Pages

Pages

Wednesday, February 05, 2014

TANESCO inavyopewa rungu kuwapiga walalahoi wa Tanzania wasiojua siku yao inaanzaje na kuishaje

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
NI mateso makubwa. Wananchi wenye kipato cha chini wanaendelea kulia na kusaga meno kutokana na maisha yao kuwa magumu. Kila siku, mahitaji yenye umuhimu kwao yanaongezeka na gharama zake zikiongezeka pia.
Waziri wa Nishati na Madini, Sospeter Muhongo pichani.
 Mtanzania wa leo hana matumaini yoyote. Wale aliowaamini kwa kiasi kikubwa wamemuangusha. Suala hili linahitaji mjadala mpana mno. Mjadala huu utajaribu kuweka mazingira mazuri kwa wananchi wote.

Hii ni kwasababu hakuna tumaini jipya kwa Mtanzania, hata wakiangalia ile hoja ya Maisha bora kwa kila mtanzania, wimbo ulioimbwa na watawala wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), chini ya Rais Jakaya Mrisho Kikwete katika nyakati tofauti, wakati anawania kiti cha urais.
Miundo mbinu ya umeme kama inavyoonekana pichani.
Nimejikuta nikiangalia mtiririko wa matukio mbalimbali kwa Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania TANESCO. Shirika hili kila siku limekuwa likitafuta mbinu ya kupandisha bei ya umeme hapa nchini.
Pamoja na kupandisha bei hiyo, bado shirika hilo limeshindwa kujiendesha. Kila mahali ni malalamiko kutoka kwa walaji, ambao ni wananchi wenyewe. Ingawa bei hizi hubarikiwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), kabla ya kupandishwa, ila wote hao wanaonekana hawana machungu na Watanzania.
Angalia, katika kikao chake cha Desemba 10 mwaka 2013, kilikubaliana kupandisha ongezeko la bei za umeme kwa viwango mbalimbali kwa makundi ya wateja, ikiwa ni dalili za kuongeza mzigo kwa wananchi.
Mbaya zaidi, uthubutu wa kupandisha bei hizo hudaiwa kuwa Shirika la TANESCO linakabiliwa na mzigo mzito wa madeni. Hawana uwezo wa kujiendesha. Sawa, ila madeni hayo yamepatikana vipi?
TANESCO kwa kushirikiana na serikali chini ya Wizara ya Nishati na Madini imeangalia ongezeko hili ni halali kwa wananchi wao? Ikiwa tunapigia kelele vijijini kupelekwa huduma ya umeme, wananchi hao wataziweza gharama hizi?
Nchi hii imeoza. Bado siku chache sana tutashuhudia majuto makubwa ndani na nje ya mfumo wa Taifa letu. Sioni mwenye machungu na walalahoi. Kwanini nasema hivi; siku zote zinapopandishwa gharama zozote, wanaoathirika zaidi ni wananchi, tena wale wenye kipato cha chini.
Hatua hii ni mbaya isiyojali utu wa watu na thamani yao, huku ikitarajiwa kuongeza gharama za maisha kwa wananchi. Pia itaathiri uchumi wa nchi yetu. Nchi inayojiendesha kwa kuangalia matukio.
Mara baada ya kuanza mwaka mpya, Watanzania waliingia kwenye bei mpya ambazo TANESCO iliziomba kutoka EWURA mwishoni mwa mwaka jana. Wakafanikiwa kupandisha bei hizo hata kama wamejua ugumu wa maisha na jinsi Watanzania wanavyoishi kwa kubahatisha.
Awali kundi hili lilikuwa linatunia wastani wa matumizi ya uniti 50 kwa mwezi, ambapo bei mpya sasa ni sh 100 kwa uniti moja, kutoka shilingi 60 za sasa, sawa na ongezeko la shilingi 40.
Kundi T1 linalohusisha watumiaji wakubwa wa umeme majumbani, biashara ndogondogo, mashine za kukoboa na kusaga nafaka, taa za barabarani, mabango n.k wameguswa kwa bei ya Sh 306 kwa uniti moja, ikiwa ni ongezeko la Sh 85 ya bei ya sasa, ambapo pia TANESCO ilipendekeza ongezeko la Sh 131.
Mtiririko huo unalitaja kundi T2 lenye watumiaji wa umeme wa kawaida unaopimwa kwa msongo wa volti 400, ambao matumizi yao ya wastani kwa mwezi ni zaidi ya uniti 7,500, huku wateja wao wakiwa ni wafanyabiashara wakubwa na viwanda vya kati, ambapo bei yao itakuwa Sh 205 kwa uniti moja, sawa na ongezeko la Sh 73.
Nchi hii mtu akitaka kumkomoa mwenzake anakaa na kuja na mapendekezo ambayo hadi mwisho wake hakuna wa kukataa. Ndio maana TANESCO iliwasilisha maombi yao EWURA, ikiomba kuanzia Oktoba 11 Oktoba 2013 kuwe na mabadiliko ya bei kwa asilimia 67.87, asilimia 12.74 kuanzia tarehe 1 Januari 2014 na asilimia 9.17 kuanzia Januari 1 mwaka 2015.
Ili kupangilia ombi lao, TANESCO waliomba tena kuidhinishwa kwa kanuni ya kurekebisha bei ya umeme kulingana na mabadiliko ya bei za mafuta, mfumuko wa bei na mabadiliko ya thamani ya shilingi ya kitanzania. Kwa kipengele hichi tu, kinaonyesha namna gain shirika hili lisilokuwa na mipango linavyojipanga kuwahadaa na kuwalangua Watanzania masikini.
Ni kauli chungu kwa Watanzania. Kama mtu anakosa hata hela ya kununulia sukari, atawezaje kuununua umeme kwa bei kubwa? Na mbaya zaidi, gharama hizo haziendi sambamba na huduma bora.
Umeme wa Tanzania unakatika bila mpango. Wateja wao wanapata hasara kwa kuunguliwa na vifaa vyao. Mteja akipata tatizo lolote hajui wapi aende kudai fidia. Huu ni mpangilio ovu kwao.
Endapo kungekuwa na shirika lingine la kutoa huduma hiyo, TANESCO wangefahamu namna gain wamechokwa na hakuna Mtanzania anayeheshimu walau robo tu ya huduma zao mbovu na zinazoangalia maslahi zaidi.
Unaweza kuangalia ujinga huu na kubaini ni Tanzania tu. Nchi za wengine wangeshaingia barabarani. Wangeandamana, maana wanacholipia hakilingani na huduma wanayoipata. Viwanda vitakuwa vimepata mahali kwa kupandisha bei ya bidhaa zao, maana serikali yao imebariki unyonyaji huu.
Kwani kundi T3-MV linalohusisha wateja wakubwa wa viwanda vikubwa waliounganishwa katika msongo wa kati (Medium Voltage) bei yao ni Sh 166 kwa uniti moja, sawa na ongezeko la Sh 45, wakati kundi T3-HV linalohusisha wateja wakubwa waliounganishwa katika msongo wa juu (High Voltage – Voti 66,000 na zaidi) ikiwa ni pamoja na ZECO, Bulyanhulu, na Twiga Cement wao watalipia Sh 159 kwa uniti moja, sawa na ongezeko la shilingi 53 la bei ya sasa, wakati TANESCO katika mapendekezo yao walitaka walipe Sh 80 kwa uniti moja.
Ila woga wa Watanzania unatokana na heshima ya Taifa lao. Pia wengine wanaogopa kauli za vitisho kutoka kwa viongozi wa juu. Huu si utawala bora. Hakuna utawala bora usioangalia thamani ya mtu.
CCM inayoamini inaweza kuongoza milele, inafanikisha vipi maisha bora? Je, dhuluma hizi wanaziangalia vipi? Je, TANESCO ikishindwa tena kujiendesha ingawa wamepandisha bei zao wataongeza tena?
Hii si sawa. Naanza kumuelewa Mfanyabiashara Reginald Mengi, katika malalamiko yake dhidi ya Waziri wa Nishati na Madini, Sospeter Muhongo. Mengi alimwambia waziwazi kuwa waziri huyo ni mwongo.
Akaona haitoshi, akamwambia tena ni wakati wake kukaa chini na kuangalia namna ya utendaji wake hasa juu ya umeme wa Tanzania, ambao wengi hawaupati na wanaopata wanaulipia kwa gharama kubwa. Kwa jinsi hali inavyokwenda, kila mmoja atajua nani mkweli kati ya Mengi na Muhongo.
Ukimuuliza mtendaji wa TANESCO na viongozi wao kuwa wanajivunia nini juu ya masuala ya nishati hapa Tanzania utabaki unacheka. Watakwambia wamepeleka umeme vijiji vingi. Pia watasema kuwa wamepunguza bei ya nguzo za umeme na vifaa vingine vilivyokuwa vinauzwa bei ghari.
TANESCO na Wizara yao inajifariji kuwa imepunguza gharama za kuunganisha umeme vijijini kwa asilimia 33 hadi 77. Kwa mujibu wa wizara hiyo, kwa wateja wanaopenda kuunganishiwa umeme kwa kujengewa njia moja na kuwekewa nguzo mbili watalazimika kulipa Sh 454,654, huku maeneo ya mjini wakitakiwa kulipa Sh 696,640 badala ya 2,001,422 zinazolipiwa kwa wateja hao sasa.
Punguzo hilo ni sawa na asilimia 77.28, wakati kwa wateja watakaowekewa njia moja na kufungiwa nguzo moja kwa maeneo ya vijijini watalazimika kulipia Sh 337,740 na wanaoishi mjini watalipia Sh 515,618 badala ya Sh 1,351,884 zilizokuwa zinalipwa hapo awali, sawa na asilimia 75 kwa wanaoishi vijijini na asilimia 61.86 kwa wateja wanaoishi mjini juu ya punguzo hilo.
TANESCO, EWURA na Wizara yao inachanganya mambo. Na sisi wengine tukisema, tutaambiwa tuache porojo juu ya mambo hayo ya kitaalamu. Inashangaza. Ukiangalia gharama hizo za kufungiwa umeme kushushwa na sasa jinsi ya kuununua kwa bei juu unajiuliza unafuu upo wapi?
Mbaya zaidi gharama hizo zimeshindwa kuwatambua matajiri na masikini. Wote wanalia. Kama kwenye kushusha waliangalia wanaoishi mjini na vijijini, kwenye manunuzi ya umeme huo hilo limeangaliwa?
Vijiji sasa ni majuto. Watanzania sasa ni mateso bila chuki. Waziri Muhongo alinukuliwa na vyombo vya habari mwaka jana kuwa bei ya umeme haitapanda. Leo ulivyopanda Muhongo anasemaje katika hili?
Au ndio wadau tuache porojo? Najikuta nikiumia zaidi kila ninapoangalia maisha magumu yanavyotawala katika kaya mbalimbali za Watanzania. Kuna baadhi ya wilaya zinazosumbuliwa na shida ya maji.
Shida hii itazidishwa kasi hata kwa vile visima vinavyotumia umeme kuvuta maji kutoka chini ya ardhi. Kama leo wananchi hao wananunua ndoo ya lita 20 kwa Sh 500 hadi 700 leo umeme umepanda bei watauziwa shilingi ngapi?
Katika hili wabunge wetu wanasemaje? Au nao wamebaki kimya kwasababu wakisema wataambiwa waache porojo? Kwamba wao ni wanasiasa? Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inayoongozwa na Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), huku Waziri Kivuli akiwa ni John Mnyika inasemaje.
Nauliza hilo kwasababu katika suala la kodi za simu wabunge, wananchi na mashirika ya haki za binadamu walikuja juu. Walilalamika kupita kiasi. Matokeo yake yalisababisha kodi hizo kusitishwa.
Kwanini suala la umeme linalowagusa watu wengi na linaloweza kupandisha au kushusha uchumi wetu linaachwa kama lilivyo? Lazima tuliangalie hili kwa kina. Ukimya wa viongozi na wananchi hauwezi kutusaidia.
Ukiangalia mpangilio wa bei hizo, utagundua kuwa mwananchi wa kawaida ameguswa kila mahali. Asipotumia umeme nyumbani kwake, basi atashikwa kwenye matumizi mengine ya lazima. Wenyewe wanaona ni gharama ndogo, ila kiukweli hazina manufaa na jambo zuri kwa walalahoi. Angalia, EWURA imeongeza mahitaji ya umeme kufikia uniti 75 kwa wateja wadogo wa majumbani, hasa vijijini, wanaotumia wastani usiozidi wa Uniti 75 kwa mwezi.
Haya ni mambo yanayoshangaza kupita kiasi. Bei hizi zinamhusu Mtanzania mwenye kipato cha kawaida. Kwanza atalazimika kuulipia umeme kwa bei kubwa nyumbani kwake nab ado atabanwa tena kwenye manunuzi ya bidhaa ambazo lazima zitapanda bei kwa kisingizio cha gharama za uzalishaji.

No comments:

Post a Comment