Pages

Pages

Thursday, February 06, 2014

Mangu afanya mabadiliko Jeshi la Polisi kwa Makamanda wake

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
MKUU wa Jeshi la Polisi Tanzania, Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) Ernest Mangu pichani, ameanza kufanya mabadiliko ya baadhi ya makamanda wa mikoa, wakuu wa upelelezi wa mikoa, wakuu wa usalama barabarani wa mikoa pamoja na watendaji wengine wa vikosi na vitengo mbalimbali ndani ya Jeshi hilo. 
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Msemaji wa Jeshi la Polisi, Advera Senso-SSP; miongoni mwa makamanda wa mikoa waliofanyiwa mabadiliko ni pamoja na aliyekuwa Kamanda wa Mkoa wa Ruvuma Kamishna msaidizi mwandamizi (SACP) Deusdedit Nsimeki anayekwenda kuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara, aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara Kamishna msaidizi (ACP) Akili Mpwapwa sasa anakuwa Kamanda wa Polisi Ruvuma. Taarifa hiyo imeeleza aliyekuwa Ofisa Mnadhimu Mkoa wa Lindi, Kamishna Msaidizi (ACP) Renatha Mzinga anakuwa Kamanda wa Mkoa wa Lindi, aliyekuwa Ofisa Mnadhimu Mkoa wa Dodoma Kamishna Msaidizi (ACP) Suzan Kaganda amehamishwa kuwa Kamanda Mkoa wa Tabora huku aliyekuwa Kamanda wa Polisi Tabora (ACP), Peter Ouma amehamishiwa Polisi Makao Makuu. 
Wengine ni pamoja na aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Mtwara, (ACP) Eliyakimu Masenga anakwenda kuwa Mkuu wa Upelelezi Kikosi cha Tazara, Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Tabora (ACP) David Mnyambuga anakwenda kuwa Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Ilala, na aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Ilala, (ACP) Juma Bwire, anakwenda kuwa Ofisa Mnadhimu Mkoa wa Tabora. Aidha, aliyekuwa Ofisa Mnadhimu Mkoa wa Tabora Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP) John Kauga anakuwa Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Tabora, aliyekuwa Mkuu wa Polisi Wilaya ya Rombo (SSP) Mrakibu Mwandamizi, Ralph Meela anakwenda kuwa Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Mtwara na aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi Kikosi cha Tazara, Mrakibu wa Polisi (SP) Isack Msengi anakuwa Kaimu Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Pwani.
Katika mabadiliko ya wakuu wa Polisi wa mikoa Usalama Barabarani; aliyekuwa Mkuu wa Trafiki Mkoa wa Kinondoni (SSP), Ibrahim Mwamakula amehamishiwa Trafiki Kanda Maalum Dar es Salaam, Mkuu wa Polisi wa wilaya ya Mtwara (SP), Awadh Haji anakwenda kuwa Mkuu wa Trafiki Mkoa wa Kinondoni, na (SP), Ezekiel Kiko Mgeni aliyekuwa Ofisi ya RPC Temeke, anakuwa Mkuu wa Trafiki Mkoa wa Temeke. 
Wengine ni aliyekuwa Mkuu wa Trafiki Mkoa wa Lindi Mrakibu wa Polisi (SP) James Kiteleki anakwenda kuwa Mkuu wa Trafiki Mkoa wa Njombe, aliyekuwa Mkuu wa Trafiki Mkoa wa Ilala, Mrakibu wa Polisi (SP) Meloe Buzema anakwenda kuwa Mkuu wa Trafiki Mkoa wa Lindi, aliyekuwa Kaimu Mkuu wa Trafiki Mkoa wa Temeke Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP) Prackson Kibogoyo anakwenda kuwa Mkuu wa Operesheni Mkoa wa Pwani, na aliyekuwa Mkuu wa Trafiki Mkoa wa Njombe, Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP) Chacha Nsaho Maro anakwenda kuwa Mkuu wa Trafiki Mkoa wa Ilala. Hata hivyo taarifa hiyo imefafanua kuwa mabadiliko hayo ni ya kawaida kwa mujibu wa kanuni, taratibu na miongozo ya Jeshi la Polisi katika kuhakikisha kwamba wananchi wanaendelea kupata huduma bora ya usalama.

No comments:

Post a Comment