Pages

Pages

Sunday, April 27, 2014

Tunapandisha timu tusizozipenda?



Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
LIGI ya Tanzania Bara imemalizika juzi Jumamosi, ambapo Azam FC imefanikiwa kunyakua taji kwa mara ya kwanza, ikiziacha Yanga na Simba zikibaki kujiuliza nini tatizo?
Kikosi cha timu ya Mbeya City pichani.
Hii ni kwasababu wao walionyesha shauku ya kulitwaa taji hilo, hata hivyo maandalizi yao hayajakuwa ya uhakika. Kwa kumalizika kwa ligi hiyo, ni maandalizi ya kuanza kwa ligi ijayo, huku timu tatu zikifanikiwa kupanda daraja, jambo linalowapa fursa ya kushiriki Ligi ijayo itakayokuwa na ushindani wa aina yake.

Timu zilizopanda daraja msimu huu ni pamoja na Stand United ya Shinyanga, Ndanda FC ya mkoani Mtwara na Polisi Morogoro. Timu hizi msimu ujao zitashiriki Ligi Kuu, ambapo kwa sasa ni dhahiri wanapaswa kujiandaa vizuri ili zionyeshe soka lao.

Hata hivyo, ni wakati wa mashabiki wa soka katika mikoa ya Shinyanga, Mtwara na Morogoro kuzithamini timu zao. Mashabiki hawa wa soka waone namna ya kupanga muda wao kuzishangilia timu zao ili zifanikiwe kucheza soka lao la haja.

Mashabiki wa mkoani Mbeya waliweza kuonyesha uzalendo kwa timu yao ya Mbeya City kiasi cha kuifanya kuonyesha cheche zao. Ingawa mashabiki hawa walipunguza mapenzi kwa timu yao ilipofika timu ya Simba au Yanga, lakini bado mashabiki hawa walionyesha shauku na mapenzi kwa timu yao.

Huu ndio uzalendo unaotakiwa. Uzalendo huu ukiendelezwa, walau mafanikio yanaweza kuwa makubwa kwa soka la Tanzania. Hakuna haja ya kuzalisha timu za mikoani ambazo zinakutana na kasumba za Simba na Yanga. Tunahitaji kuona watu wote wa mkoa wa Mtwara wanashirikiana kuibeba timu yao ya Ndanda hata itakapotokea kucheza na Simba au Yanga.

Ukiacha timu ya Polisi Morogoro, inayosimamiwa na Jeshi la Polisi, bado uzalendo ni muhimu kwa timu zote za mikoani. Huu ndio ukweli wa mambo. Kuna haja gani ya kuziacha yatima timu za mikoani? Ndugu zetu wa Coastal Union ya Tanga, Mtibwa Sugar ya Turiani Mogorogo, Kagera Sugar ya mjini Bukoba na timu nyingine zinahitaji ushirikiano wa wadau na mashabiki wa soka wa mikoani kwao.

Kule Ulaya ndio utaratibu wao. Timu za Manchester United, Arsenal, bado si sababu ya mashabiki wa soka Uingereza kushindwa kuzithamini timu zao za Manchester City, Chelsea na nyinginezo. Mtindo huo unawapa faida kubwa. Soka lao linafanya vizuri. Watanzania ni wakati wetu kujifunza na kuweka mikakati yenye kuibua chachu ya maendeleo yetu.

Ni ujinga timu za mikoani kushindwa kufanya vizuri kwasababu ya uzalendo duni wa mashabiki wa soka dhidi ya timu vigogo. Huu ni wakati wa mabadiliko kwa mustakabali wa soka letu Tanzania. Tumeona mara kadhaa timu zetu ndogo zikisua sua kwasababu ya watu kuweka macho yao kwa timu vigogo.

Hivyo suala hili si zuri kwa maisha ya soka. Wakati tunazipongeza timu za Ndanda, Polisi Morogoro na Stand United ya Shinyanga, ni wakati wetu kujua mbinu nzuri za kuziendeleza timu hizi. Tuhamasishe timu zetu. Tununuwe jezi na vifaa vyao vya michezo ili kutunisha pia mifuko yao. Tunapoona wanaishi kwa kubangaiza, wale wenye uwezo wao wajitokeze kunusuru ukata wao ili mambo yao yawe mazuri.

Tanzania yetu ilivyo, mtu anaweza kutumia Milioni 50 kwa timu ya Simba au Yanga, wakati timu yake ya mkoa inasua sua. Huu ni ujinga wa karne. Na ndio maana tumeshuhudia Mbunge wa Singida Mjini, Mohamed Dewji ‘Mo’ akaishindwa timu ya African Lyon, hali ya kuwa bado anaisaidia klabu ya Simba, licha ya timu hiyo kuwa ya kiubabaishaji.

Hili ni jambo la ajabu kupita kiasi. Nadhani wakati huu tunazipongeza timu tatu zilizopanda daraja msimu ujao, vyema wote tukafahamu kuwa tusipokuwa makini, zitashuka daraja kabla hata ya kujiimarisha, ukizingatia kuwa Ligi ya Tanzania Bara ina changamoto lukuki.

+255712053949

No comments:

Post a Comment