Pages

Pages

Friday, August 09, 2013

Coastal Union watangaza shangwe zao kesho Jumamosi



Timu ya vijana Coastal Union ya Tanga Tanzania
Kwa mara nyingine tena kesho jumamosi Coastal Union inakuwa karibu zaidi kwa mashabiki na wanachama wake kwa kufanya sherehe ya klabu kama ilivyokuwa mwaka jana ‘Coastal Union Day’.

Sherehe hizo ambazo zitajumuisha kutambulisha wachezaji wote watakaoshiriki ligi ya soka Vodacom msimu huu, pamoja na kukutana mashabiki wa timu kongwe ambapo kilele cha sherehe itakuwa ni mechi dhidi ya Polisi Combine, ambayo ni timu inayounganisha timu zote za jeshi hilo la Tanzania.
Uongozi wa klabu unawaarifu wapenzi wote wa soka mjini Tanga na kwingineko kufika uwanjani mapema kabla ya saa tisa alasiri kushuhudia burudani hizo hasa ile burudani ya kuwaona wachezaji wapya na wa zamani ambao kwa kipindi hiki cha usajili wamekuwa gumzo ndani na nje ya Tanzania.

Tayari wageni kutoka mikoa ya jirani wameshaanza kufurika jijini Tanga na usiku wa leo Mungu akipenda kikosi kamili cha ‘fitna za habari’ ndani ya klabu mwandishi wa klabu Hafidh Kido, pamoja na bosi wake yaani msemaji wa klabu Eddo Kumwembe ambae ni mwanahabari na mchambuzi nguli wa soka nchini, huku hamasa ikishambuliwa na mtangazaji mwenye mbwembwe nyingi na historia ya soka la Tanzania kutoka Clouds Media Group, Mbwiga wa Mbwiguke (mkola wa nyani kibwaya mkia), ambapo watakuwa ndani ya gari la mkurugenzi wa ufundi Nassor Ahmed ‘Binslum’.

Sherehe hizi hazihitaji kuhadithiwa ni vema ukashuhudia mwenyewe, wale wafia Coastal Union ama Coastal Nyumba itakuwa ni Eid kwao kwani kwa waumini wa kiislamu leo kuna Eid mbili yaani Ijumaa na Eid El Fitri, pia wale mashabiki wa Coastal Union wa imani zote kesho itakuwa sikukuu yao pia.

Ikumbukwe mechi ya kesho dhidi ya Polisi combine itakuwa mechi ya tatu ya kirafiki kujiandaa na msimu huu ambapo mechi mbili zilizotangulia Coastal Union iliibuka na ushidi wa 1-0 dhidi ya URA ya Uganda na 1-0 dhidi ya Simba SC, mechi zote zilichezwa uwanja wa Mkwakwani.

Coastal Union, inawatakia Eid Mubarak waislamu wote ulimwenguni. Kauli mbiu mwaka huu ‘Ubingwa lazima’.

COASTAL UNION
9 AUGUST, 2013
DAR ES SALAAM, TANZANIA

No comments:

Post a Comment