Pages

Pages

Saturday, February 08, 2014

Vigogo wilayani Handeni wafikishwa mahakamani kwa ufisadi wa Milioni 600



Na Mwandishi Wetu, Handeni.
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) wilayani Handeni mkoani Tanga,imewapandisha kizimbani watumishi 12 wa halmashuri hiyo wakiwatuhumu kutumia nyaraka mbalimbali ambazo ni hati za malipo (payment voucher) na kujipatia fedha isivyo halali. Watumishi waliofikishwa mahakamani ni aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo Mpangalukela Tatala, Erasto Vicent ambaye alikuwa injinia wa maji, 

Mkurugenzi wa kampuni iliyokuwa ikifanya utafiti wa kutafuta maji Beda Joseph, Julius Mhando ofisa maendeleo ya jamii, Ofisa Afya wa wilaya Benson Bundala na Maajabu Kambi aliyekuwa mhasibu wa halmashauri hiyo. 

Wengine ni fundi bomba Shabani Mfundo na Ahmad Buraa, Raphael Nkoba aliyekuwa ofisa Afya na sasa ni ofisa afya halmashauri ya mji Handeni, Michael Mosha mkaguzi wa ndani, Hemed Kandarua aliyekuwa dereva na Violeth Swai ambaye ni ofisa elimu sayansi Kimu. 

Akiwasomea mashitaka hayo Mwendedsha Mashitaka wa Takukuru Samwel Gabriel akisaidiwa na Sweetbert Rwegasira mbele ya hakimu mkazi mfawidhi wa mahakama ya wilaya Handeni Patrick Maligana, alisema kuwa katika mwaka 2005 hadi 2007 kwa nyakati tofauti watumishi hao walitumia hati za malipo,(payment voucher) na kujijazia na kumdanganya mwajiri wao kuwalipa pesa kwa ajili ya kazi mbalimbali wakati kazi hizo hazikufanyika kama walivyoomba.

Mwendesha mashitaka huyo alisema kuwa kutokana na kitendo hicho watuhumiwa hao waliisababishia serikali hasara ya Sh. 654,944,492.37 kwa kutumia hati za malipo ya uwongo wakiwa na lengo la kumdanganya mwajiri wao.
“Mheshimiwa hakimu kutokana na kitendo hicho watuhumiwa hawa waliisababishia serikali hasara ya Sh. 654,944,492.37 kwa kutumia hati za malipo ya uwongo wakiwa na lengo la kumdanganya mwajiri wao ambapo pesa hizo ni miongoni mwa fedha ambazo zilitolewa na benki ya Dunia kwa ajili ya kufadhili mradi wa kuchimba visima virefu wilaya Handeni,” alisema.

Baada ya watuhumiwa hao kusomewa makosa mbalimbali 49 na la 50 la jumla la kuchukua fedha za safari zikiwa hewa, mwanasheria huyo alisema dhamana ipo wazi na masharti ya dhamana lazima yazingatiwe chini ya kifungu cha 148 (5) cha sheria ya uhujumu uchumi chenye mashariti ya kuwa mtuhumiwa anatakiwa kutoa kiasi sawa na thamani ya mali ya kesi inayomkabili, hivyo kutakiwa watoe milioni 54 kila mmoja. 

Alisema kila mshitakiwa anatakiwa kulipa nusu ya mali anayotuhumiwa nayo ikiwa ni kuanzia shilingi milioni 10 atatakiwa kulipa nusu yake hivyo washitakiwa hao kwa kuwa wanadaiwa kiaisi cha shilingi milioni 600 walitakiwa kila mmoja kulipa shilingi milioni 54 papo hapo na mdhamini pia anatakiwa kutoa fedha hiyo. 

Baada ya wanasheria hao kuwasilisha maombi hayo, hakimu Maligana, alisema kwamba kutokana na vifungu vya sheria ya dhamana vilivyotolewa na takukuru inambidi kuchukua siku saba kusoma sheria hiyo kabla ya kutolea uwamuzi wake, hivyo watumiwa hao walirejeshwa rumande hadi 13 mwezi huu. 

Washitakiwa wote walikana mashitaka lakini walirudishwa tena rumande kutokana na hakimu kuomba muda wa kupitia sheria hiyo na kusema kuwa hawezi kutoa jibu la papo kwa hapo ni lazima afuatilie katika kesi kama hizo kuwa ni maamuzi gani yanachukuliwa.

“Kwanza naomba kuagiza washitakiwa wasiokamatwa wakamatwe haraka,waliohospitali watasomewa mashitaka yao huko huko na mliobaki hapa siwezi kusema mtapata dhamana au hapana kwani nahofia kufanyakazi kiholelaholela ila nipate muda wa kujiridhisha na na vifungu hivi harafu baadae ndio nitoe maamuzi hivyo watuhumiwa wote watarudi rumande hadi tarehe 13 mwezi huu,”alisema Maligana. 

Watuhumiwa kadhaa walijitetea kuwa wanamatatizo hivyo wanaomba kusaidiwa kupata dhamani lakini hakimu alisema kuwa haiwezekani kutokana na vifungu vilivyotajwa vinambana kutoa ruhusa hiyo. waliofikishwa mahakamani walikuwa tisa kutokana na kwamba Mosha amelazwa katika hospitali ya wilaya baada ya juzi kukamatwa kisha kupata mshituko uliosababisha alazwe hospitali, huku Tatala ametolwa taarifa kwamba amelazwa Muhimbili na Lyimo hajapatikana na anatafutwa huku hakimu akisisitiza watu hao watafutwe.

No comments:

Post a Comment