Pages

Pages

Saturday, September 28, 2013

SIWEZI KUVUMILIA: Yanga ijiandae kushindwa na kushinda



Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
KATIKA mchezo wa soka, suala la kushinda, kutoka sare na kushindwa ni jambo la kawaida, hivyo klabu za soka Tanzania, ikiwamo Yanga, Simba lazima zijiandae kwa matokeo hayo.
Mwenyekiti wa Yanga, Yusuf Manji, pichani.
Si ajabu timu kufungwa au kushinda. Lolote linaweza kutokea maana ni jambo la kawaida kwenye mchezo wa soka. Wakati nasema haya, nagundua jinsi baadhi ya timu zinaposhindwa kukubali matokeo ya kufungwa au kutoka sare ndani ya uwanja.
Huwa naumia kichwa ninapoona timu moja inashindwa kukubali matokeo ya kufungwa au kutoka sare. Siku zote wanataka washinde. Inapofungwa au kupata sare inalalamika mno.
Hili si jambo jema. Na ndio maana siwezi kuvumilia, hasa kwa kuanza kusikia malalamiko kutoka kwa baadhi ya mashabiki wa soka Tanzania, hasa wale wa Yanga.
Mara baada ya kupata sare ya bao 1-1 dhidi ya timu ya Mbeya City, mkoani Mbeya, Yanga walitangaza nia ya kukata rufaa wakipinga matokeo ya mchezo huo wa ligi.
Yanga walifanya hayo kama vile walijiandaa zaidi kushinda na sio sare au kufungwa, ukizingatia kuwa ni jambo la kawaida katika mpira wa miguu duniani kote.
Na sio Yanga tu, ila hata Simba mara kwa mara imekuwa ikiingia kwenye wasiwasi wa aina yake kutokana na mashabiki wake au viongozi kukaa chini na kusubiria ushindi.
Hii sio haki hata kidogo. Katika mchezo wa soka, hata viongozi au mashabiki lazima waelewe kuwa lolote linawezekana. Kama wao wanataka washinde, hata wenzao nao wanataka ushindi.
Hakuna timu inayoingia uwanjani huku ikitaka ifungwe. Inapotokea tofauti, basi huwa matokeo ya kawaida ndani ya uwanja, hivyo kwa timu zetu lazima zijiandae.
Ili timu iweze kushinda uwanja lazima ijipange. Ijipange kwasababu kila timu inahitaji ushindi. Huu ni wakati wa timu hizo kujitambua kwa ajili ya kukuza soka letu.
Inauma sana Yanga kulalamikia matokeo ya Mbeya City kama vile wameonewa na walistahili kushinda. Kwanini? Kwani Mbeya City nao si timu ya kushinda mbele za wengine.
Au hawa Mbeya City wamekuja kwenye ligi kushiriki na kusindikiza wengine ndani ya uwanja? Yanga, Simba na timu nyingine zote zinapaswa kuwa makini na kucheza soka lao la uhakika.
Inapotokea inafungwa au kutoka sare haipaswi kuanza kutafuta mchawi maana katika mpira wa miguu lolote linawezekana. Huu ndio ukweli wa mambo na lazima tuukubali.
Japo tunazipenda sana timu zetu, ila si wakati muafaka wa kuleta chokochoko inapopata matokeo mabaya. Hakuna sababu ya kulia na kutoa lawama.
Ndio inawezekana kabisa mwamuzi akawa ameibana timu, ila tusilione jambo hilo kwasababu tumefungwa au tumepata sare. Japo wapo watu wanaodharau timu zilizopanda daraja, lakini nazo zinautaka ushindi na ndio kilichowaleta kwenye ligi Kuu.
Nafikiri Yanga na timu nyingine zote zinapaswa kuwa makini katika kucheza soka lao la ushindani na sio kuanza kutoa lawama kwasababu wamefungwa au wametoka sare.
Huu ndio ukweli wa mambo, hivyo siwezi kuvumilia kuona baadhi ya timu zinajiandaa zaidi kushinda na inapotokea tofauti kunaibuliwa mkanganyiko usiokuwa na kichwa wala miguu.
Tubadilike kwa ajili ya kuokoa soka letu. Tunahitaji soka la ushindani ndani ya uwanja. Katika hilo, kila timu icheze soka lake ili ipate matokeo mazuri ndani ya uwanja.
Na inapotokea tofauti basi mkubali matokeo na mjipange kwa mechi zijazo, maana ni dhahiri kufungwa, kushinda na kutoka sare ni jambo la kawaida katika ligi yoyote duniani.
kambimbwana@yahoo.com
+255712053949

No comments:

Post a Comment