Pages

Pages

Tuesday, April 21, 2015

SIWEZI KUVUMILIA: Malinzi huu si muda wa mnyukano TFF

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam

NI wakati wa Rais wa Shirikisho la Soka nchini (TFF), Jamal Malinzi kukaa chini kwa ajili ya kuangalia namna ya kuendeleza soka letu na si kuonyeshana ubabe na wadau wengine waliokuwa ndani ya sekta hiyo au vinginevyo.


Hii ni kwa sababu mpango huo unaweza kuibua ari na maendeleo ya soka, kuliko ilivyokuwa sasa, hususan mgogoro mzito uliokuwa ndani ya Shirikisho hilo kwa Damas Ndumbaro kuonekana kama vile anawekewa kauzibe.


Soka letu la Tanzania limeshindwa kumea kutokana na wakati mwingi kuwaza siasa zisizokuwa na tija kwa namna moja ama nyingine. Mara zote hakuna mipango kamili ya wadau, wakiwamo viongozi wa soka au wengineo kuibua vipaji vya vijana wetu.


Wanaoibua vipaji hivyo basi ni wale wanaosubiri mwaka wa kampeni kama ulivyokuwa huu, ndipo wanapojihusisha na michezo, hususan huu mpira wa miguu. Hapo ndipo nisipoweza kuvumilia. Siwezi kuvumilia, maana naelewa namna gani tutadumazwa.


Mpira wa miguu ni ajira. Watu wengi duniani wameendelea kimaisha kutokana na kulipwa fedha nyingi kutokana na kucheza mpira wa miguu. HJata hivyo wana michezo hao ingawa wametumia zaidi nguvu zao na maarifa yao, ila pia wametumia juhudi za wadau.


Nchi zao zimejipambanua vizuri kuhakikisha kwamba kila mmoja kwa nafasi yake anatimiza wajibu wake na sio kama Tanzania inayoendeleza soga. Kila mtu akiingia kwenye madaraka ya mpira wa miguu anajaribu kuwawekea wengine kauzibe.


Tulishuhudia hili kwa Katibu Mkuu wa zamani wa kilichokuwa chama cha Mpira wa Miguu Tanzania FAT sasa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Michael Wambura anavyobanwa kila anapojaribu kuingia. Wakati tunatafakari namna ya kuondoa kasumba hiyo, Malinzi tena kwa kushirikiana na kamati zake, anajaribu kumfungia Ndumbaro kujihusisha na soka kwa miaka 2.


Hakika siwezi kuvumilia. Nikajua sasa Malinzi atashirikiana na kila mmoja ili kuona soka letu linapiga hatua na si vinginevyo. Huu ni wakati wa kuangalia upya nyendo zetu. Dosari na vijisababu vya kukomoana si wakati wake.


Kinyume cha hapo tutazidi kudumaa wakati nchi za wenzetu zinapiga hatua na vijana wao wanawika ndani na nje ya nchi zao.

Tuonane wiki ijayo


+255 712053949




No comments:

Post a Comment