Pages

Pages

Monday, October 06, 2014

SIWEZI KUVUMILIA:TFF mpya bado imesimama, haijaanza mwendo


Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam

BADO nipo pembeni ya barabara kuangalia msafara wa safari ya mafanikio ya soka la Tanzania linaloratibiwa na Shirikisho la Soka nchini TFF, chini ya Rais wake Jamal Malinzi, aliyeingia kwa mbwembwe nyingi katika ofisi hizo.


Mtu ambaye siku moja baada ya kuingia madarakani alifanya mabadiliko makubwa kwa kumuondoa Katibu Mkuu wake Angetile Osiah pamoja na Mkurugenzi wa Ufundi Sunday Kayuni. Yalifuata pia mabadiliko mengine, ambayo baadhi yake yameshavurugika.


Kubwa ni lile la kutakiwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani FIFA kurejea katika ofisi zao za zamani zilizokuwapo Karume, Ilala, jijini Dar es Salaam, badala ya PPF Tower kama walivyodhamiria na kusisitiza ndipo palipokuwa na hadhi ya TFF mpya.


Pia vurugiko jingine ni baada ya kusitisha kwa mkataba wa Mkurugenzi wao wa Sheria Evodius Mutawala. Ukiacha hayo, pia yapo matatizo lukuki ambayo kwa kiasi kikubwa yameonyesha kuwa safari ya TFF mpya ina mashaka.


Bado haijaanza. Wanaopaswa kuanza safari hiyo, akiwamo Malinzi mwenyewe bado hajajua anaotaka kusafiri nao, jambo linalonifanya nishindwe kuvumilia. Bado najiuliza, Tanzania tumedhamiria kweli kusonga mbele kimaendeleo ya mpira wa miguu au tunacheza shere?

Naona tumekuwa wapiga hadithi tu. Wengine tunajifunza namna bora ya kulaumu hataa pale tunaposhindwa kutimiza wajibu wetu. Tangu Malinzi aingie madarakani, sikutaka kusema lolote juu ya safari yake. Ukimya wangu sikutaka niwe miongoni mwa wanaolaumu mara kwa mara, ila w3akati mwingine mtu anashindwa kuvumilia.


Ndio hapo ninapopata hoja ya kumuuliza Malinzi, ni kweli una ndoto ya kukuza soka la Tanzania? Hii ni kwasabababu maneno yamekuwa mengi kuliko vitendo. Na panapokuwa na vitendo basi vinaonekana havina mashiko.


Bado akili zetu tumezielekeza kwenye mechi za kirafiki za Taifa Stars. Labda tunaamini mashabiki wanaweza kuingia kwa wingi, hivyo gharama za kambi kujilipa. Kama huo ni uongo, basi upo karibu kabisa na ukweli. Akili nyingine ipo kwa Simba na Yanga, ingawa tunajua kuwa bado hatuna mfumo unaowaibua vijana na watoto kutoka vijijini.


Ndio hapa tunapohitaji wana mkakati wa TFF wenye mipango kabambe kwa ajili ya kufanya mchakamchaka maeneo ya Tanzania kutafuta vipaji si kwa kuwachagua mmoja mmoja wakiwa wamekaa vijiweni, ila tuandaye ligi bora kuanzia ngazi ya Kata, wilaya na Mkoa ili tupate wachezaji wengi wenye vipaji ambao ndio uti wa mgongo wa soka letu.

Kinyume cha hapo tupiga soga, miaka isonge.

Tuonane wiki ijayo

No comments:

Post a Comment