Pages

Pages

Thursday, April 23, 2015

KAMBI MBWANA: Mdau wa maendeleo aliyeibuka na kitabu cha Dira na Tumaini Jipya Handeni

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
KULALAMIKA bila kutoa suluhisho ni kujipotezea muda. Ndivyo unavyoweza kusema unapoanza kuelezea wazo la kuandikwa kitabu cha Dira na Tumaini jipya Handeni, kilichoandikwa na Kambi Mbwana, moja ya wana harakati wa kimaendeleo hapa nchini.
Mwandishi wa kitabu cha DIRA NA TUMAINI JIPYA HANDENI, Kambi Mbwana, pichani.
Kitabu hicho kilichoangazia mambo mengi ya kijamii kama vile kero ya migogoro ya ardhi, shida ya maji, ukosefu wa elimu ya uraia na namna bora ya kujikwamua  kiuchumi kwa  kutumia fursa mbalimbali zinazopatikana.
Kwa muda mrefu sasa, vijana wengi wamekuwa wakijiweka ‘busy’ katika kulaumu mifumo kadhaa, wakiwamo viongozi kama vile madiwani, wabunge na watendaji mbalimbali wa  serikalini.


Katika kulaumu huko, baadhi yao wanakosa muda muafaka wa kufanya kazi nyingine za kuwakwamua  kiuchumi au hata kutimiza wajibu wao kama wananchi, badala ya kuendelea kulaumu siku hadi siku.

Katika mazungumzo yaliyofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita, Mbwana anasema kwamba wilaya ya Handeni ina changamoto nyingi zinazopaswa kuorodheshwa kwa ajili ya kuangalia namna bora ya kuzitatua.


Hali hiyo ilimfanya afanye ziara katika maeneo mengi ya wilaya hiyo kwa ajili ya kuandika kitabu ambacho kimeanza kuwafikia watu mbaalimbali wenye uelewa wa kusoma vitabu ili kutanua ubongo wao.


“Sijasubiri viongozi wa serikali au wanasiasa wafanye wao kila jambo, ndio maana nikapata wazo hili la kuandika kitabu cha Dira na Tumaini Jipya Handeni, ambacho kama wananchi watakielewa na kukisomaa, agharabu hata wale wenye kiu ya kuboresha maisha yao na si wananchi wao.


“Ukiacha hayo mambo ya kisiasa, bado wananchi hawaelewi namna gani wanaweza kuongeza kipato chao kwa kujihusisha na kilimo bora, ufugaji wa kuku, mbuzi, ng’ombe na shughuli  nyingine halali kwa ajili ya kuwapatia maisha bora, badala ya kutegemea kilimo cha mazoea ambacho ni mahindi pekee na kuyategemea kwa chakula na biashara,” alisema.


Mbwana ambaye pia ni mwandishi wa habari za michezo anasema kitabu chake kimetaja kero kadhaa na namna ya kuzitatua, hivyo ni jukumu la kila mmoja kukipata kwa ajili ya kuona namna bora inavyoweza kumnufaisha kwa namna moja ama nyingine.


Anasema wazo la kuandika kitabu limetokana na umuhimu wakutoa elimu ya uraia kwa wananchi sanjari na kutumia kipaji chake kwa ajili ya kushirikiana na jamii yao, hususan kwa wilaya ya Handeni yenye uhitaji wa majarida, vitabu, makongamano na mikutano ya hadhara yenye dhamira ya kuwabadilisha kifikra na kimtazamo ili wapige hatua.

Wilaya ya Handeni licha ya kuwa kongwe, lakini ina changamoto nyingi, hivyo ni jukumu la kila mwananchi kutimiza wajibu wake kwa ajili ya kuitangaza kwa kupitia sekta mbalimbali.

Kwenye suala la migogoro ya ardhi, wananchi wengi hawajui kama wanapaswa kuhoji au kusimamia watu wote waliopata ardhi kinyume cha sheria katika maeneo yao. Hii inawafanya watu wamiliki ardhi kinyume cha sheria na wengi wao wanawakandamiza walalahoi.


Mbwana pia anasema yapo maeneo ambayo viongozi wa serikali na wananchi wao hawana ushirikiano. Anaitaja Misima ambayo sasa inajulikana kama Kata ya Mabanda, upo mgogoro mkubwa unaoweza kuhatarisha usalama wa raia na mali zao, chanzo kikiwa ni eneo hilo kuingizwa kwenye Mamlaka ya Mji bila kushirikishwa.


Hali hiyo inawafanya viongozi washindwe kuzungumza na wananchi wao kwa hofu ya kuzua mtafaruku au aibu, pale anapopita viongozi wa juu wa serikali, jambo linalohitaji kuangaliwa upya.


“Wilaya hii yenye shida lukuki inapaswa kwanza kutambua changamoto hizi, kuzikubali na kushirikiana pamoja kwa ajili ya kuzitatua kwa kuhakikisha kuwa kila mtu anatimiza wajibu  wake.


“Hata hili wazo la kuandika kitabu ni kwa sababu nahitaji kutimiza wajibu wangu, nikiamini kuwa watu hawana uelewa wa mambo mengi, hivyo endapo watasoma machapisho mbalimbali wanaweza kufika mbali,” alisema Mbwana.


Aidha Mbwana anawataka watu kufahamu umuhimu wa kusoma vitabu na jinsi vinavyoweza kuwakomboa wananchi katika kukuza mitazamo yao, bila kusahau namna bora ya kuweza kubadilisha mitazamo yao.


Anasema kitabu hicho kimeandikwa na kuelemea zaidi katika wilaya ya Handeni, ingawa baadhi ya kero au maudhui ya yaliyoandikwa humo yanashabihiana katika maeneo mengi ya Tanzania.


Anawataka wadau wote, wakiwamo viongozi wa serikali na vyama vya siasa kukubaliana na matokeo ya umuhimu wa kuelimisha wananchi wanaoshiriki kuwaingiza watu wengi kwenye nafasi za uongozi, ingawa mara kadhaa wamekosa faida ya jambo hilo.


Mbwana ambaye pia alishiriki kuanzisha wazo la kuundwa kwa taasisi ya Handeni Kwetu Foundation yenye Makao yake Makuu wilayani Handeni, mkoani Tanga, anasema kuwa changamoto kubwa iliyopo ni kuona baadhi ya watu hawakitaki kitabu hicho kwa faida wanazojua wenyewe.


Hii ni kwa sababu watu hao wanaona kilichoandikwa kwenye kitabu hicho kikitumiwa vyema na wananchi kinaweza kuleta athari kutoka kwa baadhi ya watu wasiokuwa na dhamira ya
kuwakomboa wananchi wao.


“Nimeweza kuchapa nakala 1000 za kuanzia ambapo nimejibana mno katika kuandaa kitabu hiki, hivyo kwa bei ya Sh 3500 kwa kitabu kimoja, niliamini kuwa endapo kitanunuliwa vizuri, ningeweza kuchapa nakala nyingine ili kiweze kusambaa katika maeneo mengi zaidi, maana lengo si kutajirishwa na kitabu hiki, ila kuwaelimisha wananchi wenzangu.


“Wakati ambao naendelea kukisambaza, ni wakati wa wadau kukinunua au kunisaidia namna ya kukisambaza kwa wananchi, yakiwamo mashirika, taasisi za serikali, wadau wa maendeleo kwa mmoja kwa mmoja, bila kusahau vyama vya siasa ambavyo navyo vinapaswa kusambaza nakala ya kitabu hiki, ukizingatia kuwa lengo ni moja kuwazindua wananchi, maana kwa miaka kadhaa sasa wananchi wameendelea kudidimia licha ya kuwa kwenye wilaya yenye rasilimali nyingi, kama vile ardhi, dhahabu nk,” alisema.


Maeneo ambayo tayari kitabu hicho kinapatikana ni Handeni Mjini kwa Ayubu Magazeti, Misima, Sindeni, Kwamatuku, Komsala, wakati Korogwe Mjini kinapatikana Kituo cha mabasi karibu na lango la kutokea kwa Bony muuza magazeti, Tanga Mjini kikipatikana stendi ya zamani, bila kusahau katika baadhi ya maeneo ya jijini Dar es Salaam.


Hata hivyo Mbwana anasema kwamba licha ya kitabu hicho kuuzwa kwa bei ndogo tu ya Sh 3500, lakini bado inaonekana ni kubwa, hivyo anajaribu kuwatafuta wadau wengine wa kimaendeleo katika kushirikiana nao ili watafute namna bora ya kuwapatia kitabu hicho.

 
Habari za kitabu hicho cha Dira na Tumaini jipya Handeni zimeanza kuenea siku chache zilizopita katika mitandao ya kijamii facebook na blogs na baadhi ya magazeti, huku wahitaji wa kitabu hicho wakiombwa kuwasiliana na mwandishi wa kitabu hicho anayepatikana kwa namba +255 712053949 au barua pepe yake kambimbwana@yahoo.com.


Kwa mujibu wa Mbwana, kitabu hicho ni sehemu ya kuwakomboa wananchi na wakazi wa Handeni, ambao kwa miaka kadhaa wameshindwa kupata mwangaza na kuendelea kudidimia kwa kuhakikisha kuwa wanayatumia maandishi yaliyomo kwenye kitabu hicho kupata ufumbuzi wa changamoto zao za kimaisha, hususan katika kipindi hiki ambacho wanasiasa waroho watakapoanza kupitisha fedha chafu, zawadi ambazo zote ni rushwa inayopaswa kupigwa vita.

No comments:

Post a Comment