Pages

Pages

Saturday, September 28, 2013

Kwanini tunaandaa tamasha la Utamaduni wilayani Handeni mwaka huu?


TAMKO LA KUFANYIKA KWA TAMASHA LA UTAMADUNI HANDENI

NDUGU ZANGU WATANZANIA
NDUGU ZANGU WANA HANDENI
NDUGU MDAU WA UTAMADUNI, MABIBI NA MABWANA
SALAAM!
Mkuu wa Wilaya Handeni, Muhingo Rweyemamu, pichani.
Kwa heshima kubwa kwako naomba niwasilishe ombi kwenu kwa mdau yoyote wa utamaduni na Mtanzania kwa ujumla juu ya kuandaa Tamasha la Utamaduni wilaya ya Handeni, mkoani Tanga, ifikapo Desemba 14 mwaka huu.
Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya Handeni, Dr Khalfany Haule, pichani.
Tamasha hilo tunakusudia kufanya katika Uwanja wa Azimio. Hata hivyo, Uwanja huu wa Azimio upo kwenye matengenezo, hivyo tunaweza kuendelea na tamasha letu kwa upande usiokuwa kwenye ukarabati.
Mbunge wa Handeni, Dr Abdallah Omari Kigoda, pichani.
Ndugu mdau na serikali kwa ujumla; kwa muda mrefu sasa kumekuwa kukifanyika matamasha ya kila aina katika mikoa mbalimbali ya Tanzania. Kabla ya yote, napenda kuwapongeza waandaaji wote wanaoandaa matamasha hayo yenye kujenga jamii inayoheshimu utamaduni wao
Kambi Mbwana, mratibu wa Tamasha la Utamaduni wilayani Handeni, mkoani Tanga, litakalofanyika mwishoni mwa mwaka huu.
Yapo matamasha mengi yanayofanyika katika mikoa hiyo na nisingependa kuorodhesha yote zaidi ya kuwashukuru na kutambua mchango wao katika sekta ya Utamaduni hapa Tanzania.

Kwa kuandaa matamasha hayo na kufanyika kwa mafanikio licha ya kuwa na changamoto za kiubinadamu, imesababisha kujenga usawa kwa wadau wa utamaduni na wananchi kwa ujumla.

Leo hii pamoja namambo mengine, lakini mtu anajiona yupo mtupu, pindi anapodharau utamaduni wao na kukimbilia tamaduni za watu wan je, hususan waliokuwa kweny Mataifa makubwa.

Ndugu zangu wadau wa Handeni Kwetu, wilaya ya Handeni ni kati ya zile zinazokabiriwa na changamoto nyingi mno. Wilaya hii iliyopakana na wilaya Korogwe, imekuwa kwenye joto kubwa la kupokea wageni mbalimbali, huku kila mmoja akiwa na utamaduni wake.

Katika tamaduni hizo, wapo wale wanaoeneza mambo mazuri na wale wanaoeneza sumu, yani tamaduni zisizokuwa nzuri nao pia hawakosekani katika utitiri huo.
Kwa wale wanaofahamu mwingiliano wa watu katika wilaya ya Handeni, watakubaliana na mimi kuwa kuna kubadilishana kwa tamaduni kutoka upande mmoja kwenda mwingine.

Kwakuwa lengo ni kuongeza ufanisi katika kujieletea maendeleo yao; hakuna tatizo katika hilo. Hata hivyo, kwa kulijua hilo, ndipo tulipokaa na kubuni wazo la kuanzisha Tamasha la Utamaduni la Handeni Kwetu.

Wazo na jina la Tamasha hili kwa kiasi kikubwa linatokana na kuwapo kwa Mtandao blog yenye jina la Handeni Kwetu. Blog hii licha ya kupewa jina hilo, lakini inachanganya habari zote bila kubagua.

Ndio Gazeti tando lililojipatia umaarufu kwa kiasi kikubwa na kwa haraka mno. Mbali na blog hiyo, pia kuna forum yenye jina la Handeni Kwetu. Group hili lilianzishwa maalum kwa ajili ya kupeana mawazo na changamoto za kimaisha miongoni mwa jamii.

Group hili lilikuwa na dhamira pia ya kukusanya mawazo mapya na kuunganisha nguvu kwa ajili ya harakati za kimaisha. Tunashukuru kwa wale waliotuelewa na kushirikiana na sisi.

Kwa wale wanaofuatilia group hili, watakubaliana na mimi kuwa kwa sasa tumefikia hatua nzuri zaidi kwakuwa wengi wao wamekubali kushirikiana mawazo yao kwa ajili ya jambo la kimaendeleo.

Ndugu zangu wadau wa Handeni Kwetu; Tamasha la Handeni Kwetu linaandaliwa chini ya Kampuni inayojulikana kama Raha Company And Entertainment, yenye maskani yake jijini Dar es Salaam.

Kwa kupitia Kampuni hii; tunaamini kwa pamoja tutaweza kufanikisha kwa tamasha hili katika ardhi ya wilaya ya Handeni, mkoani Tanga. Sisi tunaamini kuwa changamoto nyingi zinaweza kujitokeza, ila tutakabiriana nazo kwa ajili ya kufungua historia mpya.

Tangu nchi hii ilipopata uhuru wake, katika wilaya ya Handeni na Tanga kama mkoa hakujakuwa na fursa kama hizo. Vijana wengi wana vipaji au wanapenda kushiriki kwenye mambo ya utamaduni, ila wanakosa sehemu ya kuonyesha kwa vjtendo.

Mbali na hilo, kwa wale wanaotamani kujiingiza kwenye mambo ya utamaduni na sanaa kwa ujumla, wanakosa sehemu ya kuongeza chachu yao kutokana na uhaba wa matasha ya aina hii.

Watu wanajiuliza, hata kama kuna kikundi au mtu anapenda mambo ya utamaduni, ila wapi aende kuonyesha? Swali jingine ni namna gani anaweza kuishi wakati wote anapokuwa kwenye harakati hizo?

Maswali haya na mengine yote yanaongeza ugumu katika kupambana na changamoto za kimaisha na sekta nzima ya Utamaduni. Pamoja na hayo; ndipo tulipoamua kuanzisha wazo hili.

Ndugu wadau wa Handeni Kwetu; Wazo aina hii halijakuja tu kiholela bali liliandaliwa na kupangiwa mtitiriko wote. Hata kuanzishwa kwa blog au group la Handeni Kwetu kulikwenda sambamba.

Ni kwa kupitia blog na group letu, tumeweza kujiingiza katika mtandao mpana wa kuweza kuuza mawazo yetu. Kuwaonyesha watu kile tunachokijua na kukithamini mbele ya jamii inayotuzunguuka.

Watu wanaoishi ndani ya Tanzania na nje ya nchi wamepata sehemu ya kuijua vyema wilaya ya Handeni. Sisi tunaamini kuwa hata kama sio leo au kesho, ila wapo wafanyabiashara, wawekezaji wanaweza kuguswa katika kuitembelea wilaya yetu na kuweka makazi.

Ndugu zangu wadau wa Handeni Kwetu; kwakuwa tayari tumeamua kuanzisha wazo kama hili, ni wakati wako wewe unayeguswa na mambo ya utamaduni kushirikiana na sisi.

Tunakuomba sana, kwa nafasi yako, uweze kushirikiana na sisi katika kufanikisha tamasha hili la Utamaduni la wilaya ya Handeni. Sisi tunaamini ushirikiano ndio unaoweza kufanikisha yote hayo.

Msaada wowote unaoona unafaa tupo tayari kuupokea. Kama unaona una taasisi yako, Kampuni yako au shirika na kuna uwezekano wa kudhamini, basi unakaribishwa, ambapo pia ni nafasi ya kujitangaza kwa wilaya hii.

Nashukuru kwa wale waliokubali kukaa pamoja na kulijadili suala hili hadi kutamani kudhamini katika Tamasha hili litakalofanyika mwishoni mwa mwaka huu.

Maandalizi ya tamasha hili yanaendelea. Mazungumzo mengi yameshafanyika. Hadi kufikisha wazo hili kwenu, tulikaa chini na kujitafakari kwa kina juu ya kufanikisha kwa vitendo suala hili.

Ndugu zangu wadau wa Handeni Kwetu; sisi tunaamini serikali pekee haiwezi kuleta maendeleo ya mtu mmoja mmoja bila hata kushirikiana. Kwa kufanyika kwa tamasha hili, tunajua tutafungua fursa nyingine za kimaendeleo wakati wowote kuanzia sasa.

Tutaweza pia kukutana kwa pamoja watu wote katika tamasha hilo na kuweza kujadiliana juu ya mustakabari wa maisha yetu. Tutaweza kuitangaza vyema wilaya yetu.

Watu wenye nafasi zao, uwezo wao watakapoona juhudi hizo, wanaweza kuingia kwa miguu yote katika uwekezaji wa wilaya hii. Wote tunajua jinsi changamoto za uhaba wa maji na umeme unavyosumbua.

Kwa kufanyika kwa tamasha hili, kuna uwezekano mkubwa makampuni yanayotoa huduma wa umeme wa jua, uchimbaji wa visima na mengineyo kuguswa na kuwahudumia wananchi wote.

Pia tunaamini kuwa kwa kufikia hatua ya kuitangaza kama tulivyofanya kwa kuanzisha blog na forum, basi wageni wenye dhamira wanaweza kutembelea katika wilaya hii hivyo kukuza pato la Handeni na Tanzania kwa ujumla.

HITIMISHO

Tunajua wapo wanaoweza kujiuliza kwanini Handeni? Najua pia wapo watakaojiuliza maana ya Tamasha hili. Najua pia watu hao wanaweza kuingiza fikra nyingine, hasa za kisiasa.

Lakini watu hao wanapaswa kujua kuwa hakuna njia ya mkato inayofanywa katika kufanyika kwa tamasha hili. Ni kutokana na mapenzi ya dhati kwa wilaya hii, mkoa wa Tanga na Tanzania kwa ujumla.

Haya na mengine yote, yamesukuma hamu ya kuanzisha kwa tamasha hili ambalo tunaamini ni la kwanza kuwahi kufanyika kwa historia ya wilaya ya Handeni, mkoani Tanga, hivyo tutafurahi kama kila mmoja ataona faida ya kushirikiana na sisi ili tufanikishe maendeleo.

Katika hilo, tunaomba serikali kwa kupitia Mkuu wa Wilaya Handeni, Muhingo Rweyemamu, Mkurugenzi Mtendaji wa wilaya, Mbunge wa Jimbo la Handeni, Ofisa Utamaduni wa wilaya na viongozi watuunge mkono bila kinyongo chochote kwa faida ya Handeni na watu wake.

Kadri ya mambo yatakavyosonga mbele, tutaendelea kujulishana kwa kupitia njia mbalimbali na kuwapa watu fursa ya kufuatilia mwelekeo wa Tamasha la Handeni Kwetu.

Pamoja ni Ushindi.
Tunathubutu, tutaweza na tutasonga mbele.
Mungu ibariki Handeni
Mungu ibariki Tanzania na watu wake wote.
Kambi Mbwana, Mratibu.
mbwanakambi@gmail.com
+255 712053949
+255 753806087



No comments:

Post a Comment