https://tpc.googlesyndication.com/simgad/8045142562622600543


Recent Post

Tuesday, February 10, 2015

SIWEZI KUVUMILIA:Tumekubali kuwa na wanamichezo masikini?

NA KAMBI MBWANA, DAR ES SALAAM
IFIKIE wakati kama Taifa tuone haya pale tunaposhuhudia wingi wa wachezaji ambao mwisho wa siku ni masikini. Mchezaji anawika kwa nyakati kadhaa, lakini ukimuangalia mfumo wake wa maisha utagundua hakuna kitu chochote anachoweza kujivunia.

Mimi si wa kwanza katika kilio hiki. Watu mbalimbali wameshawahi kuonyesha malalamiko yao, wakiwamo wanamichezo wenyewe. Kabla ya kuhukumiwa kifungo cha miaka 3 jela, bondia tishio, Francis Cheka, mara kadhaa Amelia juu ya maisha yake kuwa magumu, licha ya umaarufu aliokuwa nao.

Ukiacha Cheka, wapo wengine ambao majina yao hayalingani kabisa na kipato chao, hususan hawa wanaocheza michezo tofuati na mpira wa miguu wenye unafuu katika jamii yetu.

Wachezaji kama vile Mbwana Matumla, Rashid Matumla, Francis Miyeyusho, Japhet Kaseba, unaweza kulia utakapogundua majina yao makubwa si sawa na kipato chao na maisha yao kwa ujumla.

Na hili ndio sababu kuu ya kuwaathiri wanamichezo hao kisaikolojia. Na suala hilo litazidi kuwazorotesha wao kimichezo. Kamwe siwezi kuvumilia. Ni wakati sasa wa wanajamii kuweka mipango yenye tija na mbolea.

Tuelezane ukweli na kuamua kwa dhati kufanya mambo yenye kusababisha maendeleo na mafanikio. Mabondia wetu na wanamichezo wote kwa ujumla wawekewe mazingira bora na rafiki.

Kwa bahati mbaya, matatizo yote hayo yanaanzia chini ya serikali kwa kupitia Wizara ya Habari, Michezo na Utamaduni ambako hakuna sera au zipo lakini zina matege.

Na ndio maana tumekuwa na wanamichezo wengi wenye majina, lakini ni masikini wa kutupwa. Hii si sawa. Tuweke mifumo mizuri si tu kwa ajili ya kuendeleza michezo, bali pia kuwapatia maisha bora wanamichezo hao ili waishi vizuri kulingana na majina yao.

Kuanzishwe mashindano, mapambano makubwa kwa mabondia wa Tanzania, sambamba na kuwekewa mifumo ya kutoka nje na kushiriki kwenye matukio makubwa yenye kuingiza fedha nyingi.

Kinyume cha hapo michezo na wanamichezo wetu wa Tanzania wataendelea kuwa hohe hahe. Tatizo hili si rafiki kwa wanamichezo wetu. Na pia ni sehemu inayoifanya michezo ishindwe kupiga hatua.

Ukiacha mpira wa miguu tena ule wa wanaume, michezo mingine kwa Tanzania inatoa ajira kwa wanamichezo wetu au inawapotezea muda tu, maana muda mwingi mazoezini, lakini hakuna wanachoambulia zaidi ya kufanikisha majina makubwa, lakini mfukoni sifuri.

Hii ni hatari na haiwezi kuvumilika. Nani anafurahia tatizo hili kwa wanamichezo wengi wa Tanzania? Je, wadau wa michezo na viongozi wanaliangalia suala hili kwa kirefu?
Serikali inachoweza wao ni kutoa pongezi tu au kutoa pole panapokuwa na msiba, lakini si kubuni au kusimamia sera zenye mashiko kwa ajili ya kuendeleza michezo na kuwapatia maisha bora wanamichezo na Watanzania kwa ujumla.

Tunapaswa kubadilika, kinyume cha hapo siwezi kuvumilia kuona wanamichezo wetu wanaendelea kuogelea kwenye wimbi la umasikini, hali ya kuwa wana vipaji kama vile vinavyowapatia utajiri nyota duniani kote.
Tuonane wiki ijayo
+255712053949

Friday, February 06, 2015

Jeshi la Polisi yazindua magari ya Security Group Africa

 Mwakilishi wa Mkuu wa Jeshi la polisi nchini Kamishina wa Polisi Mussa Ally Mussa akiwa na mkuu wa jeshi la polisi mstaafu Philimon Mgaya akikata utepe wa kuashiria kuzindua magari mapya Zaidi ya ishirini ya kampuni ya ulinzi ya Security Group Africa ambayo yataanza kutumika katika kazi mbalimbali za kampuni hiyo hivi karibuni.Katikati yao ni mkurugenzi mkuu wa kampuni hiyo Eric Sambu.
 Mwakilishi wa Mkuu wa jeshi la polisi nchini Kamishina wa Polisi Mussa Ally Mussa  akipokea msaada wa pikipiki mbili aina ya Boxer toka kwa mwenyekiti wa bodi wa kampuni ya Security Group Africa ambae pia ni mkuu wa  jeshi la polisi mstaafu Philimon Mgaya kwaajili ya kusaidia jeshi hilo katika oparasheni mbalimbali za kupambana na uhalifu,Katikati yao ni mkurugenzi mkuu wa kampuni ya SGA nchini  Eric Sambu.
 Mkurugenzi mkuu wa kampuni ya SGA nchini  Eric Sambu akizungumza kwenye hafla ya kuzindua magari mapya Zaidi ya ishirini ya kampuni ya ulinzi ya Security Group Africa ambayo yataanza kutumika katika kazi mbalimbali za kampuni hiyo hivi karibuni.Hafla hiyo imefanyika katika ofisi za kampuni hiyo Mbezi Beach jijini Dar Es Salaam.
 Mwakilishi wa Mkuu wa jeshi la polisi nchini Kamishina wa Polisi Mussa Ally Mussa  akikagua gwaride maalum la kuashiria kuanza kwa shuguli ya kuzindua magari mapya Zaidi ya ishirini ya kampuni ya ulinzi ya Security Group Africa ambayo yataanza kutumika katika kazi mbalimbali za kampuni hiyo hivi karibuni.Kulia kwake ni mkuu wa kitengo cha mafunzo cha SGA bwana Rogers Lumwaji.
 Mwakilishi wa Mkuu wa jeshi la polisi nchini Kamishina wa Polisi Mussa Ally Mussa  akipeperusha bendera kuashiria kuanza kutumika kwa magari magari mapya Zaidi ya ishirini ya kampuni ya ulinzi ya Security Group Africa ambayo yataanza kutumika katika kazi mbalimbali za kampuni hiyo hivi karibuni.Katikati yao ni mkurugenzi mkuu wa kampuni hiyo Eric Sambu.

Mahakama ya Kisutu yampa haki yake Hans Macha


Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, imethibitisha kwamba mfanyabiashara Hans Macha alinunua nyumba kwa kufuata utaratibu na kihalali kutoka kwa Ramadhani Balenga.

Hayo yalithibitishwa leo kupitia hukumu iliyosomwa na Hakimu Mkazi Frank Moshi kwa niaba ya Hakimu Mkazi Devotha Kisoka, ambaye alisikiliza kesi ya kughushi inayomkabili Macha.

Katika kesi hiyo, Macha alikuwa akikabiliwa na mashitaka matatu ya kughushi hati ya umiliki wa kiwanja kilichopo eneo ya Kigogo, Dar es Salaam, kinachodaiwa kuwa mmiliki wake ni Ramadhani Balenga.

Pia alikuwa anadaiwa  kughushi mkataba wa mauziano wa eneo hilo kuonyesha kwamba Balenga alihamisha umiliki wa kiwanja hicho kwenda kwake na kuwasilisha nyaraka ya kughushi.

"Mahakama imepata muda wa kutosha wa kupitia ushahidi na vielelezo vyote. Makosa yote matatu hayajathibitishwa ipasavyo. Mlalamikaji  (Balenga), alimuuzia mshitakiwa eneo hilo kwa kufuata utaratibu na kihalali," alisema Hakimu huyo.

Alisema mahakama inamuachia mshitakiwa kwa mashitaka yote matatu na mlalamikaji ana nafasi ya kukata rufani.

Baada ya kusomwa kwa hukumu hiyo, Wakili wa Serikali Nassoro Katunga, aliuliza iwapo nakala ya hukumu ipo tayari, ambapo Hakimu Moshi alimwambia haipo tayari na kama wanaitaka wafuate taratibu kwa kuwasilisha maombi mahakamani hapo.

Wakati wa usikilizwaji wa kesi hiyo, upande wa Jamhuri uliita mashahidi na upande wa utetezi ulileta mashahidi takriban 10 akiwemo mshitakiwa mwenyewe na aliyekuwa mke wa mlalamikaji Balenga, Nury Ahmadi.

Baada ya upande wa Jamhuri kufunga ushahidi wao, Novemba, mwaka jana, mahakama hiyo ilimuona Macha ana kesi ya kujibu nahivyo kutakiwa kuwasilisha utetezi wake.

Wakati akijitetea mfanyabiashara Macha alidai tuhuma zinazomkabili ni za uongo na kuiomba mahakama kumuachia huru.

Katika utetezi wake, mfanyabiashara Macha aliiomba mahakama huyo kutupilia mbali mashitaka hayo kwa kuwa tuhuma hizo ni za uongo na Balenga anajua wazi kwamba alimuuzia hiyo nyumba namba 183 kitalu A iliyoko Kigogo.

Akiongozwa na Wakili Deo Ringia, Macha alidai alikuwa akimkopesha Balenga fedha huku akiweka dhamana hati za nyumba, hadi deni lilipofikia sh. milioni 879  ambalo hakuwahi kulilipa.

"Baada ya kushindwa kulilipa nilipomuuliza aliniambia makontena yake yalikamatwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), hivyo hakuwa na fedha ya kunilipa tena.

"Alinijulisha ana hati nyingine ya nyumba ya ghorofa tano iliyoko Kigogo, hivyo aniuzie na nyumb nyingine ya Manzese ambayo hati yake nilikuwa nayo na nimuongeze na sh. milioni 20," alidai

Macha alidai Balenga alimuambia  nyumba ya Kigogo,  amekopea mkopo benki ya Azania, hivvyo hati ipo huko na kumwahidi ataenda kuitoa ili wabadilishane kwa kumuuzia hiyo nyumba na kumuongezea sh. milioni 20  na baada ya hapo amrudishie hati nyingine nne alizokuwa amezishikilia.

"Makubaliano hayo tuliweka maandishi ya mauziano baada ya kuletya hati yake ya Kigogo. Hiyo ilikuwa mwaka 2011, nyaraka ya mauziano nakumbuka ilikuwa mkataba wa mauziano na pande zote mbili mimi na Balenga tulitia saini ofisini kwangu katika hoteli ya Rick Hill, iliyoko mtaa wa Kipata, Mnazi Mmoja, Dar es Salaam," alidai

Alidai wakati wanatiliana saini kulikuwa na mashahidi ambao ni Mashaka (mjomba wa Balenga), David (rafiki wa Balenga) na John Mboya na mkataba huo ulishuhudiwa na wakili Henry Mkumbi  ambaye aligonga mhuri baada ya kumueleza makubaliano yao  na alimkabidhi Balenga sh. milioni 20 mbele ya wakili huyo.

Macha alidai baada ya mauziano walitia saini hati ya kubadilisha umiliki na Balenga alimkabidhi nyaraka nyingine zinazohusiano na jengo hilo zikiwemo kibali halisi cha ujenzi, ofa ya jengo, michoro halisi ya jengo inayotoka Manispaa, mkataba alioingia na mjenzi na risiti mbalimbali.

Alipoulizwa na wakili anaielezeaje mahakama kuhusu madai ya Balenga kwamba hajamuuzia nyumba hiyo, Macha alidai ni ya uongo kwa kuwa alimuuzia na Balenga anajua kwamba alimuuzua hiyo nyumba.

Shahidi mwingine alikuwa aliyekuwa mke wa Balenga, Nury Ahmadi ambaye aliieleza mahakama kuwa mlalamikaji alimtamkia kwamba amemuuzia nyumba Macha.

Mashahidi wengine wa upande wa utetezi walikuwa mawakili wa kujitegemea Henry Mkumbi na Castro Rweikiza, ambao walidai walishuhudia utiliaji saini wa mkataba wa mauziano  baina ya Balenga akiwa muuzaji na Macha mununuzi na hati ya kuhamisha umiliki. Walidai katika nyaraka hizo, wao walitia saini na kugonga mihuri ya ofisi zao.

Wednesday, February 04, 2015

MGODI UNAOTEMBEA:Dkt Kigoda anastahili kupumzika jimbo la Handeni

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
UKWELI unauma. Na ili ufahamu hilo, mara nyingi watu wanaosema ukweli huwa hawapendwi. Watazushiwa na kusemwa mno kutokana na misimamo yao ya ukweli wanayosema mbele ya hadhira.
Waziri wa Viwanda na Biashara ambaye pia ni mbunge wa Handeni, kwa miaka 20 sasa, Dkt Abdallah Omary Kigoda, pichani.

Wakati nasema haya, najipa moyo kuwa hata kama wapo watakaochukizwa na ukweli wangu, ila ipo siku jamii itaishi vizuri kutokana na kukombolewa na harakati za ukweli zinazoweza kupingwa na wachache wao waliokuwa kwenye nafasi mbalimbali za kiutawala.

Ndio, bora niseme tu Dkt Abdallah Omary Kigoda anastahili kupumzika kuongoza kama Mbunge wa Handeni, mkoani Tanga. Kigoda ni mbunge wa Chama Cha Mapinduzi CCM kwa miaka 20 sasa.

Kigoda aliingia madarakani kwa mara ya kwanza kama mbunge mwaka 1995. Watoto waliozaliwa miaka ya 1995 mwaka 2015 wametimiza miaka 20. Ni kipindi kirefu mno kuongoza katika nchi inayojipambanua kuwa inaongozwa kwa misingi ya kidemokrasia.

Aidha, watoto hao waliozaliwa miaka ya 1995 na kukuta kero nyingi kama vile kukosa maji safi na salama, umeme vijijini, elimu duni, afya na mengineyo wanashangaa kama hadi leo kero hizo hazijatatuliwa ipasavyo licha ya kuongozwa na mbunge aliyekaa madarakani kwa muda mrefu.

Kwanini Kigoda anastahili kupumzika? Licha ya Handeni kuwa wilaya kongwe na kubwa mno, lakini wananchi wake wanaishi maisha magumu na kuvumilia shida mbalimbali, jambo lililowachosha.

Wilaya hii haina maji. Wananchi wake wanalazimika kununua ndoo ya maji kwa Sh 700 hadi 1000 yanapotoka mbali zaidi. Kwa mtu mwenye familia ya watu wanne, atalazimika kununua ndoo tatu hadi tano.

Endapo atanunua ndoo tano, basi atalazimika kulipia Sh 3500 kama atayanunua kwa Sh 700. Lakini kama atanunua kwa Sh 1000, basi mwananchi huyo atayanunua maji kwa Sh 5000. Je, pato lake kwa siku lipoje?

Mbaya zaidi, licha ya kuwa wilaya kongwe, lakini Hospitali ya wilaya ya Handeni haina chumba cha kuhifadhia maiti. Watu wanalazimika kupelekwa Hospitali ya wilaya Korogwe (Magunga) kuhifadhiwa kabla ya kuzikwa au kusafirishwa kwa wale wenye utaratibu huo.

Makala:Unafuu wa ada Twayyibat Sekondari wamkuna DC Temeke

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
ILI elimu ya Tanzania izidi kukua kunahitajika kuwa na shule nyingi za serikali na zile za binafsi zinazomilikiwa pia na taasisi za kidini na mashirika yasiyokuwa ya kiserikali.
Mkuu wa wilaya Temeke, Sofia Mjema, akizungumza na wanafunzi wa Shule ya sekondari ya Kiislamu, Twayyibat, iliyopo Manispaa ya Temeke, jijini Dar es Salaam, wiki iliyopita.

Kuwapo kwa shule hizo kutazidi kuongeza idadi kubwa ya watoto wanaopata elimu ya msingi, sekondari na vyuo Vikuu kwa ajili ya kujikomboa katika maisha yao.

Ukiacha mikoani ambako hakuna shule nyingi hususan maeneo ya vijijini, jijini Dar es Salaam kumefanikiwa kuwa na shule nyingi mno, zikiwamo za serikali na mashirika.

Zipo shule za kidini ambazo wakati wote zimekuwa zikifundisha watoto elimu ya Dunia na ile ya kufahamu Mungu ni nani, nazumgumzia pale watoto wanapofundishwa kisawa sawa na kukolea kiimani kama njia ya kumjua Mungu na kutenda matendo ya kiungwana.

Mwishoni mwa wiki iliyopita, Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Sofia Mjema, alitembelea katika shule ya Twayyibat Islamic Seminary, iliyopo Temeke, jijini Dar es Salaam.

DC Sofia alitumia muda huo kuikagua shule hiyo pamoja na kuzungumza na wadau wa elimu, walimu na wanafunzi wa shule hiyo kwa ajili ya kuona inakuwa kati ya shule bora wilayani Temeke na Dar es Salaam kwa ujumla.

Miongoni mwa mambo yaliyomkosha DC Sofia ni pale alipoambiwa kuwa ada ya shule hiyo kwa mwaka mmoja ni Sh 200,000 tu, jambo ambalo ni agharabu kuliona wala kulikisia katika shule mbalimbali jijini Dar es Salaam.

Akizungumza shuleni hapo, Mkuu huyo wa wilaya ya Temeke, Sofia, anasema kwamba ameshangazwa na kuwapo kwa ada nafuu katika shule ya Twayyibat.

UNESCO watembelea kijiji cha Ololosokwa

DSC_0022
 Afisa Miradi ya Mawasiliano, Habari na Tehama wa Shirika la Kimataifa la Sayansi, Elimu na Utamaduni (UNESCO) Al Amin Yusuph akibadilishana mawazo na Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) Tanzania, Zulmira Rodrigues (aliyeipa mgongo kamera) wakati wa ukaguzi wa mwisho wa eneo la mradi wa kijiji cha digitali wa Samsung unaoendeshwa na UNESCO lilitolewa na serikali ya kijiji. Katikati ni Mwenyekiti wa kijiji cha Ololosokwan wilaya ya Ngorongoro, Kerry Dukunyi .(Picha zote na Zainul Mzige wa modewjiblog)

Na Mwandishi wetu, Ngorongoro
SHIRIKA la Elimu ,sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa, UNESCO, limeanza maandalizi ya kuumilikisha mradi wa kijiji cha digitali cha Ololosokwan kwa wananchi wa kijiji hicho kwa kuendesha warsha ya siku mbili ya kutambua vipaumbele vya wananchi vitakavyoingizwa katika mradi huo.

Vipaumbele hivyo ni katika elimu, afya na uchumi.
Warsha hiyo ilishikirikisha wanakijiji wa Ololosokwan na vijiji vingine vinavyozunguka kijiji hicho,viongozi wa halmashauri, viongozi wa kimila, viongozi wa vijiji na wataalamu mbalimbali wa sekta ya afya, elimu na uchumi.

Katika majadiliano yao wananchi walitambua changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo ambazo zina uhusiano wa moja kwa moja na mazingira na mfumo wa utamaduni walionao wakazi wa eneo hilo.
DSC_0042
Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) Tanzania, Zulmira Rodrigues akikagua eneo la mradi wa kijiji cha kidigitali Ololosokwani wilayani Ngorongro. Kushoto ni Mwenyekiti wa kijiji cha Ololosokwan, Kerry Dukunyi na Mratibu wa miradi wa Taasisi ya Irkiramat, Salanga Mako.

Kituo cha Uwekezaji Tanzania chafanya mkutanao na wafanyabiashara wa Ujerumani

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC),Juliet Kairuki (wa pili kushoto) akizungumza katika mkutano maalum kati ya Uongozi wa TIC na ujumbe wa wafanyabiashara kutoka nchini Ujerumani,wenye lengo la kuhamasisha na kukuza Uwekezaji na biashara kati ya Tanzania na Ujerumani,uliofanyika jana jioni kwenye ukumbi wa Mikutano ya kituo hicho,jijini Dar es salaam.Ujumbe huo unaongozwa na Waziri wa Masuala ya Kiuchumi na Nishati wa nchini Ujerumani,Mh. Matthias Machnig (wa pili kulia). Picha zote na Othman Michuzi.
Mratibu wa Uwekezaji wa Kimataifa wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC),Zacharia Kingu akifafanua jambo wakati akiwasilisha taarifa ya uwekezaji katika maeneo mbali mbali nchini wakati wa mkutano maalum kati ya Uongozi wa TIC na ujumbe wa wafanyabiashara kutoka nchini Ujerumani,wenye lengo la kuhamasisha na kukuza Uwekezaji na biashara kati ya Tanzania na Ujerumani,uliofanyika jana jioni kwenye ukumbi wa Mikutano ya kituo hicho,jijini Dar es salaam.
Ujumbe wa wafanyabiashara kutoka nchini Ujerumani pamoja uongozi wa TIC ukifatikia kwa makini taarifa ya uwekezaji iliyokuwa ikitolewa na Mratibu wa Uwekezaji wa Kimataifa wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC),Zacharia Kingu (kushoto).

Tuesday, February 03, 2015

Dkt Nchimbi apongeza mfumo mzuri wa CCM na kuitabiria ushindi wa kishindo

nchimbi 3
Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Sherehe za Maadhimisho ya miaka 38 ya CCM, ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Songea, Dk. Emmanuel Nchimbi akizungumza katika maadhimisho ya miaka 38 ya CCM, yaliyofanyika kitaifa juzi kwenye Uwanja wa Maji Maji mjini Songea, Mkoani Ruvuma.Kutoka kushoto ni Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete, Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, Philip Mangula na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana.

Na Mwandishi Wetu
Mwenyekiti wa maandalizi ya sherehe za maika 38 ya Chama Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambaye pia ni mbunge wa Songea mjini Dkt Emmanuel Nchimbi amesema kuwa chama chake kina kila sababu ya kushinda kwa kishindo kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka huu kwa kuwa kina mfumo na muundo imara.

Akizungumza muda mfupi baada ya maadhimisho hayo mjini Songea, Dkt Nchimbi ambaye pia ni mjumbe wa halmashauri kuu ya chama hicho alisema kuwa chama chake hakina tatizo la kimfumo wa muundo na kuongeza kuwa ushindi ni lazima.

“Chama hakina tatizo la muundo wala mfumo na tutakachofanya ni kubadilisha mikakati tu ili kujihakikishia ushindi katika uchaguzi ujao,” alisema
nchimbi 4
Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Sherehe za Maadhimisho ya miaka 38 ya CCM, ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Songea, Dk. Emmanuel Nchimbi akizungumza na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe katika maadhimisho ya miaka 38 ya CCM, yaliyofanyika kitaifa juzi kwenye Uwanja wa Maji Maji mjini Songea, Mkoani Ruvuma katikati ni mwenyekiti wa CCM mkoa wa Ruvuma Oddo Mwisho.

Aliongeza, “Kwa kwa kaida hakuna mkakati unadumu. Mar a zote mikakati hubadilika kulingana na mazingira na hiki ndicho tutakachokifanya,”
Akizungumzia kuhusu kauli ya mwenyekiti wa chama hicho Rais Jakaya Kikwete kuwataka viongozi wa chama kuwatembelea wanachama na kushawishi wanachama wapya, alisema CCM ni chama kikubwa na ndani yake wapo viongozi waliolala ambao mwenyekiti wa taifa aliwakumbusha kuamka na kufanya kazi.

Temeke yapigiwa saluti na Ilala


NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
CHAMA cha kandanda mkoa wa Dar es salaam DRFA, kimeipongeza timu ya Temeke kwa kutwaa Ubingwa wa Taifa Wanawake,baada ya kuifunga Pwani kwa bao 1-0,kwenye mchezo wa fainali uliopigwa jumapili ya Januari 31 kwenye dimba la Azam Complez huko Chamazi.
Katika fainali hiyo iliyohudhuriwa na waziri mwenye dhamana ya michezo Dk.Fenella Mukangara,imeshuhudiwa Temeke ikijipatia bao lake mnamo dakika ya  66 kupitia kwa mchezaji wao Neema Paul.

Temeke walifanikiwa kutinga hatua ya fainali baada ya kuwafunga ndugu zao Ilala kwa mabao 4-0,huku pwani wakitinga hatua hiyo kwa kuifunga Kigoma mabao 3-2,katika michezo ya nusu fainali.
Mshindi amejinyakulia kitita cha shilingi milioni tatu, makamu bingwa sh. milioni mbili, wakati mshindi wa tatu ameondoka na sh. milioni moja katika michuano hiyo.
Mbali na Temeke kubeba ubingwa huo,pia imefanikiwa kutoa mlinda mlango bora, Belina Julius aliyezawadiwa kitita cha shilingi 500,000/-.

Mchezo wa kutafuta mshindi wa tatu uliwakutanisha, Ilala dhidi ya Kigoma ambapo ilala imefanikiwa kuchukua nafasi ya tatu baada ya kushinda mabao  3-0.
Uongozi wa DRFA,unatoa shukurani kwa mashabiki wa mkoa wa Dar es salaam na maeneo ya jirani,ambao wamejitokeza kwa wingi kushuhudia michuano hiyo,na kuwaomba waendelee na mfumo huo ili kuleta hamasa kwa wachezaji.

Monday, February 02, 2015

TFF yamlilia bosi wa IRFA, John Ambwene wa mkoani Iringa

NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko taarifa ya msiba wa Kaimu Katibu Mkuu wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Iringa (IRFA), John Ambwene Mwakalobo uliotokea jana (Februari 1 mwaka huu) mkoani Iringa baada ya kuanguka akiwa nyumbani kwake.

Taarifa iliyotumwa kwenye vyombo vya habari na Mkurugenzi wa Mashindano wa TFF, Boniface Wambura, ilisema kuwa msiba huo ni pigo kwa wadau wa mpira wa mpira wa miguu kwani wakati wa uhai wake, Mwakalobo alitoa mchango mkubwa akiwa kiongozi. Mwaka 2011 alichaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa IRFA, kabla ya 2012 kushinda nafasi ya Katibu Msaidizi.

Alizaliwa Februari 4, 1954 na kupata elimu ya sekondari katika shule ya Azania, Dar es Salaam na baadaye mafunzo ya ualimu kwenye Chuo cha Ualimu Mpwapwa mkoani Dodoma. Alianzia kazi ya ualimu Newala mkoani Mtwara kabla ya kuhamia mkoani Iringa mwaka 1981. Alistaafu mwaka 2013.

TFF inatoa salamu za rambirambi kwa familia ya marehemu, na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Iringa (IRFA) na kuwataka kuwa na subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu kwa msiba huo.

Marehemu anatarajiwa kuzikwa kesho (Februari 3 mwaka huu) kwao Kyela mkoani Mbeya. Ameacha mke, watoto wanne na mjukuu mmoja. Bwana alitoa, Bwana ametwaa. Jina lake lihimidiwe.

Mwanaharakati wa maendeleo Misima, wilayani Handeni mkoani Tanga, Rashid Kilo auchambua udhaifu wa Mbunge Kigoda

HUU NI UTHIBITISHO TOSHA WA KUKUJUZA WEWE MWANA HANDENI KWAMBA MBUNGE WETU NI MBINAFSI NA MWENYE UCHU WA MADARAKA NA MWENYE KUJALI FAMILIA YAKE.
MH. Mbunge aliingia madarakani mnamo mwaka 1995, wakati Wilaya ya Handeni ikiwa ni moja na Kilindi. Baada ya kutawala miaka 5 aliomba ridhaa ya kuongoza tena mwaka 2000 lakini wakati huu tayari alishaanza kusikia manung'uniko toka kwa Wakilindi na Wanguu waliopo Kilindi sasa, kwa kuwa anawajuwa vizuri misimamo yao, alianza mchakato wa kuigawa Wilaya ili awatenge na kuendelea na wengine ambao kimsingi amewamudu.
Alifanikiwa lengo lake na mnamo 1-7-2002, Wilaya ya Handeni iligawanywa rasmi na ikapatikana Wilaya ya Kilindi. 


Rashid Kilo, mwanaharakati wa maendeleo wilayani Handeni, mkoani Tanga, pichani.
Mwaka 2005, aliomba ridhaa katika SHAMBA lake la Handeni na kupata, kudhihirisha kuwa ni mbinafsi alimpigania dada yake AISHA KIGODA nae akawa mbunge viti maalum toka Tanga. Lakini yeye akiwa Mbunge wa Jimbo, dada yake Mbunge viti maalum, Baba yake Mzee Jabiri Kigoda akiwa diwani wa Kata ya Vibaoni akawa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya, Handeni.

Lakini pia baada ya uchaguzi wa mwaka 2005, aliona kabisa Wazigua baadhi yao wameanza kumchoka hasa wale waishio Handeni mjini, akaanzisha mchakato wa kuligawa Jimbo mwaka 2008. Akaomba ridhaa mwaka 2010 kwa kutumia ukongwe na utajiri alionao akagombea na mdogo wake Aisha kumshawishi aende Kilindi, yeye alifanikiwa kwa sababu nilizotaja ila dada yake alishindwa vibaya na Mh. Bitrice Shelukindo. Hadi mwaka 2012, alifanikiwa kuligawa Jimbo la Handeni na kupata majimbo mawili MJINI na VIJIJINI.

Ili ujue hasa yote kayafanya kimaslahi jiulize katika mgawanyo wa Handeni na Kilindi nasi kubakia na vitu vingi kama majengo ya Boma, Hospitali na Shule ya Sekondari tumepiga hatua zipi zaidi kiuchumi, kielimu na kiafya ambazo tumemzidi sana mtoto wetu Kilindi?
Leo tuna Halmashauri ya Mji Handeni, hii ndio ilikuwa shida yetu sisi wana wa Handeni? Kumlazimisha mkulima na mfugaji wa MSASA, KWAMASAKA, KWAMAGOME, KILIMILANG'OMBE, KWAMALAHO na MISIMA aishi maisha ya kimjini ya kulipia kodi nyumba yake na ardhi yake lisiwe shamba ila plan ya mipango miji haya ndio ameona yanatufaa sana kuliko kuboresha Hospitali kwa vipimo vyote, dawa na chumba cha kuhifadhia maiti, au kupata maji ya uhakika ya bomba ama kuharakisha kupata "A"levo na chuo cha maana Handeni.

Angalia dhana ya mji wakubwa wote wa Halmashauri ya mji ni rafiki zake wastahafu wa Halmashauri ya Wilaya.
Ifike wakati sasa Handeni tuseme basi! Au yeye mwenyewe kwa kuwa ni Alhaj, aone imetosha sasa kufanya dhuluma Handeni.

-MWISHO POLE WEWE ULIYEUMIZWA NA COMMENT HII- Jumatatu njema!


Huu ni mtazamo binafsi wa mwanaharakati Rashid Kilo kutoka Misima, wilayani Handeni, mkoani Tanga aliyouandika kwenye group la Handeni Kwetu kwenye mtandao wa facebook kwa ajili ya kuzungumza na wadau mbalimbali katika group hilo.
 

Saturday, January 31, 2015

Waziri Mukangara mgeni rasmi fainali ya wanawake

Na Mwandi Wetu, Dar es Salaam
Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk Fenella Mukangara atakuwa mgeni rasmi kwenye fainali ya michuano ya Kombe la Taifa Wanawake kati ya Pwani na Temeke itakayochezwa Uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi jijini Dar es Salaam.

Mechi hiyo itakayoanza saa 10.15 jioni itachezeshwa na mwamuzi wa FIFA, Jonesia Rukyaa, na itaonyeshwa moja kwa moja na televisheni ya Azam. Waamuzi wasaidizi ni Hellen Mduma, Agnes Alphonce, na Mwanahamisi Matiku wakati Kamishna ni Ingridy Kimario.

Timu za Ilala na Kigoma zitacheza mechi ya utangulizi kutafuta mshindi wa tatu kuanzia saa 8.00 mchana. Bingwa wa michuano hiyo inayodhaminiwa na kampuni ya Proin na kufanyika kwa mara ya kwanza nchini atapata kombe na sh. milioni tatu.

Makamu bingwa atapata sh. milioni mbili wakati mshindi wa tatu atapata sh. milioni moja. Kiingilio kwenye mechi hizo ni bure.

Maonyesho ya Tanzania Buildex Internatinal Trade Exhibition kufikia tamati leo Januari 31

Na Andrew Chal, Dar es Salaam
MAONYESHO ya Tanzania Buildex Internatinal Trade Exhibition January 29 -31, yanayoendelea ndani ya ukumbi wa mikutano wa Mlimani City Conference, yanatarajia kufikia tamati jioni ya leo.
Direct Sales Agent wa SimbaNET, Lilian Godfrey (kushoto) akiwa na Deusdedit Msafiri  wa SimbaNET, wakiwa kwenye maonesho ya Tanzania Buildex Internatinal Trade Exhibition, Mlimani City.
Maonyesho hayo yaliyoandaliwa na kampuni ya  kigeni kutoka falme za kiarabu  ya S.K.M Air Conditioning LLC na wadau wengine yameshirikisha makampuni zaidi ya 50, ya ndani na nje ya Tanzania ambapo wameonyesha bidhaa zao hizo pamoja na kuuza.

Baadhi ya makampuni yaliyoshiriki kwenye maonesho hayo ni pamoja na kampuni ya huduma za internet ya Simba Net (T) LTD, TRADEX  Corporation, Choice International wasambazaji wa bidhaa za Lontor, ISTSL Limited, Rehoboth, Fairy Delights,  Afri Vision, Dello Enterprises Ltd wasambazaji wa vifaa vya SKF, SATA Ltd, na mengine mengi.

Makampuni hayo ni yale ya bidhaa za ujenzi, vifaa vya magari, vitu vya ndani, bidhaa za viwandani, maofisini na sehemu mbalimbali pamoja na makampuni ya bidhaa tofautitofauti.

Friday, January 30, 2015

Friends Rangers yapoteza mechi kwa kugoma

Mechi namba 120 ya Ligi Daraja la Kwanza (FDL) kundi A kati ya Majimaji na Friends Rangers iliyochezwa jana (Januari 29 mwaka huu) Uwanja wa Majimaji mjini Songea ilivunjika dakika ya 38 baada ya Friends Rangers kugoma kuendelea na mchezo.

Kwa kitendo hicho, Friends Rangers imepoteza mchezo huo. Hatua nyingine za kikanuni zitafuata baada ya kamati inayohusika kukutana.

Wilaya ya Handeni lawamani tena, yalalamikiwa kutaka kubadili jina la Kwachaga bila kushirikishwa wananchi

Mzozo mzito umeibuka katika kijiji cha Kwachaga, Kata ya Kwachaga baada ya baadhi ya viongozi wa serikali ya Kata hiyo kupendekeza kubadilishwa jina la kijiji hicho kutoka Kwachaga na kuwa Turiani, huku Kwachaga ikiitwa kama Komkole. Uamuzi huo umeibua utata mkubwa ikiwa ni mwendelezo wa maamuzi yasiyoshirikisha wananchi wao.

Uamuzi huo unafanana kwa karibu na ule wa kuhamisha kijiji cha Misima, Kata ya Misima na kuingizwa kwenye Halmashauri ya Mji wa wilaya ya Handeni, mkoani Tanga, zaidi ikitumia pia jina la Mabanda badala ya Misima, Wadau mbaalimbali wa maendeleo ya Handeni wameanza kutoa maduku duku yao dhidi ya maamuzi hayo, huku gazeti la Majira la Januari 30 likiwa limeandika kwa kirefu kadhia hiyo ilipoanzia hadi ilipofikia wakati huu.


Thursday, January 29, 2015

DC Temeke aipongeza shule ya Twayyaibat kwa ada nafuu

Wadau wa Elimu, Abdulaziz Jaar kulia, akizungumza jambo katika matembezi ya Shule ya Kiislamu ya Twayyibat Islamic Seminary ya Temeke jijini Dar es Salaam. Katikati ni mdau kutoka Yukubu Chamber&Associate.

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
MKUU wa wilaya Temeke, DC Sophia Mjema, ameipongeza shule ya Sekondari ya Kiislamu inayojulikana kama Twayyaibat Islamic Seminary Secondary School kwa kufanya ada nafuu inayoweza kuwafanya wazazi na walezi wamudu gharama za kusomesha watoto kwenye shule binafsi.

mwanafunzi kutoka Twayyibat Islamic Seminari akisoma Quraan katika shule hiyo walipotembelewa na Mkuu wa Wilaya Temeke, Sofia Mjema, hayupo pichani.

DC Mjema aliyasema hayo alipofanya ziara katika shule hiyo na kukuta uongozi wa Twayyaibat, ukitoa ada ya Sh 200,000 tu kwa mwaka, jambo ambalo ni agharabu mno hususan kwa shule za kulipia na zinazomilikiwa na taasisi za kidini.

Akizungumza kwa mshangao mkubwa mbele ya wadau wa elimu, DC Mjema alisema ameshangazwa na shule hiyo kufanya ada nafuu, hivyo ni jukumu la wazazi na walezi kujitokeza kuwasomesha watoto wao kwa nguvu zote.
 Mkuu wa Wilaya Temeke, Sofia Mjema, kulia akimkabidhi cheti Mr Yakubu kwa kutambua mchango wake kwa maendeleo ya shule ya Twayyibat Islamic Seminary, iliyopo Temeke, jijini Dar es Salaam jana.
 Meneja wa Skywadrs Construction, Saeed Pirbaksh Mulla, akipokea cheti cha kutambua mchango wa kampuni yao kwenye shule hiyo. Cheti hicho anakabidhiwa na Mkuu wa Wilaya Temeke, Sofia Mjema, kulia.

Alisema pamoja na ada hiyo kuwa nafuu, ni jukumu la serikali hususan Halmashauri ya Wilaya Temeke kupanga mbinu bora zinazoweza kuisaidia shule hiyo kwa hali na mali ili waweze kufanya kazi ya kutoa elimu kwa kiwango cha juu.

“Hii naweza kuiita shule ya sekondari ya mshangao hasa baada ya kuona unafuu wa ada yake, nikiamini kuwa Dunia ya leo kukuta unafuu wa namna hii unaonyesha namna gani kuna wadau wana mtazamo wenye maendeleo.

Wednesday, January 14, 2015

Bayport yaja na ‘Chagua chochote unachotaka Bayport italipia’

Meneja Masoko na Mawasiliano wa Bayport Financial Services, Ngula Cheyo kushoto, akizungumza jambo na waandishi wa habari hawapo pichani katika uzinduzi wa huduma mpya ya 'Chagua chochote Bayport italipia' jijini Dar es Salaam. Kulia kwake ni Meneja Biashara, Thabit Mndeme.

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
TAASISI ya kifedha ya Bayport Financial Services, imezindua tena huduma mpya inayojulikana kama ‘Chagua chochote unachotaka Bayport italipia’, ikiwa na lengo la kuwapatia mikopo ya bidhaa mbalimbali wateja wao na Watanzania kwa ujumla.


Huduma hiyo ni mwendelezo wa ile 'Mikopo ya Bidhaa' ambapo watu wanakopeshwa bodaboda, sambamba na Bima ya Elimu iliyozinduliwa pia mapema mwaka jana kwa ajili ya kuleta urahisi katika mfumo wa maisha ya Watanzania wengi.


 Ngula Cheyo anazungumza jambo na kulia kwake ni Thabit Mndeme.
Akizungumza katika uzinduzi wa huduma hiyo mpya, Meneja Biashara wa Bayport Financial Services, Thabit Mndeme, alisema huduma hiyo sasa itawapatia fursa wateja wao kukopeshwa magari, nyumba, vifaa vya ujenzi, pembejeo za kilimo, ada ya shule, pikipiki, bajaj, tv, injini ya boti na nyinginezo kwa ajili ya kuwapatia mwangaza mzuri wa kimaisha na kiuchumi.

Alisema kuwa kuanzisha huduma hiyo mpya imetokana na ile ya mikopo ya bidhaa kufanya vizuri tangu ilipozinduliwa mwishoni mwa mwaka jana na kupatikana nchi nzima kwa kupitia matawi yaliyosambaa katika mikoa mbalimbali.
Meneja Biashara wa Bayport Financial Services, Thabit Mndeme kulia akizungumza jambo katika uzinduzi wa huduma mpya ya 'Chagua chochote Bayport italipia', ikiwa ni mwendelezo wa huduma ya mikopo ya bidhaa, ambapo wateja wa Bayport wanapata fursa ya kukopeshwa bidhaa mbalimbali, kama vile nyumba, magari, vifaa vya ujenzi na nyinginezo.
Picha zote na Mpiga Picha Wetu.

 “Bayport ilifanya mazungumzo na wateja wake mbalimbali baada ya kuzindua huduma ya Mikopo ya Bidhaa na kuona mafanikio makubwa waliyopata, hivyo mwaka huu tumeona tufike mbali zaidi kwa kuangalia namna gani Watanzania wanaweza kukopeshwa bidhaa nyingi kwa ajili ya kukuza uchumi wao.

“Ni rahisi mno kupewa mkopo wa chagua chochote unachotaka Bayport italipia kwasababu anachotakiwa kufanya mteja ni kuchagua bidhaa anayoitaka katika duka au msambazaji yoyote aliye karibu naye, kisha atapewa fomu ya malipo na kuipeleka kwenye tawi la Bayport lililo karibu yake ili apate mkopo aliyohitaji,” alisema Mndeme.

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...