Pages

Pages

Tuesday, March 04, 2014

Hongereni Twiga Stars, hakuna wa kuwalaumu


Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam

YOYOTE anayeza kuinua kinywa chake kuwalaumu wachezaji wa timu ya Taifa ya wanawake Twiga Stars, huyo atakuwa na moyo wa chuma kupita kiasi.


Ni kwasababu timu hiyo imekuwa ikijiendesha kwa kubangaiza ufundi na namna ya kulinda vipaji vyao vya mchezo wa soka.

Baadhi ya wachezaji wa Twiga Stars wakishangilia moja ya mechi zao uwanjani.
Inashangaza kidogo, kunakuwaje na timu ya Taifa ya wanawake hali ya kuwa hakuna ligi yoyote imara inayohusisha jinsia hiyo?


Hata hawa wachezaji wanachaguliwa kwa mtindo gani? Hawa makocha wa Twiga Stars wanazingatia vigezo gani kuwapata mabinti hawa?


Hivi hawa mabinti katika maisha ya soka wanatarajia waje kuishi kwa mtindo gani? Hivi soka kwao ni kujiburudisha au wanahitaji kunufaishwa kwa wao kujiingiza kwenye mpira wa miguu?


Katika kujiuliza maswali yote hayo, utapata jibu kuwa Tanzania haina malengo ya kuendeleza soka la wanawake, hivyo hata kwa hawa vijana waliopo wanaocheza wanajitahidi tu.


Nimejikuta nikianza hivi; baada ya Twiga Stars, kuondoshwa katika mchujo wa kuwania kufuzu michuano ya Kimataifa ya Afrika kwa wanawake (AWC), baada ya kulazimishwa sare ya bao 1-1 nyumbani na timu ya Zambia ‘Shepolopolo’.

Mechi hiyo iliyokuwa na msisimko wa aina yake ilipigwa Ijumaa ya Februari 28, katika Uwanja wa Azam Complex, jijini Dar es Salaam.


Ikumbukwe kuwa, Twiga pia ilishawahi kufungwa bao 2-1 nchini Zambia katika mchezo wa kwanza, hivyo kwa matokeo hayo Twiga Stars itakuwa imeondoshwa kwa ujumla wa bao 3-2.


Ni tofauti ya bao moja tu. Kama hivi ndivyo, hakika vijana hawa wanahitaji pongezi kubwa. Ndio, maana wametumia nguvu kubwa kulitangaza Taifa, ambalo lenyewe haliwatangazi.


Tangu zamani tumekosa utaratibu wa kuijenga Twiga, ili iwe imara ndani na nje ya nchi. Hatuijengi kwasababu hakuna mashindano makubwa kwa ajili yao.


Tumeweka nguvu zaidi kwa soka la wanaume. Akina Mrisho Ngassa, Juma Kaseja, Athuman Idd, Mbwana Samatta, Haruna Chanongo na wengineo wanaogelea katika pesa, vipi hawa wenzao.


Vipi hawa akina Shelida Boniface, Fatuma Mustafa, Sofia Mwasikili, Asha Rashid, Fatuma Omary, Amina Ali na wenzao nini faida ya soka lao?


Hawa utagundua wanatumia nguvu kubwa bila kujua nini hatima ya maisha yao. Ni kama vile wanaua mende kwa nyundo.


Wanavuja jasho bila mpango. Ni kutokana na hilo, nadiriki kusema kwa kufungwa kwa idadi ndogo ya mabao na Zambia, hakika wamejitahidi.


Shirikisho la Soka nchini (TFF), wanapaswa kubuni mbinu nzuri kwa ajili ya soka la wanawake. Liweke mikakati sit u ya kuwa na ligi ya kutoa wanawake wa kuichezea timu za Taifa, ila ile itakayowapatia mwangaza wa kimaisha wasichana kwa kupitia mpira wa miguu.


Tuone akina Mwasikili wanaishi vizuri hata kabla ya kukaa kambini kwa siku tatu kwenye michuano ya Kimataifa, maana si njia nzuri.

Kuwa na ligi bora, itakayoshirikisha timu mbalimbali za Tanzania, kutaongeza mvuto na hamasa kwa mabinti wengi, hivyo kuwapatia nafasi nzuri ya kutafuta maisha ya soka nje ya Tanzania.


Hakuna haja ya kusubiri mechi za Kimataifa ndio wanaitwa mabinti wachache, tena bila utaratibu mzuri wa kuwapata, maana hakuna mashindano.


Hivi kweli unawezaje kuwa na timu ya Taifa, hali ya kuwa hakuna ligi wala mashindano makubwa. Wachezaji wachache waliojulikana kamwe, haiwezi kuwa mbeleko ya kuwavutia mabinti waliozagaa kona mbalimbali za nchi yetu, maana hawajui faida watakayoipata.


Ndio maana nasema, huu ni wakati wa TFF kulifanyia kazi jambo hili, maana kinyume cha hapo soka la wanawake haliwezi kusonga mbele. Haliwezi kuwa ajira kwa watoto wa kike, hivyo itakuwa sawa pia kwa wazazi kuwagomea mabinti wao kushiriki mchezo huo, ukizingatia kuwa miaka nenda rudi hauna faida kwao.


Hauwezi kuvuna bila kupanda. Tupande sasa kwa kuweka mifumo imara ya soka la wanawake. Tuweke mikakati ya kuvutia wadau na hatimae kuwa na ligi nzuri, jambo linaloweza kuzalisha Stars imara.

Mungu ibariki Tanzania.


+255712053949

No comments:

Post a Comment