Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
JUHUDI za kukuza kiwango cha elimu kinachagizwa na vitu mbalimbali, bila
kusahau taasisi zilizoundwa kwa ajili ya kufanya kazi kwa ushirikiano kwa
maendeleo ya Taifa.
Juhudi hizo zinakwenda sanjari na será zenye tija, ukizingatia kuwa ndio
mfumo bora kwa sekta hiyo nyeti. Hapa Tanzania, miongoni mwa será na mikakati kabambe ni pamoja na ile ya uchangiaji
wa elimu ya juu. Sera hiyo imekuwa ikitekelezwa nchini kwa wanafunzi wa vyuo vya elimu ya
juu tangu mwanzoni mwa miaka ya 1990.
Katika mazungumzo
yaliyofanyika jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Msaidizi wa Habari, Elimu na Mawasiliano wa
HESLB, Cosmas Mwaisobwa (pichani), anasema kuwa será
hiyo imezidi kushika kasi, ingawa ilikuwapo tangu wakati wa ukoloni na baada ya
uhuru hasa baada ya kuanzishwa kwa Azimio la Musoma mwaka 1974.
Anasema kuwa katika
mfumo mpya ulioanza miaka ya 1990, mwanafunzi alitakiwa kuchangia sehemu
ya gharama za elimu tofauti na ilivyokuwa mwanzo ambapo alikuwa akipata bure
elimu ya juu. Kabla ya kuanza kwa mfumo wa uchangiaji, serikali ilikuwa ikitoa kila kitu
kwa wanafunzi waliopata fursa ya kujiunga na elimu ya juu.
“Hata hivyo, kuanzishwa
kwa mfumo huo, kulitokana na mabadiliko ya kiuchumi na kijamii, hivyo kuwezesha
kuanzishwa kwa mfumo wa wananchi kuchangia gharama mbalimbali badala ya
serikali kugharimia kila kitu katika elimu, afya na huduma nyingine.
“Awamu ya kwanza ya kuanzishwa kwa mfumo
huo mwaka 1992, wanafunzi walianza kugharamia nauli za kwenda na kurudi kutoka
chuoni, ada za maombi ya kujiunga na vyuo, ada za
kuandikishwa chuoni na fedha za tahadhari,” alisema.
Aidha, wanafunzi walilipia ada za serikali za wanafunzi vyuoni. Awamu ya pili ya
uchangiaji katika elimu ya juu ilitekelezwa kuanzia Julai, 1994. Pamoja
na gharama zilizohamishiwa kwa wanafunzi na wazazi katika awamu ya kwanza,
wanafunzi waligharamia mahitaji ya chakula na malazi.
Hata hivyo, gharama
hizo zilionekana kuwa kubwa na serikali kuanzisha utaratibu wa utoaji mikopo
kwa wanafunzi kwa ajili ya gharama za chakula na malazi, huku utaratibu huo
ukianzishwa rasmi awamu ya tatu chini ya Rais Benjamin William Mkapa, mwaka
2005. Ndio hapo ilipoanzishwa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu
(HESLB), ambayo ilianza shughuli zake rasmi shughuli zake Julai, 2005.