Pages

Pages

Friday, February 07, 2014

Makamu wa Rais akutana na balozi wa Oman

Makamu wa Rais Dkt. Mohammed Gharib Bilal leo amempokea Balozi mpya wa Oman nchini Tanzania Balozi Soud Ali Mohamed Al Ruqaishi ofisini kwake Ikulu Jijini Dar es Salaam na kisha kufanya naye mazungumzo. Katika mazungumzo hayo, Mheshimiwa Makamu wa Rais amemhakikishia Balozi Ruqaishi kuwa Tanzania na Oman zina uhusiano wa kindugu wa siku nyingi na kwamba uhusiano huo umekuwa ukinufaisha nchi hizi kwa miaka kadhaa. 

Mheshimiwa Makamu wa Rais aliendelea kufafanua kuwa, Tanzania kwa sasa inashirikiana na Oman kiuchumi na kwamba kuna wawekezaji wengi kutoka Oman ambao wako nchini, sambamba na wengine wanaoonesha nia ya kuwekeza katika sekta mbalimbali hapa Tanzania.


Kwa upande wake Balozi Ruqaishi alimueleza Mheshimiwa Makamu wa Rais kuwa, Oman inafurahia uhusiano wake na Tanzania na kwamba jukumu lake la kwanza ni kuhakikisha kuwa uhusiano huo unadumu na kunufaisha nchi hizi mbili. Pili alifafanua kuwa, atahakikisha katika kipindi chake cha Ubalozi hapa Tanzania anasaidia kutanua fursa za uwekezaji kwa wawekezaji kutoka Oman sambamba na kuwafungulia fursa kama hizo wawekezaji walio na nia ya kuwekeza nchini Tanzania. 

Oman licha ya kuwa na uhusiano wa karibu na Tanzania na hasa Visiwani Zanzibar, inabakia kuwa ndiyo nchi pekee duniani nje ya Afrika iliyo na wazungumzaji wengi wa lugha ya Kiswahili. Katika siku za hivi karibuni, wawekezaji kutoka Oman wameonesha nia ya kuwekeza katika sekta ya Mafuta na Gesi sambamba na kuliimarisha shirika la Ndege Tanzania ili limudu ushindani na kuongeza ufanisi wa shughuli zake katika biashara ya safari za anga.

No comments:

Post a Comment