Pages

Pages

Friday, March 07, 2014

Ushirikina wawaponza Simba, walimwa faini na Bodi ya Ligi



Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
KLABU ya Simba, imepigwa faini ya Sh Milioni moja, baada ya kuhusishwa na vitendo vya ushirikina katika mechi yao dhidi ya Mbeya City.

Mbali na adhabu hiyo, pia mshambuliaji wao Hamis Tambwe, naye amelambwa faini ya Sh 500,000, akihusishwa na kuonyesha alama ya matusi katika mechi hiyo na Mbeya City.

Taarifa kutoka Shirikisho la Soka nchini (TFF) kwa kupitia msemaji wao, Boniface Wambura, alisema kuwa adhabu hiyo imeamuliwa na Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB), iliyokaa Jumapili ya wiki iliyopita kwa ajili ya kupitia mechi mbalimbali za Ligi ya Tanzania Bara na daraja la kwanza.

Wambura alisema kuwa Simba walifanya makosa mbalimbali, hasa vitendo vinavyoashiria ushirikina uwanjani, hivyo kuilazimu Bodi ya ligi iwapige faini.


“Simba walifanya vitendo hivyo katika mechi yake dhidi ya Mbeya City ambapo imepigwa faini ya Sh. 500,000, pamoja na Sh. 500,000 nyingine kwa makocha wake Loga, Selemani Matola na Idd Pazi kwa kudaiwa kuingia kumzonga mwamuzi katika mechi hiyo.

“Naye mshambuliaji wa Simba, Amisi Tambwe amepigwa faini ya Sh. 500,000 kwa kushangilia bao alilofunga kwenye mechi hiyo kwa kuonesha ishara ya matusi kwa kidole,” alisema.

Mbali na Simba, Mbeya City nao walipigwa faini ya Sh. 300,000 kwa washabiki wake kuingia uwanjani kwenye mechi dhidi ya Kagera Sugar iliyochezwa mjini Bukoba, wakati Coastal Union nao walipigwa faini ya kiasi kama hicho kutokana na mashabiki wao kurusha chupa za maji uwanjani.

Wengine waliotozwa faini ni kiungo wa Mtibwa Sugar, Shabani Nditi Sh 500,000,  Salvatory Ntebe Sh 500,000, Musa Mgosi Sh 500,000, Coastal Union Sh 500,000, JKT Ruvu Sh 300,000.

Kwa upande wa Ligi Daraja la Kwanza (FDL) klabu zilizopigwa faini ni Friends Rangers (sh. 200,000), Lipuli (sh. 200,000), Majimaji (sh. 400,000), Polisi Morogoro (sh. 400,000) na Transit Camp (sh. 200,000).

No comments:

Post a Comment