Pages

Pages

Tuesday, February 04, 2014

SIWEZI KUVUMILIA: Kumpigia magoti Manji ni kuonyesha udhaifu

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
MIMI ni miongoni mwa watu walioshangaa mno, pale wanachama wa Yanga, walipompigia magoti Mwenyekiti wao Yusuph Manji ili agombee tena nafasi yake baadaye mwaka huu.
Mwenyekiti wa Yanga, Yusuf Manji, pichani.
Nilipowaona nilishangaa. Walionyesha udhaifu mkubwa katika sekta ya mpira wa miguu nchini. Manji ni mfanyabiashara mwenye mapenzi na klabu hiyo tangu zamani. Hilo linajulikana. Hivyo hata kutangaza kwake kutowania nafasi hiyo ni uungwana mkubwa.

Kutangaza kutowania nafasi hiyo, ni kuwataka wanachama wengine wenye mapenzi na Yanga wajiandaye kuiwinda nafasi hiyo katika Uchaguzi Mkuu wa klabu hiyo utakaofanyika Juni mwaka huu na kurithi mikoba yake.

Mengi yanasemwa wakati huu. Wapo wanaosema uamuzi wa Manji umetokana na kuchoka mwenendo mbaya wa wanachama wake wa kuishi kwa kubangaiza kutoka kwake.

Wengine wanasema kuwa uamuzi wake umetokana na kushindwa kuisaidia Yanga kama alivyotangaza hapo awali.

Inawezekana ni kati ya sababu nilizotaja zimemfanya Manji asite kuendelea kuwa mwenyekiti wa Yanga, ila mwisho wa siku lazima tujuwe Yanga ina wanachama wengi.

Sio Manji tu, mtu yoyote anaweza kuwania nafasi hiyo, hivyo kinachotakiwa ni mapenzi, moyo wa uthubutu na malengo ya kuisaidia klabu ya Yanga.
Hakika siwezi Kuvumilia. Hii ni baada ya kuona wanachama wa Yanga wanajidanganya kuwa Manji atakuwa mwenyekiti wa milele. Hii sio kweli hata kidogo na lazima wadau hawa wapingwe.
Wanaojidanganya kuwa Manji anafaa kuwa mwenyekiti miaka yote, hawajui wajibu wao. Kwanini sasa wampigie magoti? Asipokuwapo Manji, Yanga haitakuwapo?

Wanampigia magoti hata pale alipotangaza kusimama kwa ajili ya kuwaachia wengine waongoze na yeye kufanya biashara zake? Hapo ndipo unaposhangaa Yanga.

Yanga ni kati ya timu zenye wanachama na wapenzi wengi. Wana kila sababu ya kuwa timu tajiri kama watakuwa na moyo wa uzalendo na mbinu nzuri za kuendesha kibiashara.

Mtaji wa wanachama wanao. Sasa kwanini washindwe kujua wajibu wao? Kwani Manji ndio nani? Hakika siwezi kuvumilia na jambo hili linashangaza Dunia.

Hata yeye huenda anawacheka Yanga. Anajiuliza, hawa wanaonipigia magoti wana mawazo sahihi? Baada ya kuwaza na kujiuliza, atapata jibu kuwa wanampigia magoti ili maisha yao yaendelee.

Wanajua watavuna chochote kitu, ukizingatia kuwa ndio hao hao wanaopitisha hoja za migogoro klabuni hapo ili wapate visenti vya kula wao na familia zao.

Hakika siwezi kuvumilia. Ni wazi Yanga na klabu zote zinastahili kujiendesha kwa mipango kwa kutumia rasilimali watu na rasilimali fedha na kuacha kuwa tegemezi miaka nenda rudi.

Baada ya kusema hili, naamini huu ni wakati wa wanachama wa Yanga kujiandaa kumpongeza Manji kwa uzalendo wake na nia yake ya kupisha wengine waongoze itakapofika Juni mwaka huu katika Uchaguzi Mkuu wa klabu hiyo.

Na wale wanaona kuwa Manji amefanya makosa sana kupisha wengine basi wajuwe wao ni wadhaifu na vitendo vyao hivyo vinaweza kufifisha maendeleo, wakidhani hoja zao zinaweza kuwa na mashiko, wakati zimekuja maalum kuneemesha matumbo yao.
+255 712053949

No comments:

Post a Comment