Pages

Pages

Sunday, October 13, 2013

Mbunge aishauri serikali kuangalia vibali vya walimu Jumuiya ya Afrika Mashariki

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
MBUNGE wa Bukoba vijijini, Jasson Rweikiza, ameitaka serikali kuangalia upya utaratibu wa utoaji vibali kwa walimu kutoka Jumuia ya Afrika Mashariki.

Rweikiza alitoa ombi hilo juzi, kwenye mahafal ya tatu ya kidato cha nne, shule ya sekondari Brilliant, iliyopo Mbezi kwa Msuguri jijini Dar es Salaam, ambapo mgeni rasmi alikuwa ni mbunge wa Sengerema, William Ngeleja.

Alisema Tanzania ina upungufu wa walimu zaidi ya 130,000, lakini shule binafsi haziwezi kuagiza kutokana na urasimu na gharama kubwa za kibali cha kazi.

"Nchi ina uhaba wa walimu, lakini wenzetu Kenya na Uganda wana idadi kubwa ya walimu kuliko mahitaji, sasa unapoagiza mwalimu kutoka nchi hizo, kuna urasimu mkubwa wa kupata kibali, na kikitoka hiyo gharama yake, utajuta," aliongeza Rweikiza ambaye ni mmiliki wa shule hiyo.

Alisema pamoja na mambo mengi kuchangia matokeo mabaya kwa wanafunzi, lakini ukosefu wa walimu ni sababu kubwa zaidi inayochangia matokeo hayo mabovu.
Aliitaka serikali kuruhusu walimu kutoka nchi hizo kuja kufundisha na nchi itakapojitosheleza basi waondoke.

Naye mbunge wa Karagwe, Gosbert Blandes ambaye alikuwa ameambatana na Ngeleja, alisema watalipigia kelele suala hilo pindi wakifika bungeni.

"Wenye mapenzi mema na taifa, tusukume jambo hili lifanikiwe ili kunusuru elimu,"alisema.
Ngeleja akijibu hoja hizo kwa majumuisho alisema watapigia debe uingiliano huru wa kazi kwa nchi za Afrika Mashariki

Aliahidi kutoa mifuko 100 ya saruji kwa ajili ya kumpa nguvu Rweikiza katika kukamilisha ujenzi wa shule, kwani uwekezaji kwenye elimu haumsaidii yeye na familia yake tu bali taifa zima.

Ngeleja aliahidi pia kwenda kuzungumza na Waziri wa Ujenzi, ili kushughulikia tatizo la ubovu wa barabara zinazoingia shuleni hapo na nyingine zaidi ya sita zinazozunguka eneo hilo.

No comments:

Post a Comment