Pages

Pages

Wednesday, April 30, 2014

Ni mapema kumlaumu Jamal Malinzi

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
NI kawaida ya wadau wa mpira wa miguu kulaumu viongozi pale zinaposhindwa kuonyesha soka safi uwanjani na kupatikana ushindi. Mengi yatasemwa zikiwamo lugha za matusi ili kuhalalisha maneno yao dhidi ya uongozi husika.

Ni haki yao, maana wanachojua wao ni ushindi hata kama kiongozi wanayemlaumu hachezi yeye zaidi ya wachezaji wanaosajiliwa kwa ufundi au kuchaguliwa katika timu ya Taifa (Taifa Stars).

Katika kusema hayo, naamini kwa sasa kila mtu anaangalia uongozi wa rais wa Shirikisho la Soka nchini, TFF, Jamal Malinzi kutokana na mwenendo wa soka letu.

Kwa matokeo mabaya hasa ya Taifa Stars na Burundi, mechi iliyopigwa juzi katika Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam na Stars kulala kwa bao 3-0, maneno makali yataelekezwa kwake, wakiamini uongozi wake unasua sua.

Ni mapema kumsakama Malinzi, isipokuwa wadau wa soka wampe moyo kama kweli wana lengo la kukuza sekta ya mpira wa miguu nchini.

Kabla ya kucheza na Burundi, TFF ilifanya tukio kubwa la kuwatafuta vijana ili kuwaunganisha kwenye Taifa Stars.

Monday, April 28, 2014

SIWEZI KUVUMILIA: Nimekerwa na mgogoro wa Coastal Union

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam

WIKI iliyoisha jana nimeimaliza vibaya baada ya kupata habari zilizonipasua kichwa kupita kiasi. Kiukweli sijapendezwa na habari hizo. Ni kuhusu mgogoro mkubwa uliokuwa ndani ya klabu ya Coastal Union, yenye maskani yake jijini Tanga. Awali mgogoro huo ulikuwa siri ya viongozi wao kwa wao.


Sisi wadau wa soka hususan katika timu hiyo, tuling’amua jambo hilo tangu mapema, hasa pale Mkurugenzi wa Ufundi na aliyekuwa mfadhili wao, Nassor Bin Slum, kujitoa pole pole katika majukumu ya klabu hiyo. Kadhia hiyo niliamini ingetoweka. Kumbe nilijidanganya, maana Msemaji wa klabu hiyo, Hafidh Kido, naye akatangaza kujiuzuru kwa kuchoshwa na migogoro.


Hapa ndipo nisipoweza kuvumilia. Siwezi kuvumilia kwasababu kujiuzuru kwa Kido ni mwendelezo mbaya kwa timu hii iliyoanza kupoteza tena thamani yake. Coastal imemaliza ligi ikiambulia nafasi ya tisa, yani chupu chupu kushuka daraja. Kwa timu hii iliyoandaliwa vizuri kiasi cha kuweka kambi ya wiki mbili nchini Oman, inashangaza kwanini imeangukia pua.


Hata hivyo, sisi wadau hatuwezi kushangaa, maana hakuna nyumba yenye migogoro kusha malaika wa kheri akawa ndani yake hata kidogo. Ndio hapo ninapoibuka na kuwataka viongozi wa klabu hii na mashabiki wote kuwa makini. Kama msimu huu imeambulia nafasi ya tisa, basi kuna hatari msimu ujao ikashuka daraja, maana bado haijatulia.

Sunday, April 27, 2014

Tunapandisha timu tusizozipenda?



Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
LIGI ya Tanzania Bara imemalizika juzi Jumamosi, ambapo Azam FC imefanikiwa kunyakua taji kwa mara ya kwanza, ikiziacha Yanga na Simba zikibaki kujiuliza nini tatizo?
Kikosi cha timu ya Mbeya City pichani.
Hii ni kwasababu wao walionyesha shauku ya kulitwaa taji hilo, hata hivyo maandalizi yao hayajakuwa ya uhakika. Kwa kumalizika kwa ligi hiyo, ni maandalizi ya kuanza kwa ligi ijayo, huku timu tatu zikifanikiwa kupanda daraja, jambo linalowapa fursa ya kushiriki Ligi ijayo itakayokuwa na ushindani wa aina yake.

Timu zilizopanda daraja msimu huu ni pamoja na Stand United ya Shinyanga, Ndanda FC ya mkoani Mtwara na Polisi Morogoro. Timu hizi msimu ujao zitashiriki Ligi Kuu, ambapo kwa sasa ni dhahiri wanapaswa kujiandaa vizuri ili zionyeshe soka lao.

Hata hivyo, ni wakati wa mashabiki wa soka katika mikoa ya Shinyanga, Mtwara na Morogoro kuzithamini timu zao. Mashabiki hawa wa soka waone namna ya kupanga muda wao kuzishangilia timu zao ili zifanikiwe kucheza soka lao la haja.

Mashabiki wa mkoani Mbeya waliweza kuonyesha uzalendo kwa timu yao ya Mbeya City kiasi cha kuifanya kuonyesha cheche zao. Ingawa mashabiki hawa walipunguza mapenzi kwa timu yao ilipofika timu ya Simba au Yanga, lakini bado mashabiki hawa walionyesha shauku na mapenzi kwa timu yao.

Mashali avunja mazoezi ya kumuwinda Nyilawila

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam


BONDIA Thomas Mashali, amesema kwamba amesimamisha mazoezi kwa muda ya kumkabiri Kalama Nyilawila baada ya kupata ajali ya gari, ila bado si tatizo la yeye kuweza kumvaa Nyilawila na kumuonyesha adabu. 

Bondia Thomas Mashali pichani.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Mashali alisema kuwa ana uhakika wa kumpiga Nyilawila ingawa pambano hilo limesogezwa mbele hadi litakapotangazwa tena na promota wao Ally Mwazoa.


Alisema ajali aliyoipata si kubwa ingawa imemfanya asimamishe mazoezi kwa siku kadhaa kwa ajili ya kuvaana na Nyilawila katika pambano lao.


“Nilipata tatizo kidogo la ajali lakini naamini ni changamoto zitakazonifanya nijiandaye vyema.


“Ushindi kwangu dhidi ya Nyilawila ni muhimu na lazima apigwe kwasababu uwezo wangu ni mkubwa,” alisema.


Kwa mujibu wa Mashali, pambano hilo limesogezwa mbele hadi litakapotajwa tena, hivyo kwake yeye itakuwa ni sehemu ya kujiandaa vizuri.

Serikali ya China kuijengea Zanzibar Uwanja wa Michezo uliopo Kikwajuni



Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
SERIKALI ya Jamhuri ya Watu wa China, imeridhia na kukubali kugharamia ujenzi wa Kiwanja cha michezo kilichopewa jina na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar la Mau Tse Tung, kilichopo miperani Kikwajuni Mjini Zanzibar.

Kauli hiyo imetolewa na Balozi Mdogo wa Jamuhuri ya Watu wa China aliyepo Zanzibar Bw. Xie Yunliang wakati akizungumza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi hapo katika Ofisi yake iliyomo ndani ya Jengo la Msekwa  Bungeni Mjini Dodoma.

Balozi Xie Junliang alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba Timu ya wataalamu wa China inatarajiwa kukifanyia utafiti na uchunguzi kiwanja hicho baadaye mwaka huu sambamba na utiwaji saini makubaliano ya ujenzi wa kiwanja hicho unaotarajiwa kufanyika mapema mwaka ujao.

Alisema ujenzi wa uwanja huo uliopewa heshima ya jina la kiongozi muasisi wa Taifa la China marehemu Mao Tse Tung utajumuisha kiwanja cha mchezo wa soka pamoja na michezo mengine ya ndani mfano mchezo wa Table Tennis.

“Tunatarajia ujeni wa kiwanja cha Mao utakapokamilika utakuwa na uwezo wa kuhudumia wanamichezo wa michezo tofauti ukiwemo ule unaopendwa zaidi wa soka “. Alisema Bwana Xie Junliang.

Balozi Mdogo wa China aliyepo Zanzibar alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba uhusiano wa kidugu uliopo kati ya Zanzibar na Tanzania kwa ujumla pamoja na China unastahiki kuenziwa zaidi.


Twanga Pepeta kupagawisha Leaders Club leo


Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam

BENDI ya The African Stars, Twanga Pepeta, leo itawaonyesha kazi mashabiki wao katika Viwanja vya Leaders Club, jijini Dar es Salaam katika onyesho lao la  bonanza linalofanyika kila Jumapili.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Meneja wa bendi hiyo, Hassan Rehani, alisema onyesho hilo lina mvuto wa aina yake.

Alisema mashabiki wao hupata nafasi ya kuburudisha mashabiki wao kuanzia saa nane mchana hadi saa nne usiku.

“Bonanza la kila Jumapili hutoa fursa kwa mashabiki wote kufurahia burudani za Twanga Pepeta. 
“Tunaamini tutaendelea kuwa pamoja na mashabiki wetu ili kulinda heshima yetu katika muziki huu,” alisema.

Twanga Pepeta ni miongoni mwa bendi zenye mashabiki wengi katika kona ya muziki wa dansi nchini.

Friday, April 25, 2014

Bunge la Maalum la Katiba laahirishwa hadi Agosti 5, mwaka 2014 kuendelea na mijadala ya kutengeneza Katiba



Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Bunge la Katiba limeahirishwa hadi Jumanne ya Agosti  5 mwaka 2014 kuendelea na vikao vya kujadili Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Bunge la Maalum la Katiba limeahirishwa huku sura ya kwanza na sita ikiwa imeshika kasi kiasi cha kuibua mizozo iliyozalisha chuki kwa baadhi ya wajumbe.

Wajumbe wengi walionekana kuvutana huku baadhi yao wakipinga serikali mbili wakitaka tatu na wengine kusema serikali tatu ni mbaya zibaki mbili. Mvutano huo ulisababisha Wajumbe wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) kujitoa.

Akizungumza wakati anaahirishwa Bunge hilo Maalum la Katiba leo mjini Dodoma, Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samuel Sitta, alisema kuwa wajumbe watakutana tena Agosti 5, mwaka 2014 kuanzia saa tatu asubuhi.

Alisema kuwa wajumbe wengi wameonyesha kufanya kazi nzuri kuchangia mijadala ya Katiba Mpya, ingawa changamoto zilikuwa nyingi.

“Natangaza kuahirisha Bunge hili nikiamini kuwa tutakutana tena kuendelea na vikao vyetu kwa ajili ya kuitengeneza Katiba Mpya ya Watanzania,” alisema.

Awali wakati anachangia, Mjumbe wa Bunge hilo, ambaye pia ni Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mizengo Pinda, alishangazwa na vijana wadogo kudharau kazi za waasisi wa Taifa hili kwa kisingizio cha kutoa hoja ya Katiba Mpya.

Pitia mchango wa kimaandishi wa Maria Sarungi Tsehai kwa Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba

Mh. Mwenyekiti, naomba nichukue fursa hii nichangie kwa maandishi mjadala unaoendelea bungeni kuhusu sura ya 1 na ya 6 na kuhusu mwenendo mzima wa Bunge lako tukufu.
Mh Mwenyekiti, tokea tumefika Dodoma zaidi ya siku 70 tumeweza kushuhudia mengi, katika huu mchakato wa kujadili rasimu ya pili ya Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Tunamaliza siku rasmi tulizopangiwa bila kufanya maamuzi yoyote kuhusiana na Rasimu na bila muafaka.
Maria Sarungi pichani.
Mh. Mwenyekiti, tunamaliza siku hizi 70, tukiwa tumegawanyika na kuparanganyika katika makundi, na kilichobaki ni kurushiana vijembe, kutukanana, kususiana na kununiana. Bunge lako tukufu lilitakiwa kuwa kioo cha muafaka wa kitaifa ila sasa tumegeuka na kuwa chanzo kinachosababisha mpasuko ndani ya jamii.  Na ikiwa hali hii ya mpasuko ndani ya Bunge itaendelea kuwepo, kuna hatari kubwa ya kuhatarisha amani na utulivu tunaojivunia ndani ya nchi yetu – naomba jambo hili tulisichukulie kama mzaha. 

Mh. Mwenyekiti, kama utakumbuka nilichangia awali kabisa chini ya uenyekiti wa muda wa Mh. Pandu Kificho na nilizungumzia ubabe wa walio wengi (Tyranny of Majority) na jinsi inavyoweza kupelekea mchakato huu kuharibika. Leo maneno haya yametimia. Ieleweke kuwa mi si nabii bali ni mwanafunzi mzuri wa historia. Na siku zote maridhiano na ushirikishwaji wa pande zote ni sehemu muhimu ya mchakato kama huu wa kuandika Katiba.
Mh Mwenyekiti, Tanzania tunasifika duniani kwa kuwa mstari wa mbele kukomboa nchi za kiafrika na kupatanisha mataifa.  Baba wa Taifa letu, Hayati Mwalimu Nyerere aliongoza michakato mingi na mojawapo kubwa ni mapambano ya watu weusi dhidi ya utawala dhalimu na wa kibaguzi wa makaburu huko Afrika Kusini. Nilifarijika sana kumsikia aliyekuwa Rais wa Pili wa Afrika Kusini, Thabo Mbeki katika video akizungumzia juhudi za Mwalimu Nyerere hata katika mchakato wa kuandika katiba yao ya Afrika Kusini. Katiba ambayo inasemekana ni moja ya katiba bora barani Afrika.

Msemaji wa Coastal Union Hafidh Kido atangaza kujiuzuru kwenye klabu hiyo kutokana na kuzuka migogoro mizito



Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
MSEMAJI wa klabu ya Coastal Union yenye maskani yake jijini Tanga Tanzania, Hafidh Kido, ameachia ngazi kutokana na migogoro mizito inayoendelea kuitafuna timu hiyo iliyomaliza ligi katika nafasi ya tisa kwenye msimamo wa ligi.
Msemaji wa zamani wa Coastal Union, Hafidh Kido pichani.
Akizungumza leo asubuhi jijini Dar es Salaam, Kido alisema kuwa amelazimika kujiuzuru ili kulinda hadhi yake katika sekta ya habari kutokana na mikanganyiko ndani ya timu hiyo.

Msemaji wa zamani wa Coastal Union, Hafidh Kido, akiwa katika majukumu yake.
Alisema awali uongozi wa klabu hiyo haukumpa ushirikiano katika majukumu yake, hali iliyolazimika kusaidiwa kwa kiasi kikubwa na aliyekuwa Mkurugenzi wa Ufundi wa klabu hiyo na Mfadhili wao, Nassor Bin Slum.

“Mimi Hafidh Athumani Kido, nikiwa na akili timamu natangaza kutojihusisha na shughuli zote za Coastal Union, hasa usemaji wa klabu, huku miongoni mwa sababu nyingi zilizonifanya kutangaza uamuzi huo ni sintofahamu iliyozuka ndani ya klabu yetu.

“Kwa taaluma yangu ya uandishi wa habari lazima niwe na msimamo juu ya mambo yanayoendelea kwenye jamii ili niendelee kufanya kazi na klabu hii kwa wakati huu wa misuguano, lazima niwe na upande; kwa maana upande unaounga mkono uongozi ama upande usiokuwa na Imani na uongozi,” alisema Kido. 

Kwa mujibu wa Kido, yeye ameamua kutounga mkono upande wowote, akiamini atakuwa katika mstari sahihi na kukaa pembeni ili afanye shughuli zake za uanahabari kwa furaha na amani, huku akisema kuwa ataendelea kuwa mwanachama halali wa Coastal Union Sports Club mwenye kadi 0013.

Mwandishi ageukia muziki wa injili



Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
MWANDISHI mwandamizi wa habari nchini, George Kayala yupo katika hatua ya mwisho ya kukamilisha albamu yake ya nyimbo za injili akiwa chini ya leo ya Best Record inayoongozwa na Mkurugenzi, Benjamin Nzogu.

George Kayala, mwandishi aliyeingia katika muziki wa injili.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Kayala alisema kwa muda mrefu amekuwa na kiu ya kumtumikia Mungu kwa njia ya uimbaji na wakati umefika na anatarajia kuachia kibao kimoja wiki ijayo ambacho kitaanza kusikika kwenye vituo mbalimbali vya redio nchini.

“Kila jambo na wakati wake, binafsi nimekuwa na kiu ya kumtumikia Mungu kwa njia ya uimbaji kwa muda mrefu lakini sikufanya hivyo kwa sababu nilikuwa nasikiliza sauti ya Roho Mtakatifu na sasa ameruhusu nifanye hivyo, hivyo albamu yangu itakuwa tayari muda wowote kuanzia sasa,” alisema Kayala.

Kayala alizitaja nyimbo hizo kuwa ni Siwema, Usinipete, Wamebeba Matatizo,  Jehova Yile, Safisha Moyo Wangu,  Wanijua Vema Bwana na  Unayejibu kwa Moto na mpaka sasa hajapata jina la albamu kutokana na kila wimbo kuwa na sifa ya kubeba albamu.