https://tpc.googlesyndication.com/simgad/8045142562622600543


Recent Post

Saturday, April 05, 2014

Navy SC, Abajalo, Mshikamano kuwakilisha Dar Ligi ya Mabingwa wa mikoa



Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
CHAMA Cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA), kimetangaza timu tatu zilizofanikiwa kucheza Ligi ya Mabingwa wa Mikoa baada ya kufanya vizuri katika Ligi Daraja la Pili Mkoa wa Dar es Salaam iliyomalizika Jumapili iliyopita.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Afisa Habari wa DRFA, Mohamed Mharizo, alisema timu hizo ni Navy SC ya  Temeke iliyokua vinara baada ya kujizolea pointi 34 ikifuatiwa na Abajalo ya Sinza iliyojikusanyia pointi 31 na Mshikamano ya Temeke iliyokua na pointi 30.

“Ligi yetu naweza kusema ilikua bora na yenye ushindani kwa sababu tulianza raundi ya kwanza tukiwa na timu 32 na baadae zikabaki timu 16 ambazo katika hizo tatu ndio zimefanikiwa kuwakilisha mkoa wetu wa Dar es Salaam katika Ligi ya Mabingwa wa mikoa inayotarajia kuanza Aprili 20 mwaka huu.

“Kwa niaba ya uongozi wa DRFA, tunazipongeza timu hizi na tunaamini kwa dhati kabisa kuwa zitatuwakilisha vyema katika Ligi ya Mabingwa wa mikoa na hatimaye kufuzu kucheza Ligi Daraja la Kwanza,” alisema Mharizo.

Yanga: Hatuna presha na Simba



Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
UONGOZI wa klabu ya Yanga, umesema kwamba hawana presha na mechi yao ya Aprili 19 dhidi ya Simba SC, badala yake wanaelekeza nguvu kwa mechi nyingi kabla ya kuvaana na mtani wao wa jadi katika Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.

Yanga kwa sasa imeweka kambi yao mjini Bagamoyo, ambapo Jumapili wataingia uwanjani kumenyana na timu ya JKT Ruvu ya mkoani Pwani, huku wakiwa na mipango kabambe ya kuhakikisha kuwa wanaibuka na ushindi mnono.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, Afisa Habari wa Yanga, Baraka Kizuguto, alisema kuwa ingawa watu wamekuwa wakiangalia zaidi mechi ya Simba, lakini timu yao inakabiriwa na michezo migumu mno, hivyo hawaoni sababu ya kuwekeza katika mechi moja ya watani.

Alisema mipango yao ni kunyakua ubingwa wa Bara na sio kumfunga mtani wa jadi, huku wakishindwa kutetea taji lao ambalo kwa sasa linaelekea kuchukuliwa na timu ya Azam baada ya kufikisha pointi 53, huku Yanga wao wakishika nafasi ya pili wakiwa na pointi 46.

“Hatuwezi kuwekeza zaidi mechi ya Simba wakati tuna mechi nyingine ngumu, ikiwamo ya JKT Ruvu, hivyo tunakwenda hatua kwa hatua kwa ajili ya kuiweka timu yetu katika mazingira mazuri ya kutetea taji letu la Ligi ya Tanzania Bara.

“Tusipokuwa makini tunaweza kuifunga Simba lakini tukapoteza mechi nyingine, hivyo kusababisha kuuweka rehani ubingwa wetu wakati ndio mipango tunayoiweka kuhakikisha kuwa kila kitu kinakwenda vizuri kwa kufanya maandalizi ya kila mechi na si ile ya watani wa jadi tu,” alisema.

Ligi ya Tanzania Bara imezidi kukolea joto huku timu ya Yanga na Azam zikionekana kukabana koo kuwania taji hilo, ambapo kwa mtani wake wa jadi Simba, msimu huu ameonekana hana chake baada ya kupata matokeo mabaya kwenye mechi zake.

TAZARA wapinga vifaa bandia vya Simba



Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
KATIBU mwenezi wa tawi la Simba la TAZARA lenye maskani yake jijini Dar es Salaam, Alfred Mdemu, amesema kwamba watawashawishi wanachama wao wanaotokea katika tawi lao kujilinda na ununuaji wa vifaa vya michezo vyenye nembo ya Simba ambayo ni batili.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Mdemu alisema katika kulifanyia kazi suala hilo, kila mwanachama wao lazima anunuwe vifaa hivyo mahali panapojulikana au kuagizwa kwa pamoja kutoka sehemu husika.

Alisema kununua jezi ya Simba ambayo ni bandia hakuwezi kuisaidia klabu hiyo kwakuwa fedha zao zinakwenda kwa wafanyabiashara wachache wasiokuwa na malengo ya kuiletea mafanikio klabu yao hiyo yenye maskani yake jijini Dar es Salaam.

“Kuanzishwa kwa matawi ya Simba kuende sambamba na kufanikisha maendeleo kwa kuhakikisha kuwa wanachama wananunua vifaa halali vya michezo, zikiwamo jezi ambazo timu nyingi ndio biashara halali.

“Kwa sisi TAZARA tunajipanga kuona namna gani tunanunua vifaa halali tukiamini ndio klabu yetu itaingiza fedha nyingi badala ya kununua kwa watu ambao sit u hawatambuliki, bali pia vifaa vyao vinakuwa vya bandia,” alisema Mdemu.

 Tawi la Simba TAZARA lina wanachama 176, huku likiwa na mipango kabambe ya kuhakikisha kuwa ujio wao huo unakuwa na tija kwa klabu yao inayoongozwa na Ismail Aden Rage kwa sasa.

Migogoro ya ardhi inavyoitafuna wilaya ya Handeni



Katibu wa Baraza la Kata ya Kwamatuku, wilayani Handeni, mkoani Tanga, pichani.
Na Kambi Mbwana, Aliyekuwa Handeni
“KATIKA nchi kama yetu, ambayo Waafrika ni masikini na wageni ni matajiri, kuna uwezekano mkubwa kwamba Mwafrika akiruhusiwa kuiuza ardhi, katika miaka themanini au miaka ijayo, ardhi yote ya Tanganyika itamilikiwa na matajiri wageni, na wenyeji watakuwa watwana.

“Lakini hata kama wageni wasingekuwa matajiri, litaibuka tabaka la Watanganyika matajiri wajanja. Tukiruhusu ardhi iuzwe kama kanzu, katika muda mchache, kutakuwa na kundi dogo la Waafrika wakiwa na ardhi na walio wengi watakuwa watwana.” Haya ni maneno ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambare Nyerere.


Mwalimu Nyerere ambaye kwa sasa ni marehemu, aliyasema haya mwaka 1958, kauli ambayo hadi sasa inaendelea kuishi. Mengi yanatokea katika migogoro ya ardhi. Wachache wanamiliki ardhi, huku wananchi wengi wakibaki kama watwana.

Mjumbe wa Baraza la Kata ya Kwamatuku, wilayani Handeni, mkoani Tanga, Mwanahamisi Nyata, pichani.
Nimelazimika kuanza na kauli ya Nyerere baada ya kuona jinsi Tanzania inavyogubikwa na migogoro ya ardhi. Kila kona zinasikika kauli tata au vilio vya wananchi wengi wakionyesha jinsi wanavyotafunwa na kadhia hiyo.

Thursday, April 03, 2014

SIWEZI KUVUMILIA: Ligi isha nisikie vibweka vya majina ya usajili

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam

KUNA wakati unaweza kupata uchizi unapoangalia vitu ambavyo kwa bahati mbaya havikufurahishi. Unachofanya ni kuviacha vipite ili visisumbuwe akili yako. Kwa bahati mbaya, unashindwa maana baadhi ya vitu hivyo vinakukereketa kupita kiasi. Hatua hiyo inakufanya uanze kuviwaza hali ya kuwa ulijiapiza kuacha kuvifikilia na kuviweka moyoni na akilini mwako.

Moja ya wachezaji mahiri wanaotoka nje ya nchi, Khamis Kiiza, akikipiga katika klabu ya Yanga ya jijini Dar es Salaam, nchini Tanzania.
Katika soka la Tanzania, huwa nawaza kila kinapofika kipindi cha usajili. Kuanzia tetesi hadi dirisha hilo linapofunguliwa na kufungwa, utashangaa majina mengi kutajwa.

Wakati mwingine, wanaotajwa si wale wenye kiwango kizuri. Tena kuonyesha umbumbumbu wetu, majina hayo hupendekezwa na watu wasiojua lolote juu ya mambo ya kiufundi uwanjani. Mvutano huo baadaye unazalisha timu isiyokuwa na kiwango chochote katika mechi za ndani na nje ya nchi. Mbaya zaidi, timu nyepesi inapotokea, mashabiki nyanya nao huinuka na kuanza kumsema vibaya kocha wao.

Hapo ndipo nisipoweza kuvumilia. Kwa soka la Tanzania, hata aje mzee Alex Ferguson aliyestaafu akiwa na mafanikio lukuki ndani ya timu yake ya Manchester United, kamwe hawezi kudumu.

Simba waapa kufia uwanjani kusaka heshima



Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
UONGOZI wa klabu ya Simba SC, umesema ingawa wapo kwenye nafasi ngumu kuwania nafasi ya tatu ya msimu wa Ligi, ila wataendelea kujipinda hadi dakika ya mwisho, ili waone wamevuna jambo gani kwa manufaa ya timu yao.

Akizungumza jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki, Msemaji wa Simba, Asha Muhaji, alisema bado hawajakata tamaa katika ligi ya Tanzania Bara, ingawa bado hali imeendelea kuwa mbaya kwa upande wao.

Alisema benchi la ufundi na wachezaji wao wamekuwa wakifanya bidii, ila matokeo mabaya hayawakatishi tamaa ya kuendelea kusaka heshima ya klabu yao, ingawa alikiri kuwa mambo yatakuwa magumu kutokana na ushindani uliopo katika kuelekea mwisho wa Ligi ya Tanzania Bara, inayodhaminiwa na Vodacom Tanzania.

“Mechi yetu na Azam ilimalizika kwa kushuhudia tukifungwa bao 2-1 ila bado hatujakata tamaa ya kuendelea kupigania nafasi za juu, ingawa juu ya ubingwa inaonekana dhahiri kuwa tumejitoa katika mchakato huo,

“Lolote linaweza kutokea katika kuelekea mechi za mwisho za ligi ya Tanzania Bara, hivyo naamini vijana wetu wataendelea kupigania heshima ya timu yao ya Simba,” alisema,

Kufanya vibaya kwa timu ya Simba, kumepokewa vibaya na mashabiki wao, hali inayowafanya waelekeze nguvu zao kuishangilia Azam FC, wakiwa na maana ya kuwabeba ili mtani wao wa jadi, Yanga asiweze kutwaa taji hilo.

Asha Baraka awapiga vijembe wapinzani wake



Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
MKURUGENZI wa bendi ya The African Stars, Twanga Pepeta, Asha Baraka, amewapiga vijembe wapinzani wake, akisema kuwa wamekuwa wakiuchunia ukumbi wa Club Billicanas kwasababu ni mgumu kwao.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, Asha alisema hiyo ndio sababu ukumbi huo, unakimbiwa na bendi nyingine zisizokuwa na uwezo wa kuwavuta mashabiki wao popote walipokuwapo.

Alisema hiyo ndio sababu ya bendi yao kuendelea kutamba katika tasnia ya muziki wa dansi nchini, huku akisema wataanza kufanya mambo upya katika ukumbi huo kuanzia leo Jumatano.

“Bendi yetu haijakuwapo Billicanas kwa zaidi ya miezi miwili, lakini hakuna aliyejaribu kuuchukua ili wapige wao siku za Jumatano, badala yake waliufungia vioo.

“Hivyo kuamua kurudi pale ni kuonyesha kuwa Twanga ndio bendi pekee inayoweza kufanya shoo katika maeneo yote na watu wakahudhuria, hivyo huu ni wakati wa kuonyesha ubabe wetu katika muziki wa dansi,” alisema.

Shoo ya Twanga Pepeta leo itakuwa ya kwanza kwa vijana hao tangu waliporejea katika ziara zao za mikoani, ambapo walitembelea mikoa ya Njombe, Ruvuma na  Mbeya.

Wanafunzi wajifyatulia matofali wenyewe kwa ajili ya shule yao ya sekondari wilayani Handeni

Baadhi ya wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Kata ya Kwamatuku, wilayani Handeni, mkoani Tanga wakifyatua matofali kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa shule hiyo. Wanafunzi hawa walikutwa wakiendeleza ujenzi wa jengo linalokusudiwa kuwa Maabara. Picha na Mpiga Picha Wetu, Handeni.

Tuesday, April 01, 2014

Mwanahabari azindua rasmi Katiba ya watu wa Mrijo wilayani Chemba

Mhariri wa Gazeti la Mtanzania Jumamosi, Khamis Mkotya, mwenye shati la Kitenge, akishiriki kikamilifu kuzindua Katiba ya Chama Cha Watu Mrijo wilayani Chemba, mkoani Dodoma, wanaoishi jijini Dar es Salaam. Kulia kwake ni Katibu wa Chama hicho, Yasin Kimwaga. 
 Khamis Mkotya katikati, wakati kushoto kwake ni Shaaban Ng’oka na kulia ni Katibu, Yassin Kimwaga.
Khamis Mkotya katikati akizungumza katika uzinduzi wa Katiba hiyo kwa ajili ya maendeleo ya wananchi wa Chemba.

Pambano la Cheka, Mrusi lasogezwa mbele

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
PAMBANO la Francis Cheka na Varely Brudov wa
Russia lilililokuwa lifanyike Aprili 5 jijini Dar es Salaam limesogezwa mbele hadi litakapotangazwa tena,  lile la Francis Miyeyusho na Ronald Pontillas wa Ufilipino likibaki palepale.


Promota wa pambano hilo, Mussa Kova, pambano la Cheka limesogezwa baada ya Brudov kuvunjika mguu akiwa mazoezini hivyo kutakiwa kutopigana kwa wiki mbili kuanzia Ijumaa iliyopita.  Kova alisema Brudov aliteleza wakati akiwa gym kujiandaa na pambano na Cheka la kuwania ubingwa wa dunia wa WBF kwenye uzani wa light heavy lililopangwa kufanyika jijini Dar es Salaam.


"Baada ya kupokea taarifa ya kuumia kwa Brudov, tuliwasiliana na Rais wa WBF ili tubadilishiwe bondia na WBF walituambia kama bondia atabadirika pambano halitakuwa la ubingwa wa dunia. "Kwa kuwa lengo letu ni kuandaa mapambano yatakayowasaidia mabondia wa Tanzania kupanda kimataifa tuliamua kuliharisha kwa muda hadi Brudov atakapopona ingawa pambano la Miyeyusho na Pontillas litafanyika siku hiyo ya Aprili 5 kwenye ukumbi wa PTA," alisema Kova.


Akizungumzia pambano la Miyeyusho, Kova alisema maandalizi yanakwenda vizuri na kusisitiza kuwa litasimamiwa na chama cha ngumi za kulipwa Tanzania (PST).
"Mabondia wote wako katika hali nzuri ya ushindani, tunategemea Miyeyusho atafanya vizuri na kukabiliana na upinzani wa mpinzani  wake kwani ni bondia mzuri na mwenye kiwango cha juu," alisema Kova.


Katibu mkuu wa PST, Anthony Lutha alisema kama chama wamekamilisha taratibu zote za maandalizi ikiwa ni pamoja na kutoa kibali cha pambano hilo ambalo awali lilitajwa kusimamiwa na TPBF chini ya rais wake, Chatta Michael. "Tunamtaki Miyeyusho maandalizi mema kwani mabondia wa Ufilipino ni wazuri na wanakiwango kikubwa katika masumbwi, hivyo Miyeyusho ajifue kwelikweli ili kumkabili na kutwaa ubingwa," alisema Lutha.

Mdau wa muziki Tanzania, Said Mdoe afiwa na mama yake mzazi

TAARIFA YA MSIBA: MAMA MZAZI WA SAID MDOE WA SALUTI5AFARIKI DUNIA
Marehemu Bi Desta Mohamed enzi za uhai wake.
MAMA mzazi wa mmiliki wa mtandao wa Saluti5, Said Mode -Bi Desta Mohamed - amefariki ghafla Jumatatu ya tarehe 31/3/2014 saa 1 za jioni.
Alipata homa kali Jumapili mchana, akapelekwa hospitali (IMTU) akapata matibabu na kuruhusiwa kurudi nyumbani. Hali yake haikuwa mbaya wala ya kutia mashaka.
Jumatatu akaamka vizuri na akashinda vizuri hadi saa 12 za jioni hali ipoanza kubadilika tena. Akafariki akiwa njiani kupelekwa hospitali.
Msiba uko Dar es Salaam, Mbezi Beach Old Bagamoyo Road kituo cha Zena Kawawa.
Mazishi yatafanyika Jumanne 1/4/2014 saa 10 alasiri kwenye makaburi ya Mbezi Beach (New Bagamoyo Road) mbele kidogo ya  Masana Hospital.
INNA LILLAHI WAINNA ILAYHI RRAAJIUN.

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...