Pages

Pages

Sunday, February 09, 2014

Mb Dogg atabiriwa makubwa kwenye anga ya muziki wa Bongo Fleva


Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam

MKURUGENZI wa Kampuni ya Qs Entertainment, Joseph Mhonda, amemtabiria makubwa msanii wa muziki wa kizazi kipya aliyepata kutamba miaka kadhaa iliyopita, Mbwana Mohammed maarufu kama Mb Doggy, pichani chini.

Mb Doggy aliyewahi kutamba na nyimbo mbalimbali, ukiwamo Latifa, Si Uliniambia na nyinginezo, alishuka kiwango kidogo, jambo linalomfanya sasa apiganie mafanikio ili arudi tena kileleni.


Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Mhonda alisema kuwa Mb Dogg ni miongoni mwa wasanii wa kizazi kipya wanaoweza kukaa chini na kuandika mashairi mazuri, hivyo kurudi kileleni ni jambo rahisi kwake.


Alisema anaamini wakati wowote ukifika ataanza kuwika tena katika vituo vya redio na televisheni kwa kuachia nyimbo kali zenye kugusa kila mtu.


“Kwa msanii kama Mb Doggy anayeweza kuandika mashairi wakati wowote na kugusa hisia za wengi kurejea kileleni ni kitu rahisi mno kwake, hivyo naamini kwa sasa anajua kitu anapaswa kufanya.


“Naamini kila kitu kinafanyika vizuri kwa ajili ya kumuona Mb Doggy aliyezoeleka kwa wadau wa muziki wa kizazi kipya, ingawa soko la Bongo Fleva linazidisha ushindani kila wakati,” alisema.


Qs ndiyo kampuni inayofanya kazi na Mb Dogg na wasanii mbalimbali wa muziki huo, akiwamo Ney wa Mitego anayetamba na wimbo wa Muziki Gani, akimshirikisha msanii Nassib Abdulmalick, Diamond.

No comments:

Post a Comment