Pages

Pages

Wednesday, April 22, 2015

MGODI UNAOTEMBEA:Siasa za kuhubiri amani zitaiweka nchi mahali pazuri


Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam 

WATANZANIA wanajiandaa kupiga kura ya kuwachagua viongozi wao katika Uchaguzi Mkuu mwaka huu, unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba, ambapo watachaguliwa madiwani, wabunge na rais.



Uchaguzi huo unafanyika huku hali ikianza kuonekana kuwa huenda mambo yakawa magumu kwa Watanzania, hususan wale wapenda amani ambao kwa siku za hivi karibuni kumekuwa na matamko yasiyoangalia mustakabali wa amani na utulivu wa wananchi wote. 


Kwa bahati mbaya, matamko hayo hutolewa na baadhi ya wanasiasa ambao kwa hakika wamekuwa wakifuatiliwa au kuaminiwa watu wengi wanaoaamini sera na mikakati yao ya kisiasa. Hii ni mbaya mno. 


Ni mbaya kwa sababu kwa nchi changa kama hii, tunahitaji kuwa na busara na kuvumiliana pia. Kila mwanasiasa au Mtanzania yoyote anapaswa kutumia akili katika utoaji wa maneno yake ili kusizue zogo linaloweza kuepukika kwa namna moja ama nyingine. 


Wiki iliyopita tulimsikia mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe akiitaka serikali kuhakikisha kwamba Uchaguzi Mkuu unafanyika. Ni kweli utafanyika. 


Kwa madai ya Mbowe, alihisi kuna mpango wa kusogeza mbele uchaguzi huo. Sawa, lakini hata kama uchaguzi huo utasogezwa mbele, si kwa matakwa ya watu wachache bali kwa kushirikishwa watu wengi, wakiwamo viongozi wa vyama vya upinzani hapa nchini. Chama Cha Mapinduzi CCM pekee hakiwezi kusogeza mbele uchaguzi bila kusikiliza maoni ya wadau, wakiwamo Watanzania. 


Vitendo vya kutoa matamko makali yasiyochujwa ni hatari kwa Taifa letu. Mara kadhaa husikika kwamba nchi haitatawalika. Au kushawishi wananchi waingie barabarani kwa sababu ndogo zinazoweza kuepushwa na kila Mtanzania mwenye mapenzi na nchi yake. 



Tangu nchi yetu upate uhuru walau tumeendelea kubaki kwenye amani na utulivu, ingawa kadri siku zinavyosonga mbele kumekuwa na viashiria vya kutoweka kwa amani yetu. Ni vyema wanasiasa wetu wakatambua umuhimu wao kwenye jamii. Kuondoa amani ya nchi ni rahisi na kurudisha ni kazi kubwa. 


Wakati huu tunaelekea kwenye Uchaguzi Mkuu, vyema pia tukajifunza kutoka kwa wenzetu wanaopigana mara kwa mara. Tuwe wazalendo. Tuipende na kuitukuza amani ya nchi yetu. Kila mtu anayeshabikia uvunjifu wa amani ya nchi hii anapaswa kuonekana hana mapenzi mema na Taifa lake. 


Huu ndio ukweli. Ikumbukwe kuwa mwanasiasa mkubwa mwenye wafuasi wengi ni rahisi kukimbia na kuelekea mahali popote duniani kujihifadhi yeye na familia yake pale kunapotokea vurugu. Lakini mwananchi wa kawaida ambaye hata kula yake ni tabu kamwe hawezi kukwepa vifo au majeraha yatakayochochewa na hao hao wanasiasa kwa sababu zao binafsi.


Watanzania wasikubali. Wakati huu ambao demokrasia inazidi kupiga hatua, vyema pia tukafahamu umuhimu wa amani. Bado najiuliza, kama mwanasiasa yupo tayari kuzua vurugu, je yupo tayari kuongoza makaburi au wananchi waliokuwa na vilema vya maisha? Ni mwanasiasa gani anapenda kuongoza watu omba omba waliopata madhara kutokana na mabomu au mapanga baada ya kuzuka kwa vurugu za kisiasa, hali ya kuwa kungekuwa na njia muafaka ya kudai haki?


Tusiombee mabaya. Waswahili wana msemo wao, maneno huumba. Kauli hizi za utata za vurugu zinazotolewa kila uchao na baadhi ya wanasiasa wetu zina chembechembe zozote za kuipenda na kuilinda Tanzania yetu inayojulikana kama kisiwa cha amani? Watanzania ni waungwana. 


Tangu nchi yao ipate uhuru miaka 54 ya Uhuru wamekuwa wakiishi kwa upendo na kuheshimiana mkubwa na mdogo. Hawajabaguana wala kuwekeana chuki. Kama leo hii tunaona tumeichoka amani, basi ruhusa kuijaribu vurugu. 


Lakini kabla ya kuruhusu hilo, kila mmoja apate fursa ya kuangalia japo mikanda au maandiko yanayohusu vurugu za kisiasa zinavyoweza kuifanya nchi iyumbe na kuangamia kwa kiasi kikubwa mno. Siasa za vyama vingi haijaingia nchini ili kuwafanya Watanzania waanze kuishi kwa mashaka na kutoheshimiana.


 Siasa za vyama vingi imeingia nchini tangu mwaka 1992 kwa sababu ya kuisimamia serikali iliyopo madarakani kwa ajili ya kuhakikisha kwamba nchi inasonga mbele. Ni vyema mipango ikawekwa na kusimamiwa kama inavyotakiwa. 


Tuonapo mwanasiasa anatoa maneno makali yanayochochea vurugu vyema tukamuweka chini na kumkataza pia. Huo ndio ukweli wa mambo. Kumekuwa na watu wanajidanganya kuwa nchi hii itapiga hatua kutokana na vurugu. 


Kwamba hata kwenye uwezekano wa kuwekana chini kujadiliana yenye mbolea, basi hilo lifanyike kwa kutumia nguvu inayoweza kuhatarisha usalama wa nchi yetu. Huu ni wakati wa kuliangalia hilo. 


Wanasiasa wetu kutoka kwenye vyama vyote vya siasa wajiandae kufanya siasa zenye tija. Wafanye siasa zenye kujenga hoja imara na zenye mbolea pia. Binafsi naunga mkono kuzaliwa au kuwa na vyama vingi vya siasa. 


Najua hilo ndio jambo la msingi linaloweza kuifanya nchi yetu ikasonga mbele. Lakini siasa hizo ziwe na tija kwa nchi yetu. Yapo madhaifu mengi yanayoweza kupigwa vita na wanasiasa wetu, wakiwamo wale wa upinzani. 


Vitu kama vile ufisadi, rushwa na majanga makubwa yakiwamo ya ajari barabarani ni kati ya mengi yanayopaswa kukemewa usiku na mchana. Kuhusu hilo la siasa au uchaguzi, bado naamini kuwa ili amani idumu, kila mmoja anapaswa kuweka mbele maslahi ya Taifa letu.

 Tuilinde amani kama mboni ya jicho letu. Siasa zisivuruge amani yetu. Wanasiasa wasivuruge amani ya nchi hii inayopigania kujitangaza kimataifa, sanjari na kukuza uchumi wake. 


Kwa bahati nzuri, mara kadhaa tumeshuhudia serikali ikifanya juhudi kubwa kukaa pamoja na wadau wa maendeleo, wanasiasa juu ya kuangalia namna bora ya kuiongoza serikali hii sikivu, chini ya Rais Jakaya Kikwete. 


Mivutano mingi inayotokea imeishia kwa watu hao kukaa mezani kujadiliana na baadaye kuwa na maazimio mazuri yenye kujenga jamii imara na yenye ushirikiano wa aina yake. Kama kweli lengo ni kuongoza Watanzania, basi pia tuzalishe chembechembe za amani na ustawi wan chi hii. Taifa hili likiingia kwenye machafuko, akina mama na watoto ndio watakaoangamia. 


Kada hizo mbili siku zote zimekuwa zikiishia mahali pabaya kutokana na machafuko yoyote yanayoweza kutukia. Tuna mengi ya kufanya. Tushindane kuliombea mema taifa letu si mabaya.


Huu ni muda wa kuwakemea wale wanasiasa wanaoishi kwa matukio na kauli za utata zinazoendelea kutolewa bila mpango. Muhimu ni nchi yetu kuendelea kuwa ya amani na utulivu. Na kama shida ni kutaka kuiangusha CCM madarakani, zipo njia nzuri zinazoweza kuwapatia wanachokihitaji.
 

Kwa kuwa wapo watu wanaomini baadhi ya wanasiasa au vyama vya siasa hususan vya upinzani vinapenda vurugu, basi ni wakati wao kuachana na mwenendo huo ili wale wasiopenda vurugu waamini kuwa mwanzo walijidanganya ili iwe njia kubwa ya kuwaunga mkono, jambo litakaloongeza nguvu ya siasa ya upinzani nchini Tanzania. 


Kinyume cha hapo, hali ya kisiasa itazidi kuwa ya upande mmoja tu, CCM, huku zikiibuka ghasia kwa sababu wanasiasa hao wa upande wa pili wataamini wamefanyiwa hira ili washindwe, huku kauli zao na misimamo yao ya mara kwa mara ikiwa ni uchungu kwa amani ya Taifa letu. Mungu ibariki Tanzania.

kambimbwana@yahoo.com

0712 053949





No comments:

Post a Comment