Pages

Pages

Sunday, June 08, 2014

Viongozi Kwamnele wauza ardhi yote, wananchi wawasusa viongozi

Na Mzee wa Bonde, Handeni
WAZEE pamoja na wananchi wa kijiji cha Kwamnele kilichopo kata ya Ndolwa wilayani Handeni, wamesusia mikutano mikuu inayoitishwa na serikali ya kijiji hicho kutokana na kukasilishwa na madai kwamba uongozi wao umeuza ardhi yote ya kijiji kwa wageni.


Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi kijiji hapo mwishoni mwa wiki, baadhi ya wazee walisema kitendo cha kuitishwa mkutano na wao kuhudhuria ni kama nao wameridhia na kupitisha kuuzwa huko kwa ardhi hiyo ambayo imesababisha vijana wao wakose maeneo ya kulima.

Mwenyekiti wa baraza la wazee la kijiji hicho kilichopo tarafa ya Mzundu, Hussein Mavilu pamoja na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) tawi la Mkwajuni, Ahmad Yusuph 'Semsekwa', walidai kwamba licha ya kuuza ardhi hiyo, pia wameuza msitu wa Koluhombwa na Mjatakala wanayoitumia kwa matambiko na faida ya kuleta mvua.

Mwenyekiti huyo alitaja majina 23 ya wageni hao ambao wameuziwa ardhi kwa kiasi cha kuanzia ekari 200 hadi 1,000 hatua ambayo imesababisha hadi mapori ya akiba ya kijiji kukosekana ikiwemo kuuzwa kwa misitu hiyo wanayoitegemea kuleta mvua kijijini hapo.

Mwenyekiti wa CCM akichangia suala hilo, alisema kwamba mbaya zaidi viongozi wa kijiji wakiongozwa na Mtendaji Lameck Feresi, waliwachangisha vijana kiasi cha kati ya sh. 5,000 hadi sh 10,000 kwa lengo la kuwapatia ardhi kutokana kijijini hapo lakini wengi wao hawakupewa na fedha zao kuishia mifukoni mwa viongozi hao.

"Mimi kama Mwenyekiti wa Chama tuliwaita kutaka kuwaweka sawa lakini wenzetu wamekaidi hawataki kutusikiliza wanajiona ni mabwana wakubwa...Mbaya zaidi wanaamua mambo yao kupitia halmashauri ya kijiji halafu wanasema ni wananchi wameamua," alisema Semsekwa.


Wakijibu malalamiko hayo kwa nyakati tofauti Mtendaji wa Kijiji Feresi ambaye wananchi hao hawataki tena kumwona katika kijiji hicho, na Mwenyekiti wake wa kijiji Omari Sufiani, walikanusha madai hayo na kukiri kwamba wameitisha mikutano Agosti na Desemba mwaka jana lakini wananchi hawakutaka kuhudhuria.

Mtendaji huyo aliyekuwa na Mwenyekiti wa kamati ya ugawaji ardhi Shabani Mhina pamoja na Mjumbe wake Bakari Sebo, walisema uongozi wao umewauzia mashamba watu watatu tu na kila mmoja wamemuuzia ekari 100 tu na wengine waliotajwa na wananchi hawakuhusika kuwauzia mashamba wanayomiliki.

Waliwataja watu waliowauzia kwamba ni Japhet ambaye walimuuzia ekari 100 akiwa na mtoto wake na kila ekari moja walimtoza sh. 35,000, Ibrahim Mkaiani na Thomas Ngaiyani pia eari 100 kila mmoja ambazo waliwatoza ekari moja sh. 30,000 ambapo kijiji kilipata shilingi milioni 9.5 ambazo walijengea jengo.

Kuhusu kuuza msitu wa koluhombwa na Mjatakala, viongozi hao walijitetea kwamba wameruhusu kukatwa kwa magogo makubwa kwa mzungu mmoja waliyemtaja kwa jina moja la Zaboya na kisha watendelea kuutunza kufutia msitu huo kuvamia na watu wasiojulikana kutoka Kabuku hivyo waliogopa usitoweke.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa Kijiji hicho Sufiani aliwatupia lawama viongozi wa CCM wa kijiji hicho kwamba kulega kwao kiuongozi pamoja na kutofanya vikao ndiko kulikosababisha uongozi wa kijiji ulaumiwe na wananchi hao na amekiri kwamba hali katika kijiji hicho kwa sasa siyo swari baada ya kuahidi kuitisha mkutano Jumatano ijayo.

No comments:

Post a Comment