada wa Sheria ya Makosa ya Mtandao, 2015 unaokandamiza uhuru wa mawasiliano mitandaoni. 
 
Muswada wa sheria ya makosa ya Mtandaoni unaainisha makosa yanayohusiana na matumizi ya mfumo wa kompyuta na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, na kuweka utaratibu wa upelelezi, ukusanyaji na matumizi ya ushahidi wa kieletroniki na masuala mengine yanayohusiana na hayo.
 
MUSWADA WA SHERIA YA MAKOSA YA MTANDAONI, 2015
Umoja huu (TBN) ulishtushwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kukubali kupitisha Muswada wa Sheria ya Makosa ya Mtandao 2015 kwa hati ya dharura kitendo ambacho hakikutarajiwa kutokana na kuwa mitandao bado ni kitu kipya nchini hivyo tulihitaji maridhiano na wadau na elimu kati ya raia na Serikali ili wengi watambue yapi ni makosa kwa kutumia mitandao na yapi yanakubalika.
 
Kimsingi TBN haipingi Tanzania kuwa na Sheria ya Makosa ya Mtandao bali inaiomba Serikali kuwashirikisha wananchi na hasa wadau wa habari na wanamitandao ya jamii ili kuridhiana kwa vipengele ambavyo vinaonekana kukandamiza uhuru wa vyombo vya habari. Na hatimaye kutoka na sheria isiyo na viashiria kandamizi juu ya uhuru wa kupata na pokea habari.
 
Hali kadhalika tulishuhudia watetezi wa haki za binadamu pamoja na wawakilishi wa watumiaji wa Mtandao wa intaneti nchini wakitoa sababu zenye uzito za kwanini sheria hii isipite kwa hati ya dharura na kuhoji kwanini sheria hii ipite kwa dharura bila ya kupata majibu.
 
Muswada huu ambao kati ya makosa mengi uliyonayo kubwa moja wapo ni majukumu makubwa aliyopewa Mkuu wa Kituo chochote cha Polisi kuwa na uwezo wa kupekuwa na kuchukua vielelezo/data pale anaposhuku kuna suala la uhalifu unaohusu mtandao. Swali ni kuwa kwanini polisi apewe mamlaka ya kumsulubisha mtuhumiwa katika hatua ya mwanzo bila uthibitisho wa sahihi?
 
Mbali na hapo, sisi kama waandishi ulimwenguni kote tunatakiwa kufuatilia maadili ya kazi zetu. Maadili ya mwandishi yeyote yule ni kutunza usiri wa chanzo cha habari yake pale inapotakiwa lakini katika sheria hii sisi kama bloggers, sheria hii inakiuka hili kwa kutulazimisha kutaja vyanzo vya habari.
 
Kupitia sheria hii, bloga yeyote yupo hatarini kutokana na kwamba sheria inaainisha ni kosa la jinai kutoa ujumbe unaoweza kumuudhi mtu kihisia.
 
Aidha, tunamuomba Mheshimiwa Rais pia asipitishe Muswada wa Sheria ya Takwimu ya Mwaka 2013.
 
Muswada huu unavinyima uhuru vyombo vya habari vinavyotangaza takwimu mbalimbali. Kama ilivyo Ibara ya 7(4) ‘‘Chombo chochote cha habari ambacho kinachapisha taarifa za kitakwimu za uongo au upotoshaji, au kinatangaza kipindi chochote kinachohusu shughuli za ukusanywaji wa taarifa ambayo imefanywa au inafanywa na Ofisi, na hatimaye kusababisha wananchi wasishiriki kwenye shughuli hiyo ya ukusanywaji wa taarifa au wasishirikiane na maafisa wa Ofisi, kinatenda kosa.’’
 
Hii iki maanisha kuwa hata blog zetu ziko hatarini kuelekea katika kulazimika kufanya kazi za kuisifia serikali na kutangaza takwimu zilizopitiwa na serikali tu, jambo ambalo litaharibu ukuaji wa uhuru wa habari nchini.
 
Tunamkumbusha mwananchi wa kawaida anayetumia mtandao wa intaneti kuwa hayuko salama kwani sheria hii inamlazimisha mtoa huduma wa mtandao kutoa taarifa za wateja wake jambo ambalo linahatarisha uhuru wa kutoa na kupokea habari.  
Mungu Ibariki Tanzania, Mungu Ibariki Afrika
 IMETOLEWA NA;
Chama cha Bloggers Tanzania (Tanzania Bloggers Network-TBN)

Mgahawa unaouza chakula cha Kitanzania wafunguliwa rasmi nchini Sweden

IMG_1562
Mgeni rasmi Balozi wa Tanzania nchini Sweden, Mh. Dora Msechu (wa tatu kushoto) akiwa na mwenyeji wake Meya wa Trollhattan, Paul Akerlund (wa tatu kulia), Afisa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa nchini Tanzania, Tagie Daisy Mwakawago (kulia), Mmiliki wa mgahawa unaotoa huduma za chakula cha kitanzania unaofahamika kama "Lunch by Chef Issa" (The house of Tanzanian food) uliopo katika mji wa Trollhattan, Sweden unaomilikiwa na mtanzania Chef Issa Kapande (wa pili kulia) katika picha ya pamoja na wadau mara baada ya kuwasili kwenye mnuso wa uzinduzi wa mgahawa huo.(Picha zote na Zainul Mzige.

Na Mwandishi Maalumu, Trollhattan-Sweden
MGAHAWA mkubwa unaotoa huduma za chakula cha Kitanzania unaomilikiwa na mpishi maarufu duniani, Issa Kapande `Chef Issa’, umefunguliwa nchini Sweden na kuvunja rekodi ya dunia. Mgahawa huo ulizinduliwa na balozi wa Tanzania nchini Sweden, Mh. Dora Msechu.
Balozi Msechu alimpongeza Issa Kapande na mkewe kwa kufanikisha kuwapo kwa mgahawa huo ambao umeweka rekodi kuwa mgahawa mkubwa kuliko yote ya Kiafrika katika nchi za Ulaya.

Aidha, alimshukuru Torvald Brahm mwenyeji wa mji huo kwa kumuunga mkono Issa hadi kufanikisha ndoto yake ya kuwa na mgahawa wa kwanza wa Kiafrika katika mji wa Trollhattan utakatoa huduma ya chakula cha kitanzania.
Katika uzinduzi huo ambapo wenyeji wa manispaa hiyo akiwemo Meya na mwenyekiti wa Trollhattan, Paul Akerlund na msaidizi wake Peter Eriksson walikuwepo, balozi ambaye ndio kwanza ameanza kazi alielezea kufurahishwa na juhudi za Kapande.
IMG_1477
Wadau wakiwa nje ya ukumbi tayari kuhudhuria hafla ya uzinduzi wa mgahawa huo.
IMG_1567
Mgeni rasmi Balozi wa Tanzania nchini Sweden, Mh. Dora Msechu akiwa na mwenyeji wake Meya wa Trollhattan, Paul Akerlund (kushoto) pamoja na Chef Issa Kapande (kulia) wakielekea kwenye eneo la tukio.
Alisema Issa ameonesha njia kwamba inawezekana kwa watu waliopo Ughaibuni sio tu kuajiriwa, bali kujiajiri katika nyanja mbalimbali.

Alisema hilo linawezekana kutokana na kufuatilia kwa karibu taratibu za wenyeji na kisha kutumia mafunzo yaliyopo kukamilisha ndoto.
"Ni dhahiri kuwa, Chef Issa kwa kupitia taaluma yake ya upishi amewezeshwa kumiliki mgahawa huu hapa Trollhattan,S weden kwa hilo, napenda tuishangilie na kuipigia makofi Sweden na Trollhattan."

Thursday, April 02, 2015

Msemaji wa Coastal Union Oscar Assenga alivyompatia kitabu cha DIRA NA TUMAINI JIPYA HANDENI, bwana Amiri Mganga

Mdau wa maendeleo wa wilaya za Handeni na Kilindi, mkoani Tanga, bwana Amiri Mganga, mwenye t-shirt nyekundu, akikabidhiwa nakala ya KITABU CHA DIRA NA TUMAINI JIPYA HANDENI, kilichoandikwa na Kambi Mbwana, kutoka kwa Msemaji wa Coastal Union, Assenga Oscar ambaye pia ni Mwandishi wa habari wa New Habari 2006 Ltd, wachapishaji wa magazeti ya Mtanzania, Rai, Dimba, Bingwa na The African, leo jijini Tanga, Tanzania. 

Kitabu hicho kinapatikana kwa Sh 3500 tu. Maeneo yanapopatikana kitabu hicho ni pamoja na Handeni Mjini kwa Ayubu Magazeti soko la zamani, Misima, Sindeni, Kwamatuku, Komsala, Korogwe, Tanga Mjini na Dar es Salaam. Kama unahitaji kitabu hicho wasiliana nasi kwa simu +255 712053949, kambimbwana@yahoo.com.
Picha na Mpigapicha Wetu.

King Majuto ‘kuvunja mbavu’ Zanzibar siku ya KARUME DAY, Aprili 7

Na Andrew Chale
Msanii mkali wa maigizo na vichekesho, Nchini, Amri Athuman a.k.a King Majuto anatarajiwa kufanya shoo maalum ya vichekesho katika viwanja vya kufurahia watoto Kariakoo, Aprili 7, mwaka huu Mjini Unguja, Zanzibar.

Kwa mujibu wa wandaaji wa shoo hiyo kampuni ya Bond Entertainment Limited, kwa kushirikiana na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF), walieleza kuwa gwiji huyo wa vichekesho King Majuto ambaye pia ni mkongwe anayetamba ndani na nje ya Tanzania ataonyesha vichekesho vyake hivyo hiyo Aprili 7, katika mapumziko ya siku ya Karume (KARUME DAY).
mzee
KingMajuto“Ni wakati wa familia kujitokeza kwa wingi siku ya Jumanne ya tarehe 7/4/2015, kuja kumshuhudia King Majuto na kufurahia vichekesho vyake” ilieleza taarifa hiyo.
Ambaapo katika siku hiyo ya Aprili 7, kwenye shoo hiyo ya vichekesho, kiingilio kwa wakubwa ni Tsh.2,000/= huku kwa watoto itakuwa ni sh 1,000.

Mkuu wa Mkoa Dar es Salaam aongoza upandaji miti Mabwepande wilayani Kinondoni

Na Dotto Mwaibale
SERIKALI imesema waathirika wa mafuriko ya mto Msimbazi walioondoka baada ya kupewa viwanja maeneo ya Mabwepande na kurudi eneo la Msimbazi watanyang'anywa viwanja hivyo.

Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Sadiki kwenye maadhimisho ya kilele cha wiki ya upandaji miti Mkoa wa Dar es Salaam yaliyofikia tamati jana kwa upandaji miti kwenye viwanja vya Shule ya Msingi ya Mji Mpya iliyopo Mabwepande ambapo Wilaya ya Kinondoni ilikuwa mwenyeji.
 Meya wa Manispaa ya Kinondoni Yusuf Mwenda akipanda mti katika maadhimisho hayo.
 Mratibu wa mazingira kutoka Taasisi ya EBPA, Charles Lugenga (kushoto), akitoa maelezo mbele ya mkuu wa mkoa na viongozi wengine wa Manispaa Kinondoni jinsi ya upandaji wa mimea mbalimbali pamoja na miti kwa kutumia matairi ya magari yaliyotumika.

Wednesday, April 01, 2015

Barabara ya Msimbazi jijini Dar es Salaam yafungwa rasmi

Sasa barabara ya Msimbazi jijini Dar es Salaam inafungwa rasmi kuanzia leo Jumatano ya  01/04/2015. Kikao Maalum kilichowahusisha Wadau mbalimbali Kutoka kwenye Taasisi za Serikali kimekamilika punde na kukubaliana kufunga Rasmi Barabara ya Msimbazi ifikapo saa sita usiku leo. Wadau waliohusika kama inavyoonekana pichani ni pamoja na; 1. DART 2. Manispaa ya Kinondoni 3. Manispaa ya Ilala 4. 

Halmashauri ya Jiji 5. SUMATRA 6. TANROADS 7. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa 8. SMEC 9. STRABAG 10. JESHI LA POLISI. Mabadiliko mbalimbali ni pamoja na kubadilika kwa mielekeo mbalimbali ya Magari kutoruhusiwa kutumia barabara ya Msimbazi. Fuata maelekezo ya viashiria mbalimbali ili kukuepushia usumbufu. 

TUNAJENGA KWA AJILI YAKO TUNAOMBA USHIRIKIANO WAKO. Tunaomba Taarifa hii uitume kwenye Makundi mengine au kwa Rafiki yako ili kusaidia kusambaa kwa Taarifa hii muhimu kwa Wakazi wa Jiji la Dar es salaam. 
 

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...