Pages

Pages

Friday, August 09, 2013

Sikukuu ya Idd leo, Waislamu wajitafakari upya juu ya mkanganyiko huu usiokuwa wa lazima


Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
LEO ni Sikukuu ya Idd el Fitr. Waislamu wote duniani na wale wasiokuwa waumini wa dini hiyo wanafurahia siku hiyo baada ya kumaliza mwezi Mtukufu wa Ramadhani.
Waumini wa dini ya Kiislamu wakifanya ibada
Takribani siku 30 Waislamu walikuwa kwenye mfungo huo, ambao kuna kila sababu ya waumini hao kujitafakari upya. Kila siku ya Mungu, wenye imani ya dini ya Kiislamu wanatumbukia kwenye mkanganyiko wa aina yake duniani.

Kumekuwa na changamoto nyingi, hasa hili la dini moja kuwa na madhehebu lukuki, tena hata yale yasiyokuwa na tija. Naomba niwe muwazi 
Mimi ni muumini wa dini hii ya Kiislamu. Nimezaliwa katika misingi ya dini hii, hivyo lolote linaloweza kutokea tofauti, nabaki nawaza namna ya kudumisha jamii bora.

Naelewa kuwa Tanzania haina dini lakini watu wake wana dini. Rais Jakaya Mrisho Kikwete anaongoza nchi isiyofungamana na dini yoyote, ila yeye mwenyewe ana dini yake.

Ni wazi tunapaswa kuthaminiana na kuheshimiana pia. Hata hivyo, ni vyema kwenye mapungufu yasemwe kwa ajili ya kujenga jamii bora na kuacha mkanganyiko huu.

Ingawa leo ndio siku ya Idd, lakini jana baadhi ya waislamu waliswali kuonyesha kuwa ndio siku sahihi. Hapa dini moja, lakini inagubikwa na mkanganyiko mkubwa.

Walioswali jana wamezingatia nini tofauti na hawa walioswali leo, yani siku ya Ijumaa? Inawezekana walioswali jana wapo sahihi, lakini ni vyema masheikhe na wanazuoni wakalitolea ufafanuzi suala hili, kwanini ibada moja inayoangaliwa kuandama kwa mwezi na kuzama inapokuwa tofauti bila sababu za msingi?

Sheikhe Mkuu wa Tanzania, Shaban Simba kwa kushirikiana na wanazuoni wengine wa dini ya Kiislamu wanapaswa kujua kuwa dini yao inapotezwa na mitazamo ya kukanganya.

Mtu anaweza kuhoji, huyu anayeswali leo na yule aliyefanya hivyo jana kuna otofauti gani wakati wote wanapaswa kufunga au kufungua kwa kuangalia kuandamana kwa mwezi.

Watu wanasema kuwa mwezi umeandama Oman, Arabun, hivyo ni wakati wao kuswali Idd. Suala hili linachanganya na kuumiza sana vichwa, maana hali hii isipoangaliwa huenda ikaharibu thamani ya Uislamu.

Mtaa mmoja malumbano mengi yanaibuka. Kila mtu anajiona yupo juu ya mwenzake. Huyu amefunga na yule amefungua. Hali hii inauma na kukera kupita kiasi.

Vyema suala hilo likaangaliwa kwa mapana yake. Kuna hatari watoto wanaozaliwa leo wakashindwa kutambua wasimame wapi.

Dini ya Uislamu inakabiriwa na changamoto nyingi na ndio maana hadi leo waumini wake wanalia kukandamizwa, wakati wenyewe wamegawanyika.
Hakuna kinachofanywa kwa ajili ya kuujenga Uislamu na ndio maana hata uwapo wa Simba Baraza la Waislamu Tanzania (BAKWATA), linachanganya kuona wengi wao hawakubaliani nalo.

Lengo si kukashifu ila kuwakumbusha watu wawe makini katika mfumo huu unaoibua maswali kedekede kwenye jamii.
Nakutakia Idd Njema mdau wa Handeni Kwetu.

No comments:

Post a Comment