Pages

Pages

Friday, August 09, 2013

Wazee wa Ngwasuma wajigamba kufanya makubwa leo siku ya Idd Mosi



Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
WADAU wa muziki wa dansi na mashabiki wa bendi ya FM Academia, maarufu kama Wazee wa Ngwasuma, wameaswa kuhuhudhiria kwa wingi katika onyesho la Idd Mosi, katika Ukumbi wa New Msasani Club, ili wapate burudani kabambe kutoka kwa vijana hao.

FM Academia, ipo chini ya Rais wa Vijana, Nyosh El Sadaat, huku akishirikiana na wakali mbalimbali wanaoendelea kufanya makubwa katika tasnia ya muziki wa dansi hapa nchini.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Rais wa bendi hiyo, Nyosh El Sadaat, alisema kuwa kwa mwezi mzima wamekuwa wakijifanya mazoezi kabambe ili kuwapatia ladha adimu mashabiki wao.

Alisema kuwa huku wakiwa na nyimbo zinazoendelea kutamba katika tasnia ya muziki wa dansi nchini, pia imejipanga kutoa shoo kali kwa waimbaji na wanenguaji wao.

“Tunawaomba mashabiki wetu waje kwa wingi katika onyesho letu hilo la Idd Mosi katika Ukumbi wa New Msasani Club, Msasani, ambapo pia kutakuwa na matukio kadhaa yatakayotokea ukumbini hapo.

“Naamini wadau na mashabiki wote watakaohudhuria katika burudani za Idd Mosi wataona jinsi vijana wetu wanavyofanya kazi ya maana katika ufanyaji wa shoo zenye kuacha historia,” alisema.

Ngwasuma inatamba na nyimbo mbalimbali kama vile Vuta Nikuvute, Otilia, Heshima kwa Wanawake, Ana na nyingine zinazofanya vyema katika tasnia ya muziki wa dansi hapa nchini.

No comments:

Post a Comment