https://tpc.googlesyndication.com/simgad/8045142562622600543


Recent Post

Tuesday, March 17, 2015

Migogoro ya ardhi Misima yaipasua kichwa CCM wilayani Handeni

Na Mwandishi Wetu, Handeni
MIGOGORO kadhaa inayaoendelea kurindima katika kijiji cha Misima, Kata ya Mabanda, wilayani Handeni, mkoani Tanga, imezidi kuipasua kichwa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wilayani humo.
Mwenyekiti wa CCM wilayani Handeni, mkoani Tanga, Athuman Malunda, pichani.

Jana mwenyekiti wa mtaa wa Kwedigondo, Idd Kisege alifikishwa mahakama ya Mwanzo Handeni, kwa madai ya kuvamia shamba la Michael Panga (NADA), wakati kesi kama hiyo inasikilizwa kwenye Baraza la Ardhi la wilaya Korogwe, mkoani Tanga.
Mmoja wa waathirika wa migogoro Misima anayejulikana kwa jina la Idd Kisege, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Mtaa wa Kwedigongo, kijiji cha Misima, wilayani Handeni, mkoani Tanga, akizungumza na wananchi wake hawapo pichani muda mchache baada ya kutoka mahakamani, akishtakiwa kwa kosa la kuigawa ardhi ya bwana Michael Panga (NADA).

Akizungumza mjini hapa, Mwenyekiti wa CCM  Handeni, Athuman Malunda, alisema kwamba Misima kuna matatizo mengi ambayo yanaashiria kuwa mitafaruku hiyo inaweza kuwa mibaya kwa CCM.

Alisema kwamba miongoni mwa mitafaruku hiyo ni migogoro ya ardhi inayoendelea kushamiri katika eneo hilo, likiwamo la NADA, ambaye anaonyesha aliazimwa shamba hilo alime na serikal ya kijiji.

“Japo ipo migogoro mingine kama ile ya wananchi kugomea kuwa kwenye Halmashauri ya Mji, lakini si suala kubwa isipokuwa hili la ardhi ambayo kwa kipindi kirefu sasa imekuwa kero.

“Hata hivyo sisi kama chama tunaendelea kutafakari namna ya kulifanyia kazi, ikiwamo kuwashauri au kuwasimamia watendaji wa serikali ambao kimsingi wanapaswa kuwa makini katika ufuatiliaji wa suala hili,” alisema.

Misima ni sehemu pekee kwa wilaya ya Handeni ambapo katika Uchaguzi wa Serikali za mitaa na vjjiji mwaka jana walionyesha kuwaangalia wapinzani kwa mitaa kadhaa kuchukuliwa na Chama Cha Wananchi (CUF), ukiwamo mtaa wa Kwedigongo.

Monday, March 16, 2015

SIWEZI KUVUMILIA:Tiketi za elektroniki, sisi tukale wapi?

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
KWA wale wanaonufaika na wizi wa tiketi au kuuza tiketi za bandia katika viwanja kadhaa vya michezo, hususan katika Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam, kamwe hawezi kufurahia ujio wa tiketi za kieletroniki.

Hii ni kwa sababu tiketi hizo zitawaua njaa. Watashindwa kuishi vizuri mjini wao na familia zao. Ndio maana tumeendelea kushuhudia malalamiko au maoni ya wadau wakielezea uuzwaji wa tiketi hizo kwa jinsi walivyojua wenyewe. Hapa ndipo nisipoweza kuvumilia.

Katika mechi ya Simba na Yanga iliyochezwa hivi karibuni, wapo watu waliokamatwa kwa kununua tiketi za bandia. Tiketi hizi zinauzwa kama njugu na wanaokamatwa ni wachache kati ya wengi wanaofanikiwa kuingia uwanjani kwa tiketi za bandia.

Hawa wanasababisha mapato yawe kiduchu. Wanadhulumu jasho la wachezaji na maandalizi yao yanayotumia gharama kubwa. Hii si haki. Ni vyema serikali kwa kushirikiana na wadau wengine wakaweka juhudi katika uuzwaji wa tiketi hizo ili wachache wasiendelee kufanikiwa kwa wizi huo.

Wakati nasema haya, nakiri kabisa mtu asiyekuwa na mtandao wa wizi huo wa tiketi za bandia, kamwe hawezi kupinga au kuhujumu mradi wa tiketi za eletroniki maana ni jambo lenye dira na mguso.

Wachache wanatajirika kwa biashara hiyo isiyodhibitiwa. Kutodhibitiwa huko kumezidi kuongeza watu wanaohujumu mradi wa tiketi huo kwa sababu ndio kwenye pona yao. Hapa siwezi kuvumilia.

Vyema juhudi zikawekwa ili kuhakikisha kwamba juhudi za ununuaji wa tiketi za eletroniki zinawekwa ili kulinda mfumo huo na wahujumu wanaofanya mbinu za aina mbalimbali kuukwamisha.

Wachache wenye mapenzi na mpira wa miguu na ndoto ya kuona nchi yetu inapiga hatua, hatuwezi kukubali vitendo vya wizi wa tiketi za bandia unaofanywa na hawa hawa wanaopiga vita uuzwaji wa tiketi za eletroniki kwa faida zao binafsi wao na familia zao.
Kinyume cha hapo mfumo huu hautafanikiwa.

Tuonane wiki ijayo.
+255 712053949

Sunday, March 15, 2015

Nashukuru kwa kuiona siku ya kuzaliwa, vijana tuchape kazi, tuache kulalamika ovyo

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
Jana ilikuwa ni Machi 14 mwaka 2015. Machi 14 ni siku ya kuadhimisha kuzaliwa kwangu baada ya kutimiza miaka kadhaa tangu kuzaliwa kwangu. Ingawa nafurahia kuzaliwa huko, lakini hudhuni inamea nifikiriapo kila ninachokifanya leo au nitakachofanya kesho nikiwa na uhai, hakitaaweza kuonwa na baba yangu, mzee Mbwana Hemed Masoud, maarufu kama Mzee Kajembe.

Kambi Mbwana, pichani
Mzee huyo aliyefanikisha uwapo wangu duniani akishirikiana na mwanamke jasiri na mkarimu na mwenye upendo kwa familia yake na jamii kwa ujumla, Bi Fatuma Omary, alifariki mwaka 2012 katika Hospitali ya Wilaya Korogwe (Magunga) na kuzikwa kijijini kwake Komsala, wilayani Handeni, mkoani Tanga.

Lala pema peponi baba yangu. Baada ya kusema hayo, nachukua fursa hii kuwatakia kheri wote walionitakia kheri ya kuzaliwa hiyo jana. Nimekuwa mwenye furaha kubwa nionapo jamaii yangu inaniheshimu na kunithamini. Kila nionapo mtu anayeguswa na mwenendo wangu, hakika nafarijika kupita kiasi.
Mdau wa Maendeleo na mmiliki wa mtandao wa Handeni Kwetu, akizungumza jambo katika moja ya matukio aliyoandaa likiwamo la NSSF Handeni Kwetu lilofanyika mwishoni mwa mwaka jana, wilayani Handeni, mkoani Tanga.

Nimekuwa nikifanya mambo mengi kwa ajili ya kuitumikia jamii na Tanzania kwa ujumla. Kama ilivyokuwa kawaida ya mambo mazuri hayakosi changamoto, nimekuwa nikitatizwa na baadhi ya mambo ambayo mwisho wa siku yanakuwa kama funzo kwangu.

Funzo hilo ni kuona naendelea kuishi kwa kufanya juhudi zote kama nilivyopanga bila kuona wangapi wananikubali na wangapi wananichukia. Nimeamua pia kukaza msuri kuanzisha vitu ambavyo ni active vyenye mchango na jamii yangu.

Mwaka 2013 nilianzisha tamasha la Handeni Kwetu linalofanyika kila mwisho wa mwaka, yani Desemba. Mwaka huu likifanyika litakuwa ni mara ya tatu mfululizo. Aidha, sehemu ya bajeti ya tamasha hilo kwa mwaka jana, pia lilitumika kugharamia safari vijijini na baadhi ya viongozi wa taasisi ya Handeni Kwetu Foundation, ambayo ni miongoni mwa waasisi kwa nia ya kuikomboa jamii ya Handeni na Tanzania kwa ujumla.

Saturday, March 14, 2015

Simba yainusa Yanga na Azam kwa kuwachapa Mtibwa Sugar bao 1-0

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Timu ya soka ya Simba, leo imeendeleza wimbi lake la ushindi kwa kuwafunga Mtibwa Sugar bao 1-0 katika mechi kali iliyokuwa na msisimko wa aina yake. Bao la Simba la pekee liliwekwa kimiani na mshambuliaji wa Kimataifa, Emmanuel Okwi  ‘mtaalamu’.

Kwa ushindi huo, Simba sasa imefikisha pointi 29, nyuma ya Azam FC yenye pointi 30 na Yanga ikishika usukani wa ligi hiyo kwa kuwa na pointi 31. Ushindi huo huenda ukapokewa kwa shangwe na wadau na mashabiki wa timu hiyo iliyoanza ligi kwa kusua sua.

Simba imeibuka na ushindi huku baadhi ya wadau wake wakiwa hawana imani na timu yao, licha ya kuibuka pia na ushindi wa bao 1-0 katika mchezo uliowakutanisha na watani wao wa jadi, Yanga, mechi ilyochezwa hivi karibuni.

Wadau wa soka wamlilia kocha Sylvester Marsh

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
WADAU mbalimbali wa sekta ya mpira wa miguu wamekipokea kifo cha aliyekuwa kocha msaidizi wa timu ya Taifa (Taifa Stars),  Sylvester Marsh, kilichotokea leo asubuhi.
Marehemu Sylvester Marsh, enzi za yhai wake.
Taarifa za msiba huo zimetokea huku Marsh akiwa ni miongoni mwa wadau wa  michezo na kocha mwenye uwezo na kipaji cha aina yake cha kufundisha soka. Mchezaji wa timu ya Azam FC, Himid Mao, aliandika kwenye mtandao wake wa facebook kuwa Tanzania imempoteza mtu muhimu kwenye sekta ya mpira wa miguu Tanzania.

Kocha huyo (Marsh) alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa kansa ya koo na hivi karibuni alisafirishwa kutoka Mwanza hadi jijini Dar es Salaam kwa ajili yaa kupatiwa matibabu kwenye Hospitali hiyo ya Taifa.

Hata hivyo, suala la afya yake liliendelea kuwa siri kubwa huku baadhi ya wadau wakishindwa kupataa habari za uhakika zilizokuwa zinamuhusu kocha huyo.

Friday, March 13, 2015

Umoja wa Ulaya watembelea skimu ya umwagilaji ya Kiroka mkoani Morogoro

DSC_0576
Msimamizi wa mradi wa FAO kijiji cha Kiroka mkoani Morogoro, Ajuaye Sigalla, akitoa muhtasari wa maendeleo ya mradi FAO unaotekelezwa na wanakikundi wa Umoja wa Wakulima Kiroka (UWAKI) mbele ya Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Mwakilishi wa shirika la Maendeleo (UNDP) nchini, Alvaro Rodriguez (kushoto) na Balozi wa Umoja wa Ulaya (EU) nchini, Filiberto Sebregondi walipofanya ziara ya kugagua miradi yao ya maendeleo mkoani Morogoro.Picha na Zainul Mzige

Na Mwandishi wetu, Morogoro
BALOZI wa Umoja wa Ulaya (EU) nchini Filiberto Sebregondi ametembelea skimu ya umwagiliaji ya Kiroka na kusema kwamba atahakikisha kwamba kwa kushirikiana na wadau wengine ikiwamo serikali wataendelea kusaidia wananchi kujiinua kiuchumi.

Akiwa katika skimu hiyo inayosaidiwa na Shirika la Chakula duniani (FAO) ametaka miradi ya maendeleo nchini kutowaacha nyuma wanawake na watoto kwani wao ndio msingi wa maendeleo ya kijamii kuanzia ngazi ya kaya hadi Taifa.
DSC_0633
Balozi wa Umoja wa Ulaya (EU) nchini, Filiberto Sebregondi akizungumza na wanakikundi wa Umoja wa Wakulima Kiroka (UWAKI) wanaofadhiliwa na FAO wakati wa ziara ya kutembelea miradi inayofadhiliwa na wadau wa maendeleo ambapo mradi wa Kiroka unafadhiliwa na shirika la Umoja wa Mataifa la FAO huku mradi wa makazi mapya kwa waathirika wa mafuriko Kilosa ukifadhiwa na Ubalozi wa Umoja wa Ulaya. Kushoto kwake ni Msimamizi wa mradi wa FAO kijiji cha Kiroka mkoani Morogoro, Ajuaye Sigalla.

Balozi huyo ambaye anatarajiwa kurejea Ulaya mwaka huu baada ya kumaliza muda wake wa uwakilishi nchini amesema kwamba kuwapo kwa asilimia 60 ya wafaidika na mradi huo wa Mpunga kuwa wanawake kumesaidia sana kuamsha maendeleo ambayo yanatakiwa kuendelea kusimamiwa.

"Wanawake wamefanikiwa kupeleka watoto wao shuleni. kuwapatia chakula kinachostahiki na kupata kipato na katika hili ni vyema wasiachwe nyuma kimaendeleo" alisema balozi huyo.

Thursday, March 12, 2015

Taasisi ya UWF yatoa msaada Hospitali ya Ocean Road

 Mwenyekiti wa Unity Women Foundation (UWF), Maryam Ajmy akiwa akikusanya misaada waliyokuwa wakitoa katika hospitali ya Ocean Road jijini Dar es Salaam kutoa msaada kwa wanawake ikiwa ni kuadhimisha siku ya wanawake duniani iliyofanyika hivi karibuni.  
Mwenyekiti wa Unity Women Foundation (UWF), Maryam Ajmy akiwa na wanaumoja wenzake wakiingia hospitali ya Ocean Road jijini Dar es Salaam kutoa msaada kwa wanawake ikiwa ni kuadhimisha siku ya wanawake duniani iliyofanyika hivi karibuni.   
---
Chalila Kibuda, Globu ya Jamii.
Unity Women Foundation (UWF), umetoa msaada kwa wanawake wagonjwa katika hospitali ya Ocean Road jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na baada ya kutoa msaada katika Siku ya Wanawake Duniani iliyofanyika hivi karibuni, Mwenyekiti wa UWF, Mariam Shamo amesema wanawake wanatakiwa kujitoa kwa wanawake wenzao wenye matatizo kwa siku zote kutokana na kuwepo kwa wanawake wengine hawana msaada wa mtu yeyote.
Mariam amesema wanawake siku ya wanawake itumike kwa kwa kufariajiana na kuendelea na kuweza kuona kuona mabadiliko na kuweza kutatua changamoto zetu zinazotukabiri.Amesema wanawake wenye uwezo wasaidie na kuwatembelea wanawake wenzao katika wodi mbalimbali na kutoa msaada hata kama ni kidogo lakini kinathamani yake.
Aidha amesema kama UWF wataendelea kutoa kuwafariji wagonjwa kila muda ili nao waweze kujua wanawake wa nje yao wanatambua matatizo yao.

Wednesday, March 11, 2015

SIWEZI KUVUMILIA: Aveva angalia jahazi lako lisizame

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
WATU wana kumbukumbu. Unapowaahidi jambo, hakika watakuja kukuuliza pale wanapohisi halijafanyiwa kazi. Na wasipokuuliza, bado haitakuwa sababu ya kutokuchukia.

Katika Uchaguzi Mkuu wa Simba uliofanyika mwaka jana, Rais wa sasa wa Klabu ya Simba, Evance Aveva, aliwaahidi wanachama na mashabiki wa timu hiyo mambo mengi, ukiwamo ushindi kila kila mechi.

Matokeo ya timu yanaonekana ni ya kusua sua. Na wadau wa mpira wa miguu wanajua fika, haiwezekani timu ikashinda kila mechi, huenda ilikuwa kampeni tu ili aweze kupata urais.

Ukiacha hilo la ushindi kwa kila mechi, bado Aveva akawa na ahadi nyingi, hususan ile ya kujenga uwanja, kuwa na vitega uchumi vyake pamoja na kuwa na taratibu nzuri zitakazowafanya wawike Kimataifa.

Na hapa ndipo ninaposhindwa kuvumilia. Siwezi Kuvumilia kwasababu sioni juhudi za dhati za kuipatia mafanikio timu hii kongwe iliyoanzishwa mwaka 1936, mwaka mmoja baada ya kuanzishwa Yanga SC.

Ingawa naweza kusema nyingi zilizotolewa na Aveva zilikuwa kampeni tu, lakini ahadi hizo ni kama kumbukumbu ya wanachama wake. Kesho watamuuliza na pengine kumtusi mchana na usiku.

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...