Pages

Pages

Saturday, February 08, 2014

John Mnyika atema cheche juu ya majina ya vigogo majangili

Mbunge wa Ubungo ambaye ni mjumbe wa kamati ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, John Mnyika, pichani, ameitaka serikali kuondokana na kigugumizi cha kuwataja kwa majina vigogo wa ujangili.


Akizungumza na Waandishi wa habari, Mnyika alisema kabla ya kuanza kwa Oparesheni Tokomeza sehemu ya pili ni ambayo inatajwa kuanza muda wowote kuanzia sasa, ni busara serikali ikaweka wazi majina ya vigogo wanaohusika na biashara hiyo ambao wanatajwa kuwa ni watendaji wa serikali.


Alisema ni dhahiri kwamba serikali inawafahamu vigogo wa ujangili ambao wanadaiwa kuwa ni watendaji wa serikali na viongozi wakubwa katika ngazi za vyama vya siasa na watendaji wa serikali na kwa maana hiyo Opereseheni Tokomeza awamu ya pili haitakuwa na jipya endapo majina ya wahusika hao hayatawekwa hadharani.

Alisema katika Hotuba yake ya kufunga mwaka mwishoni mwaka jana, Rais Kikwete alikaririwa akisema kuwa Operesheni Tokomeza ujangili awamu ya kwanza ilifanikiwa kufichua mitandao ya ujangili ambao wengine ni watendaji wa serikali, hivyo hakuna sababu ya kuendelea kuweka katika mabano majina yao.


“Ujangili umekithiri, kwenye hotuba yake ya mwisho wa Mwaka, Rais Kikwete, alieleza kuwa operesheni tokomeza imesaidia kufichua mtandao wa majangili ambao wengine ni watendaji wa serikali, sasa basi kabla ya kuanza kwa awamu ya pili ya operesheni tokomeza, ni vizuri kwanza vigogo ambao wanafahamika kwa majina “majangili” wakatajwa majina wazi na kuchukuliwa hatua,” alisema Mnyika.


Mnyika aliongeza kuwa ili matatizo na mapungufu yaliyojitokeza katika awamu ya kwanza yasijirudie tena, kuna haja ya kutajwa kwa majina ya wahusike ili washugulikiwe wao pekee na mitandao yao badala ya kuwalenga wananchi wasiokuwa na hatia.


Aidha Mnyika ambaye pia ndiye mkurugenzi wa habari na mawasiliano wa chama cha demokrasia na maendeleo (CHADEMA), alishauri serikali ya Tanzania kuiga mfano wa nchi nyingine kwa kupiga marufuku kwa muda zoezi la uwindaji wa Tembo na Faru katika vitalu kwani kuna watu wanaotumia uwindaji huo kuchangya uwindaji haramu na halali.


“Ili kuepusha wananchi wa kawaida kulengwa katika operesheni hii, kuna haja ya majangili vigogo majina yao kuwekwa hadharani, kama serikali itaendelea kuona kazi kutaja majina haya sidhani kama operesheni tokomeza awamu ya pili itakuwa na tija zaidi ya manyanyaso na mateso ya raia wasiokuwa na hatia,” alisema.


Kuhusu suala la mapato yanayopatikana katika maeneo ya hifadhi za taifa pamoja na kodi inayotozwa miradi inayotekelezwa na mashirika, mnyika alisema ni jambo la aibu kutoza kodi miradi ambayo inatekelezwa na mashirika ya umma, miradi ya kusaidia jamii inayozunguka maeneo ya mashirika, kama kwa hapa Tanapa na maeneo yanayozunguka hifadhi ya Tarangire.


Alisema ni busara serikali isiongeze mzigo wa kodi ilikuwezesha kiwango kidogo cha fedha kinachotoka kiweze kufikia miradi mingine zaidi kwa kuongeza kuwa serikali haitendi haki kwa mashirika hayo kwani  miradi hiyo inalenga kufanya kazi ambayo kimsingi ilikuwa ifanywe na serikali, kimsingi ilikuwa ifanywe na wananchi.


“Maeneo ambayo yanazungukwa na hifadhi kama vile maeneo yanayozungukwa na migodi, wananchi wanatarajia kwamba kiwango cha mapato kinachotokana na mazingira yao kirudi kwenye jamii, kwa hiyo ukiondoa miradi ya kusaidia kama hii ya ujenzi ya madarasa kuna haja ya kwenye mapato yanayotokana na vivutio vya utalii kuwa na mgao wa moja kwa moja kwenye Halmashauri na kuziwezesha kuwa na bajeti kubwa”, alisema Mnyika.


Akitolea mfano Hifadhi ya Tarangire ambayo kwa mwaka wa fedha wa 2013/2014, ilikusanya bilioni 9.7, sasa ukiangalia bajeti ya miradi ya jamii, ambayo ni 193 milioni pekee haifiki hata asilimia 2.5 ya mapato ambayo yamepatikana kwa hiyo ni lazima kuwa na mfumo ambao mapato makubwa zaidi zitaongezeka kama kodi ya huduma ya kijamii, kodi ya makampuni kwa sababu makampuni nazo zinatengeneza faida kubwa.

No comments:

Post a Comment