Pages

Pages

Monday, April 28, 2014

SIWEZI KUVUMILIA: Nimekerwa na mgogoro wa Coastal Union

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam

WIKI iliyoisha jana nimeimaliza vibaya baada ya kupata habari zilizonipasua kichwa kupita kiasi. Kiukweli sijapendezwa na habari hizo. Ni kuhusu mgogoro mkubwa uliokuwa ndani ya klabu ya Coastal Union, yenye maskani yake jijini Tanga. Awali mgogoro huo ulikuwa siri ya viongozi wao kwa wao.


Sisi wadau wa soka hususan katika timu hiyo, tuling’amua jambo hilo tangu mapema, hasa pale Mkurugenzi wa Ufundi na aliyekuwa mfadhili wao, Nassor Bin Slum, kujitoa pole pole katika majukumu ya klabu hiyo. Kadhia hiyo niliamini ingetoweka. Kumbe nilijidanganya, maana Msemaji wa klabu hiyo, Hafidh Kido, naye akatangaza kujiuzuru kwa kuchoshwa na migogoro.


Hapa ndipo nisipoweza kuvumilia. Siwezi kuvumilia kwasababu kujiuzuru kwa Kido ni mwendelezo mbaya kwa timu hii iliyoanza kupoteza tena thamani yake. Coastal imemaliza ligi ikiambulia nafasi ya tisa, yani chupu chupu kushuka daraja. Kwa timu hii iliyoandaliwa vizuri kiasi cha kuweka kambi ya wiki mbili nchini Oman, inashangaza kwanini imeangukia pua.


Hata hivyo, sisi wadau hatuwezi kushangaa, maana hakuna nyumba yenye migogoro kusha malaika wa kheri akawa ndani yake hata kidogo. Ndio hapo ninapoibuka na kuwataka viongozi wa klabu hii na mashabiki wote kuwa makini. Kama msimu huu imeambulia nafasi ya tisa, basi kuna hatari msimu ujao ikashuka daraja, maana bado haijatulia.

Tanga ilikua tishio kwa kupitia timu hii ikiwa na wachezaji kadhaa wenye ubora, akiwamo Juma Mgunda, Razak Yusuf Kareka, Ally Maumba, Abuu Yasin, Ally Jangalu, Douglass Muhani, Kassa Mussa na wengineo kibao walioweza kuipa hadhi timu hii.


Viongozi waache ubabaishaji na kurudia enzi za mwaka 1988 kwa kuishuhudia mkoa wa Tanga ukichanua, maana timu zake ziliwika kupita kiasi. Taji la Ligi ya Tanzania Bara lilichukuliwa na Coastal union, wakati Kombe la Muungano lilijumuisha timu za Bara za Zanzibar lilichukuliwa na African Sports, wakati Kombe la Taifa linalojumuisha mikoa yote ya Tanzania likichukuliwa na timu ya Mkoa wa Tanga  (Tanga Star).


Haya ndio mambo tunayohitaji kwa manufaa ya soka la Tanzania, hususan mkoa wa Tanga kwa kuona timu hii ambayo ni kioo cha soka mkoani humo kuacha ujinga na kurudia enzi zao. Wakazi na wananchi wa Tanga pamoja na mashabiki wa kandanda watawalaani vikali viongozi wa soka wa Coastal Union wanaoleta urasimu kiasi cha kuwafanya wadau waikimbie timu hiyo.


Mgogoro huo umechagizwa vikali na wanaojifanya miungu watu kiasi cha kuwakimbiza wadau wachanagiaji, akiwamo Bin Slum, hali iliyozidisha chuki na uhasama ndani ya timu hiyo. Naumiza kichwa kuhusu usajiri wa klabu hii msimu ujao na mipango yao kwa ujumla. Nani anaweza kuingiza fedha zake kwa klabu yenye migogoro?


Coastal kuingiza migogoro hali ya kuwa wamemaliza ligi wakiwa nafasi ya tisa? Hii ni aibu na lazima wadau tuhoji uhalali huu. Hakika Siwezi Kuvumilia. Ndio maana nasema wiki yangu ilimalizika vibaya na pengine itazidi kuwa mbaya kwasababu ya ubabaishaji huu wa viongozi wa Coastal Union na pengine inaweza kuwa ishara mbaya kwa klabu hii kongwe jijini Tanga.


Nafahamu soka linaendeshwa kwa fedha. Fedha hizo zingeweza kutoka kwa wadau mbalimbali, kwa bahati mbaya gogoro zito linaibuka katika kipindi cha kuweka mikakati kabambe ya usajiri.

Chonde, chonde Ahmed Aurora, Mwenyekiti wa Coastal Union unapaswa kuliangalia kwa umakini jambo hili maana jahazi linazama wakati wakazi na wananchi wa Tanga walikuamini kuwa utakuwa na maslahi na soka lao, ukizingatia kuwa uso wa soka la mkoani humo lipo kwa timu hii.

Tukutane wiki ijayo.


+255712053949

No comments:

Post a Comment