Pages

Pages

Sunday, October 13, 2013

Wachina wamsaidia Kigoda kuchimba visima viwili ili kupunguza tatizo la maji wilayani Handeni

Na Mashaka Mhando,Handeni
MAKALI ya tatizo la maji katika mji wa Chanika wilayani Handeni, yameanza kupungua kufuatia kuchimbwa kwa visima virefu vipatavyo 20 katika mji huo ili kukabiliana na uhaba mkubwa wa maji ambao ulikuwa kero kubwa hasa kwa akina mama wanaoshindwa kufanya kazi kwa ajili ya kutafuta maji.

 Mbunge wa Handeni Dkt Kigoda akiwapa maelezo wafadhili wake waliochimba visima viwili virefu kwa thamani ya shilingi milioni 80, kwamba sasa maji yaliyopo kwenye vioski hivyo vinasaidia wananchi ambao wanachota kwa ndoo moja sh. 50 badala ya hapo awali kununua sh. 500.

Kupungua huko kumebainishwa na mmoja ya akina mama Grace Mwinkalo alipozungumza katika hafla fupi ya Mbunge wa jimbo hilo, Dkt Abdallah Kigoda alipofika kwenye moja ya kioski cha maji kilichoko soko la zamani mjini hapa, kuwaonesha wafadhili mradi wa visima viwili walivyofadhili.
Mbunge wa Handeni na Waziri wa Viwanda, Biashara na masoko Dkt Abdallah Omary Kigoda akisalimia na wananchi wa jimbo lake alipofika kuwaonesha wafadhili wake kisima alichochimba eneo la Chanika Soko la zamani.
 Injinia wa maji wa wilaya Injinia Komba, akimweleza mbunge Dkt Kigoda pamoja na wafadhili wake akiwemo Mwenyekiti wa TCZMR Bw Zhao Daoquan (shoto kwa Kigoda), namna walivyoweza kuchimba eneo hilo na kupata maji ambayo yanatumika kwa sasa na wananchi wa Handeni.

Mama huyo mkazi wa mtaa wa Kwamngumi kata ya Chanika, alisema wanashukuru makali ya ukosefu wa maji yamepungua kwa kiasi kikubwa kufuatia sasa mtaa wao huo na mingine kuwepo kwa visima vilivyochimbwa na mbunge akishirikiana na wafadhili wake kupunguza kero ya maji iliyokuwepo muda mrefu.

"Mheshimiwa mbunge na wageni wako, kwa niaba ya akina mama wa Chanika, tunapenda kushukuru kwako na serikali kwa ujumla kwani sasa makali ya tatizo la maji katika mji wetu yamepungua kwa kiasi kikubwa, tunashukuru endelea kufanya jitihada nyingine ili tuweze kupata maji zaidi," alisema Mwinkalo.
Akizungumza kumweleza Mwenyekiti wa Muungano wa Wazalishaji Madini wa Tanzania na China (TCZMR), Zhao Daoquan, mbunge wa jimbo hilo, alisema msaada wa visima viwili walivyowapa, vimeweza kusaidia kero ya maji iliyopo wilayani humo iliyosababishwa na wilaya hiyo kuwa na mito ya kudumu ikiwemo mabwawa.

Alisema zaidi ya visimwa 20 vimechimbwa katika maeneo mbalimbali ya wilayani humo ambapo sasa wananchi wananunua ndoo moja ya maji sh. 50 badala ya sh. 500 hadi sh. 1,000 walizokuwa wakinunua kipindi cha nyuma hatua ambayo ilikuwa ikisababisha kero na watu wengine kumlaumu yeye ingawa tatizo la maji ni la Kitaifa.

Naye mwenyekiti wa TCZMR ambaye ni raia wa China waliopo hapa nchini kwenye migodo ya Mchuchuma na Liganga hapa nchini, alisema wameanza miradi ya kusaidia maji katika jimbo la Handeni lakini wataendelea kusaidia katika maeneo mengine ya nchi ili kutatua suala la maji linaloikabili maeneo mengi.

Mkurugenzi wa halmashauri ya mji wa Handeni Thomas Mzinga alisema visima vilivyofadhiliwa na mwenyekiti huyo, vitaweza kusaidia watu wapatao 5,000 ambao kutokana na kuwepo vioski hivyo vinavyozalisha maji lita 18,500 kwa siku na kuwafikia watu zaidi ya asilimia 40 ya wakazi wote wa Chanika wapatao 9,000.

Mkurugenzi huyo alisema kioski kilichokuwa sokoni ambacho kinahudumia masaa 24 kimekuwa kikiingiza kiasi cha sh. 20,700 kwa siku sawa na sh. 600,000 kwa mwezi hatua ambayo zinatosha kufanya ukarabati mdogo pindi uchakavu unapotokea ili kuboresha huduma hiyo.

No comments:

Post a Comment