Pages

Pages

Wednesday, April 30, 2014

Ni mapema kumlaumu Jamal Malinzi

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
NI kawaida ya wadau wa mpira wa miguu kulaumu viongozi pale zinaposhindwa kuonyesha soka safi uwanjani na kupatikana ushindi. Mengi yatasemwa zikiwamo lugha za matusi ili kuhalalisha maneno yao dhidi ya uongozi husika.

Ni haki yao, maana wanachojua wao ni ushindi hata kama kiongozi wanayemlaumu hachezi yeye zaidi ya wachezaji wanaosajiliwa kwa ufundi au kuchaguliwa katika timu ya Taifa (Taifa Stars).

Katika kusema hayo, naamini kwa sasa kila mtu anaangalia uongozi wa rais wa Shirikisho la Soka nchini, TFF, Jamal Malinzi kutokana na mwenendo wa soka letu.

Kwa matokeo mabaya hasa ya Taifa Stars na Burundi, mechi iliyopigwa juzi katika Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam na Stars kulala kwa bao 3-0, maneno makali yataelekezwa kwake, wakiamini uongozi wake unasua sua.

Ni mapema kumsakama Malinzi, isipokuwa wadau wa soka wampe moyo kama kweli wana lengo la kukuza sekta ya mpira wa miguu nchini.

Kabla ya kucheza na Burundi, TFF ilifanya tukio kubwa la kuwatafuta vijana ili kuwaunganisha kwenye Taifa Stars.
Waliofanikiwa kuitwa katika timu hiyo ya maboresho ni Benedict Tinoko, Emma Namwondo, Joram Nason Mgeveja, Omari Ally, Edward Peter, Shirazy Abdallah, Yusufu Suleiman, Said Juma Ally kutoka Mjini Magharibi.
Wengine ni Abubakar Ally Mohamed, Hashimu Ramadhani, Omari Athumani, Chunga Said, Mohammed Seif Said, Ayubu Kassim, Abdurahman Othman, Paul Michael, Mbwana Mshindo na Bayaga Atanas.

Hichi ni kikosi ambacho kiliweza kuungana na wachezaji kama vile Frank Domayo, Simon Msuva, Ramadhani Singano, Aggrey Morris na Said Morad, ambao baadhi yao waliweza kucheza katika mechi iliyomalizika kwa kufungwa bao 3-0 dhidi ya Burundi.

Kama nilivyosema hapo juu, kwa timu kufungwa, kushinda au kutoka sare ni jambo la kawaida katika mpira wa miguu duniani kote.

Hivyo kinachotakiwa ni kuendeleza ushirikiano na kuwaunga mkono wachezaji wa Stars walioitwa kwenye kikosi hicho au watakaoitwa siku nyingine na Kocha Mkuu Mholanzi Martinus Ignatius, maarufu kama 'Mart' Nooij, aliyetambulishwa mwishoni mwa wiki.

Badala ya wadau na mashabiki wa soka kushutumu TFF na viongozi wake, wahamasishe maendeleo ya mpira wa miguu.

Napenda kuona Stars au timu nyingine yoyote ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inafanya vizuri, ila mwisho wa siku lawama zisibaki kwa viongozi, hasa tunapoona juhudi na mikakati ya kimaendeleo.

Hii ni TFF mpya baada ya uongozi wa rais Leodgar Tenga kumaliza muda wake. Bado kunahitajika sera nzuri za kufanikisha ushindi.
Lawama pekee sio njia ya kutuvusha hapa tulipo, maana soka letu lilianza kutumbukia shimoni miaka mingi.

Uvumilivu, ushirikiano na mawazo sahihi yataweza kutufanya tutembee kifua mbele kwa kuona si Stars tu inashinda, bali hata klabu zetu zinazinduka na kuwa vinyozi kwa timu nyingine za nje ya nchi, hasa michuano ya Kimataifa.

Kwa miaka kadhaa sasa timu za Simba, Yanga na nyingine zinazopata nafasi ya kushiriki michuano ya Kimataifa, kama vile Kombe la Shirikisho na Ligi ya Mabingwa Afrika hazipati kitu zaidi ya aibu na kuangukia pua.

Hizi ni changamoto tunazopaswa kuzifanyia kazi kama wadau wa michezo na si kumshushia zigo la lawama rais wa TFF, ambaye ndio kwanza ameingia madarakani.

Tumpe muda na ushirikiano kwasababu kwa mipango aliyoitangaza, nchi yetu ina uwezo wa kusonga mbele, hasa kwa kuboresha timu za vijana.

Mungu Ibariki Tanzania.
+255712053949

No comments:

Post a Comment