Na Kambi Mbwana, Handeni
BADO nipo pembeni ya barabara kuangalia msafara wa safari ya
mafanikio ya soka la Tanzania linaloratibiwa na Shirikisho la Soka nchini TFF,
chini ya Rais wake Jamal Malinzi, aliyeingia kwa mbwembwe nyingi katika ofisi
hizo.
Mtu ambaye siku moja baada ya kuingia madarakani alifanya
mabadiliko makubwa kwa kumuondoa Katibu Mkuu wake Angetile Osiah pamoja na
Mkurugenzi wa Ufundi Sunday Kayuni. Yalifuata pia mabadiliko mengine, ambayo
baadhi yake yameshavurugika.
Kubwa ni lile la kutakiwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu
Duniani (FIFA) kurejea katika ofisi zao za zamani zilizokuwapo Karume, Ilala,
jijini Dar es Salaam, badala ya PPF Tower kama walivyodhamiria na kusisitiza
ndipo palipokuwa na hadhi ya TFF mpya.
Pia vurugiko jingine ni baada ya kusitisha kwa mkataba wa
Mkurugenzi wao wa Sheria Evodius Mutawala. Ukiacha hayo, pia yapo matatizo
lukuki ambayo kwa kiasi kikubwa yameonyesha kuwa safari ya TFF mpya ina
mashaka.
Bado haijaanza. Wanaopaswa kuanza safari hiyo, akiwamo
Malinzi mwenyewe bado hajajua anaotaka kusafiri nao, jambo linalonifanya
nishindwe kuvumilia. Bado najiuliza, Tanzania tumedhamiria kweli kusonga mbele
kimaendeleo ya mpira wa miguu au tunacheza shere?
Naona tumekuwa wapiga hadithi tu. Wengine tunajifunza namna
bora ya kulaumu hataa pale tunaposhindwa kutimiza wajibu wetu. Tangu Malinzi aingie
madarakani, sikutaka kusema lolote juu ya safari yake. Ukimya wangu sikutaka
niwe miongoni mwa wanaolaumu mara kwa mara, ila w3akati mwingine mtu anashindwa
kuvumilia.
Ndio hapo ninapopata hoja ya kumuuliza Malinzi, ni kweli una
ndoto ya kukuza soka la Tanzania? Hii ni kwasabababu maneno yamekuwa mengi
kuliko vitendo. Na panapokuwa na vitendo basi vinaonekana havina mashiko.
Bado akili zetu tumezielekeza kwenye mechi za kirafiki za
Taifa Stars. Labda tunaamini mashabiki wanaweza kuingia kwa wingi, hivyo
gharama za kambi kujilipa. Kama huo ni uongo, basi upo karibu kabisa na ukweli.
Akili nyingine ipo kwa Simba na Yanga, ingawa tunajua kuwa bado hatuna mfumo
unaowaibua vijana na watoto kutoka vijijini.
Ndio hapa tunapohitaji wana mkakati wa TFF wenye mipango
kabambe kwa ajili ya kufanya mchakamchaka maeneo ya Tanzania kutafuta vipaji si
kwa kuwachagua mmoja mmoja wakiwa wamekaa vijiweni, ila tuandaye ligi bora
kuanzia ngazi ya Kata, wilaya na Mkoa ili tupate wachezaji wengi wenye vipaji
ambao ndio uti wa mgongo wa soka letu.
Kinyume cha hapo tupiga soga, miaka isonge.
Tuonane wiki ijayo