Pages

Pages

Friday, August 30, 2013

Pitia maoni ya Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Leonidas Gama, juu ya Rasimu ya Katiba

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama akizungumza na Waandishi wa Habari (hawapo pichani) ofisini kwake.
Kwa Mujibu wa Rasimu ya Katiba wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Sura ya sita na Ibara zake inazungumzia kuwapo kwa muundo wa shirikisho wa serikali tatu.Serikali ya Muungano, serikali ya Tanzania bara na Serikai ya zanzibar na kwamba kudumu kwa Muungano pamoja na sababu nyingine ni dhamira ya Watanzania wote.

Ni kweli Muungano ni dhamira ya dhati ya wanaoungana na kwa Muungano wetu ni dhamira ya Watanzania wote, dhamira ya dhati ya kuudumisha muungano ni ile ambayo inakubalika na inaendana na Matakwa ya walio wengi.
Leonidas Gama, Mkuu wa Mkoa Kilimanjaro
Kwa mazingira ya nchi yetu na mazingira ya kibinadamu, sio rahisi katika Taifa kama hili lenye watu zaidi ya  milioni arobaini, tukawa na dhamira moja, tutajiridhisha kinadharia tu kuwa Muungano utadumu kwa vile tuna dhamira nao, huku ni kujidanganya. Ni dhahiri kuwa ikitokea katika mfumo huu wa serikali tatu, tukapata kiongozi mkuu, ama chama, ama chombo chenye mamlaka ya kutunga sheria, ama kundi la watu ambalo dhamira yao ni tofauti na dhamira ya wengi.

Ni wazi kuwa pamoja na dhamira nzuri ya walio wengi wa kudumisha Muungano wa sasa, Muungano utavunjika kwa matakwa ya mamlaka iliyopo. Kwa maoni yangu Dhamira ya Watanzania katika kudumisha Muungano ni sehemu tu ya kuimarisha na sio suluhisho la kudumu kwa Muungano.

Muundo madhubuti unaozuia fursa ya kuvunja Muungano ndio suluhisho sahihi na la kudumu kwa Muungano. Ni vyema Watanzania  tusisahau yale ya mwaka 1977, tulikuwa na Jumuiya ya Afrika Mashariki, wote wana Afrika Mashariki tuliipenda Jumuiya yetu, tulikuwa na dhamira ya dhati ya kuidumisha.

Lakini alitokea mtu mmoja tu kwa matakwa yake, na akili zake alizoziona zinafaa alisababisha Jumuiya ya Afrika Mashariki kuvunjika sembuse Muungano wa Serikali tatu?

Waasisi wa Taifa letu, Hayati Abeid Amani wa Zanzibar na Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere wa Tanganyika, karume walipoanzisha Muungano wa Tanganyika na Zanzibar hawakukurupuka, walikuwa na sababu za msingi za kuunganisha nchi mbili hizi.

Miongoni mwa sababu hizo ni pamoja na Undugu wa damu uliopo kati ya Wananchi wa Zanzibar na Tanganyika na pili ni sababu za kiulinzi na usalama kwa nchi hizi wa mali, rasilimali na watu wake, ninaamini kuwa, sababu hizi bado ni hai hadi  sasa na ni sababu muhimu kwa mustakabali wa Taifa letu.

Watanzania hivi sasa kupitia mabaraza mbalimbali wanaendelea kutoa na kukusanya maoni juu ya katiba. wapo wanaopita huku na huko na wale wanaotumia njia mbalimbali za kutoa maoni yao juu ya Rasimu ya Katiba na hasa eneo hili la muundo wa serikali tatu.

Ni uhuru wa kila mtu kutoa maoni yake, lakini kuna haja ya Watanzania kuwa na tahadhari sana, wapo wanaojua fika kuwa kuwepo kwa serikali tatu, zenye Marais watatu katika nchi yenye mamlaka tatu, ni kuuvunja Muungano.

Hivyo wapo wanaoshabikia serikali tatu, si kwa kuimarisha Muungano ila wanajua kuwa ni kuuvunja Muungano. Wanachelea kuonyesha dhamira yao ya kuuvunja Muungano bali wanashabikia Serikali tatu kwa kujua dhamira yao itatimia.Watanzania tutafakari, tuchukue Hatua

Pamoja na Sababu nyingine nyingi unazoweza kuzichambua juu ya kudumu au kutokudumu kwa Muungano wa Serikali tatu, nimeona ni vyema nipitie maeneo ambayo binafsi nimeona yanaweza kuchochea kuunjwa kwa Muungano wa serikali tatu.

Wengine wanajadili hoja ya gharama kubwa za kuendesha serikali tatu, kwangu hili si hoja, naamini jambo lolote la kheri linahitaji gharama na kama gharama zinaweza kuhimilika, hilo si tatizo.Maeneo yanayoweza kuvunja muungano ni pamoja na:

(i)Uwezo uliosawa ki-uwiano katika kuchangia uendeshaji wa Muungano 

katika ibara ya 215 ya Rasimu, inazungumzia vyanzo vya mapato ya serikali ya Jamhuri ya Muungano, na moja kati yake ni "mchango kutoka kwa washirika wa Muungano" maana yake ni mchango toka serikali ya Zanzibar na kutoka ya Tanzania bara.

Ni dhahiri muundo na mfumo wa uendeshaji wa serikali ya Muungano kiasi kikubwa utategemea mchango huu ambao unategemea uchumi wa serikali mbili zinazounda Muungano, katika mazingira halisi ya Tanzania kwa kuzingatia rasilimali na mali zilizopo katika maeneo ya Muungano yaani Tanzania Bara na Zanzibar ni dhahiri hayatawezesha mchango ulio sawa ki-uwiano katika kuendesha serikali ya Muungano, hii itaifanya Serikali yenye mazingira mazuri ya mali na rasilimali, kulazimika kuiendesha/kuichangia Serikali ya Jamhuri ya Muungano na nyingine kushindwa kuchangia katika hali yoyote ile, mgongano wa kiuchumi na kimaslahi hautaepukika.

Lakini pia katika mazingira ya umoja na mshikamano uliopo sasa kati ya Serikali ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, ambayo ushirikiano katika uendeshaji wa shughuli za kiserikali ni ule usioepukika, (Gharama za uendeshaji na huduma katika serikali kwa mfano- Umeme , Mafuta n.k.)

Hali hiyo katika serikali tatu, haitapata nafasi, serikali itakayochangia zaidi tofauti na nyingine haitakubali hali hiyo. kwa maana ya kiuchumi, pia upo uwezekano wa serikali itakayoshindwa kujiendesha au hata kuchangia, kukopa nje katika mazingira ya kupoteza uhuru wake wa kiuchumi na kiusalama.

Tukumbuke kuwa hadi sasa bado waptu nje ya nchi wanaoitazama Zanzibar kisiwa chetu kizuri kama eneo lao, na bado wanandoto kuwa siku moja watarudi Zanzibar kiutawala.Jee iwapo Zanzibar itashindwa kuchangia katika serikali ya Muungano na kujiendesha kiuchumi ni nini kitatokea?

Ni lazima tukubali Watanzania kuwa uchumi wa nchi hizi unatofautiana sana na kuishi kwetu katika Muungano ni kule kwa kushirikiana kindugu kunakotokana pia na mfumo uliopo wa Muungano, vinginevyo kwa muundo wa serikali tatu, zenye Marais watatu, hili linalofanyika sasa halina nafasizi, ni wazi kuwa nafasi ya kudumu kwa Muungano itakuwa matatani.

(ii) Mgawanyo wa madaraka na mfumo wa kiutawala

Kwa mujibu wa Rasimu ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kutakuwa na Marais watatu na serikali tatu na kwa mujibu wa madaraka na mamlaka, kila Rais atakuwa na madaraka katika eneo lake la utawala.

Katika mfumo wa miliki za mali na rasilimali na utawala wa mali na rasilimali za nchi, kwa sehemu kubwa utakuwa katika mamlaka za serikali ya Zanzibar kwa eneo la Zanzibar na Tanzania bara kwa yaliyo chini ya Tanzania bara.

Hii ni pamoja na utawala wa serikali, serikali za mitaa, tawala za mikoa na uteuzi wa mamlaka za utendaji, Ardhi, Maji, Barabara, Huduma za kijamii ikiwemo Elimu, Afya n.k.

Kiutawala Rais wa Jamhuri ya Muungano hatakuwa na eneo la utawala kirasilimali hasa rasilimali watu, Rais wa Muungano hatakuwa na mamlaka na madaraka za kiutendaji, rasilimali na huduma za kijamii na za maendeleo, mamlaka za kuagiza wala kukemea.

Katika hali hii utendaji kazi wa Rais wa Muungano ambaye ndiye Kiongozi Mkuu, hautakuwa wenye mamlaka na madaraka. Uwepo wa mgongano wa kimadaraka kati ya Jamhuri ya Muungano na serikali ya Zanzibar na ile ya Tanzania bara hautazuilika. Na ni ukweli Rais wa Jamhuri ya Muungano atakuwa Boya, ataelea hewani.

(iii) Mfumo wa utawala na Vyama vingi vya siasa

Kwa mujibu wa sura ya kwanza ya Ibara ya 1 (2) ya Rasimu ya Katiba, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni shirikisho la kidemokrasia linalofuata mfumo wa vyama vingi vya siasa.

Kwa mtazamo wangu; katika mfumo wa kidemokrasia unaozingatia vyama vingi vya siasa, ni dhahiri kuwa utawala na mamlaka za utawala zinaweza kuwa katika matokeo ya mchanganyiko mkubwa wa Vyama mbalimbali vya kisiasa, matokeo ya chaguzi za Rais, wabunge na Madiwani zinaweza kutoa sura tofauti na katika maeneo tofauti.

Ni ukweli kuwa kila chama cha siasa, kina mfumo wake na malengo yake, kisiasa tunaamini nchi ni moja, na wote tunajenga nyumba moja kwa hiyo tofauti zetu za kisasa zisivuruge umoja na mshikamano wetu. Kwa nadharai ya kisiasa, hii ni sahihi, lakini kihalisia ni dhana isiyotakiwa kuiamini.

Upo uwezekano wa chaguzi katika serikali tatu, zikapata vyama vinavyoongoza serikali kwa tofauti kwa kila eneo la utawala: kwa mfano serikali ya Jamhuri ya Muungano ikaongozwa na chama kingine, Serikali ya Zanzibar ikaongozwa na chama kingine na ile ya Tanzanzia Bara inkaongozwa pia na chama kingine.


Kwa vyovyote vile mamlaka na madaraka yatawataka Marais wa Bara na yule wa Zanzibar kutii mamlaka ya Rais wa Muungano. Ni rahisi sana kusema hakuna tatizo lolote, wataongozwa na Katiba lakini yeyote anayejua mwenendo wa siasa za Tanzania hivi sasa na matarajio za siasa za baadae zinazoendelea hapa nchini, kwa tofauti ya sera, itikadi na mitazamo ya kimaslahi katika vyama vyetu na jamii kwa ujumla.

Kwa mtazamo wa yeyote yule ni kuwa Muungano huu wa serikali tatu, wenye Marais watatu ni ndoto kuamini kuwa utadumu katika mazingira ya utawala wa vyama tofauti katika serikali zilizopo.

Tukumbuke  Historia ya Muungano iliyoundwa kwa utaratibu unaofanana na huu ambao umeishia kusambaratika kama vile Muungano wa iliyokuwa Yugoslavia na Usavieti. Katika Yugoslavia, jimbo la Albania, ndilo lilikuwa la kwanza kutaka kujitenga na hatimaye kulitumbukiza Taifa katika vita vya wenyewe kwa wenyewe huku na majimbo mengine kama Serbia na Montenegro yakidai kujitawala; hatima na matokeo ya Muungano huo ni Kuvunjika kwa Muungano wao. 

Zipo nchi nyingi zimesambaratika kutokana na mifarakano midogo midogo ya kijamii: kumbuka Ethiopia, Eritrea, Somalia, Sudani na Sudani ya Kusini n.k

"Mimi bado naamini kuwa suluhisho la kero la Muungano siyo kuwa na serikali tatu, bado tunao uwezo na nafasi kubwa ya mjadala zaidi.Tujiulize ni nchi gani duniani yenye Marais wa watatu, wenye serikali tatu na wakakaa katika mfumo huu wa Muungano wakafanikiwa?

tujifunze kutoka kwa wenzetu walioungana duniani, Marekani imeundwa na majimbo zaidi ya 52, lakini pamoja na majimbo hayo kuwa na nguvu na rasilimali zote, bado Rais mwenye Nguvu ni mmoja tu.

Marekani haijagawa mamlaka, madaraka, usimazi, utawala na maamuzi kwa mtu zaidi ya mmoja na ndio maana Taifa la Marekani linaendelea kuwa imara sio ndani tu bali hata nje ya mipaka yake.
Watanzania wa Bara na Visiwani, kama tunadhamiria kweli kujenga umoja wa kitaifa kwa mfumo wa Serikali tatu tungekuwa na Serikali zenye muundo huu; Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yenye Rais aliyechaguliwa na Watanzania wote.

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar yenye Waziri Mkuu mtendaji aliyechaguliwa na Bunge la Jamhuri Serikali ya Tanzania Bara aliyechaguliwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano.

Hili ndilo suluhisho pekee kwa wale wanaotaka Serikali tatu, lakini nina hakika kwa sababu za tulio wengi kutawaliwa na homa ya madaraka, wazo hili wengi watalipuuzia bila kujali kuwa ndilo suluhisho.

Tujiulize ni kweli tunautaka Muungano au tunasema tunaimarisha Muungano kumbe dhamira zetu zinataka tuone Muungano unakufa kwa vile eti kwa nini Zanzibar wana bendera yao, wana wimbo wao wa Taifa, wana madai yao kila kukicha.

Watanzania wenzangu, Muungano unaondoka, chozi la Baba wa Taifa litatushukia. Kuna tafsiri fulani nimesikia zikitolewa na wale wanaotetea muundo wa serikali tatu, Jaji Warioba na kundi lake katika tafsiri zao nimesikia wakimnukuu Baba wa Taifa kupendekeza serikali tatu.

Tuache kutafsiri na kupindisha maneno ya Baba wa Taifa kwa kile tunachokitaka sisi, maana wapo wanaotumia maandishi mbalimbali ya Baba wa Taifa, kumpandikizia tafsiri ya kutaka serikali tatu kwa matakwa yao.

Baba wa Taifa amefariki akiamini na akiwa na msimamo mmoja tu “Muungano wa Serikali mbili kuelekea serikali moja”. Mwanamapinduzi Mzee Abeid Amani Karume amefariki akiamini juu ya Tanzania yenye Muungano wa Serikali moja.

Mungu Ibariki Muungano wetu. Mungu ibariki Tanzania.
 
Makala hii imeandaliwa na Mwalimu Leonidas T. Gama
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro.
haya ni Mawazo binafsi na Mapendekezo yangu!


No comments:

Post a Comment