Pages

Pages

Thursday, August 08, 2013

Rais wa TFF, Leodgar Tenga, anajipaka kinyesi usoni mwake


Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
NI ngumu kuwa na familia bora na yenye kila jema, kama wazazi hawajitambui. Mzazi anaposhindwa kufahamu mbinu za kuiweka familia yake, ni dhahiri ameamua kuyumba na kuwafanya watoto wake waishi kama ndege.
Rais wa TFF, Leodgar Tenga
Kama hivyo ndivyo, tusuburi matusi kutoka kwa wanajamii. Yapo maneno mengi ya kufanana na hayo, huku muktadha wote ukihusiana na Rais wa Shirikisho la Soka nchini (TFF), Leodgar Tenga.

Katika mpira wa miguu, Tenga ni miongoni mwa wadau wenye heshima kubwa. Kila mtu aliheshimu utendaji wake.

Wengi wanatamani rais huyo wa TFF ajiuzulu ili kuokoa soka letu, maana anachofanya ni kujipaka kinyesi usoni mwake.

Badala ya kujenga, anabomoa. Watanzania hatufahamu kwa kupita ili tutokee peupe, hasa migororo inayochipua na kukosa mbinu zenye tija, kama vile ligi bora, timu za Taifa zenye ushindi na kuendeleza soka la vijana ambao ndio msingi wa maendeleo ya mpira wa miguu duniani.

Tenga anachofanya ni kuweka njia ya maswahiba wake, bila kujua kuwa anachafuka mtaani. Ule umahiri wake unaotajwa kila kona, unapukutika kama barafu juani.

Hali inavyoonekana, Uchaguzi wa TFF kufanyika mwaka huu ni ndoto, ukizingatia kuwa hakuna mipango, ingawa ulikuja ujumbe kutoka Shirikisho la Kimataifa (FIFA) kwa ajili ya kukutana na wadau wa michezo, wakiwamo wale walioenguliwa Michael Wambura, Jamal Malinzi na wengineo.

Watu wanajiuliza, hivi kweli heshima ya Tenga imetoweka kiasi cha kushindwa kusimamia Uchaguzi hadi waje Wazungu? Wao ndio nani? Je, Tenga aliwekwa na Wazungu madarakani?

Hata Mkutano wa Dharula uliyoitishwa na kufanyika Julai 13 mwaka huu kwa ajili ya kurekebisha Katiba yao, haukuwa na jipya zaidi ya kuleta malumbano zaidi.

Hata serikali ilipinga kupitia kwa Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Amos Makalla aliyewakosoa TFF, akisema sheria hazijafuatwa, hasa wajumbe theluthi mbili kupiga kura za ndio.

Kauli ya Makalla ilikuwa tata kwa TFF ambapo Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah, yeye aliunga mkono na kusema wanasubiri baraka ya Msajili wa Vyama vya Michezo.

Katibu Mkuu wa kilichokuwa Chama Cha Soka nchini (FAT) sasa TFF, Michael Wambura, yeye aliungana na serikali, akisema kuwa Katiba ya TFF ya 2012 ilifutwa na MsajIli wa Vyama vya Michezo na vilabu kwa kuwa ilibadilishwa kinyume cha sheria (BMT)  pamoja na Katiba ya TFF ibara ya 30 kwa kutumia njia ya waraka badala ya Mkutano Mkuu.

Kwa sababu hiyo, Katiba halali kisheria inayotambulika ni ile ya 2006 na mabadiliko yake. Hali ya utata ilizidi kupamba moto, maana FIFA  na Serikali kupitia wizara yenye dhamana na michezo iliiagiza TFF iitishe Mkutano Mkuu ili ifanye mabadiliko ya Katiba.

Hili lilifuatwa na TFF, japo bado wadau wanaendelea kupinga, wakisema kuwa mchakato mzima unafanywa kiubabaishaji, kutaka kuwekana katika nafasi za uongozi.

Haya yote yaliibuka pale TFF ilipojaribu kuwaengua wadau mashuhuli katika mpira wa miguu. TFF ilimuengua Wambura, watu wakajua labda ni lile sakata lake la kupeleka mambo ya soka mahakamani.

Likatokea pia kwa Malinzi. Kwa kupitia Kamati ya Uchaguzi na Nidhamu, ilimtupa tena aliyekuwa mgombea wa nafasi ya Urais wa TFF, Malinzi na kuzua taharuki.

Hata wale waliokuwa kimya waliona uozo wa TFF. Waliona hata wale vipofu wasiojua mchanganuo wa sheria na Katiba ya Shirikisho hilo linaloendeshwa kwa rimoti kwa sasa.

Haya ni matatizo makubwa. Udhaifu wa Tenga katika miaka miwili hii, ikiwa ni harakati zake za kutaka kumuachia mtu anayefanana naye.

Kwa mujibu wa sheria, msajili husajili mabadiliko yoyote ya Chama kilichosajiliwa chini ya Sheria ya BMT kwa kuzingatia  Sheria NA 12 ya 1967 na marekebisho yake NA 6 ya 1971 ya Baraza la Taifa la Michezo pamoja na  Kanuni za Baraza la Michezo la Taifa  na Kanuni za  Usajili NA 422 za1999.

Katiba pia ni nyaraka ya kisheria hivyo chombo chenye mamlaka kisheria hapa Tanzania ya kuitafsiri ni Mahakama pale pande mbili zinapotofautiana juu ya tafsiri ya Katiba.

Ndio maana kwa kuzingatia haya, hata msajili wa vyama vya michezo amechelewa mno kubariki mkutano huo wa TFF ili chachu ya kuelekea kwenye Uchaguzi huo.

Yote haya yamekuwa yakisababishwa na udhaifu wa Rais Tenga, ukizingatia kuwa ndio kila kitu. Tenga akishindwa kusimamia masuala ya soka, hakuna anayeweza kuweka mambo sawa.

Hili ni tatizo kubwa, hivyo Tenga anapaswa kuona namna gani heshima yake iliyojengeka katika jamii inaendelea kuchanua. Huo ndio ukweli. Vinginevyo, hakuna kiongozi atakayechekwa zaidi ya Tenga.

Akiwa Rais wa TFF, Tenga amekuwa akipata bahati ya kuungwa mkono na kila mtu Tanzania. Wananchi wamekuwa wakiingia kwa wingi katika viwanja vya soka kuangalia mechi za timu ya Taifa au klabu.

Mamilioni ya shilingi yanapatikana. Wadau na makampuni yanaendelea kumwaga fedha za kutosha. Tenga anataka nini tena? Kwa kutumia wadau hawa tu, soka la Tanzania lingechanja mbuga.

Lakini hakuna kitu. Ni malumbano usiku na mchana. Watu wamekuwa wakitoana macho mchana kweupe. Wenyewe wanasema wanashughulikiana. Siasa zimeingizwa katika masuala muhimu ya mpira wa miguu.

Makalla akiwa kama Naibu Waziri anaona haiwezekani Tenga na TFF yake wafanye mambo bila kufuata sheria. Wakati yeye anaaamini hilo, TFF wao wanacheka wakiangalia tamko la FIFA, kuwa serikali haipaswi kuingilia masuala ya soka. Tamko hili linawabeba. Wataendelea kufanya ‘madudu’ yao miaka nenda rudi.

Nani wa kuwakosoa? Huu ni ubabaishaji wa aina yake. Hatuwezi kusonga mbele kamwe. Soka la Tanzania litabaki kama lilivyo kama mmea unaoshambuliwa na wadudu.

Pamoja na yote hayo, bado lawama zitabaki kwa Tenga na viongozi wenzake, akiwamo Sunday Kayuni, Mkurugenzi wa Ufundi wa TFF, ambaye hana anayempenda.

Taasisi za serikali zinazochukiwa kwa sasa, TFF inaongoza. Japo wakiambiwa hili watakataa. Ni wakati wao kujirekebisha kama wanahitaji kunyanyua soka la Tanzania.

Waache ubabaishaji. Tenga anapaswa kukumbuka namna gani Watanzania walivyompenda kwenye nafasi hiyo. Leo amesahau? Nani amemroga Tenga hadi kuchafua historia yake?

Kuna kila sababu ya kufahamu namna ya kulikomboa soka letu. Kila mtu awe na utu pamoja na mapenzi mema na masuala ya michezo, hususan mpira wa miguu unaopendwa duniani kote.

0712 053949
Mwisho

No comments:

Post a Comment