Pages

Pages

Wednesday, August 07, 2013

MGODI UNAOTEMBEA:Tanzania haina sababu ya kuivamia Rwanda


Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
NITAMSHANGAA Mtanzania yoyote anayeweza kufurahia nchi za Tanzania na Rwanda kuendelea kurushiana maneno makali kuonyesha uhusiano mbaya ulioanza kwa siku za hivi karibuni.
 Rais Jakaya Mrisho Kikwete, pichani

Tangu Mwezi Mei mwaka huu wa 2013, baadhi ya matamko mabaya yamekuwa yakitolewa na viongozi wa Rwanda. Wanasema mengi kuonyesha chuki zao kwa Watanzania na rais wao kwa ujumla.
Paul Kagame, Rais wa Rwanda
Kwa kuangalia sakata lote linaloshika kasi, ila si sababu ya Tanzania kujibu mashambulizi dhidi ya Taifa hilo linaloongozwa na Paul Kagame, maana ni kuzidi kukuza uhasama huo.

Ni wazi kuwa nchi ya Rwanda inayotajwa kufadhili machafuko nchini Kongo, hasa kwa kikundi cha M23 inaleta chokochoko kwa Tanzania, pale Rais Kikwete, alipowataka wakae na waasi kujadili tatizo.

Hali hii inashangaza mno. Kauli ya furaha inapobadilishwa na kuwa chuki na uhasama, tena bila sababu za msingi. Labda kuna sababu nyingine, ila si haya yaliyozungumzwa na Kikwete.

Wakati naangalia kwa kina mtifuano huo, kwa upande wangu nitakuwa wa mwisho kufurahia au kuombea mabaya kwa mataifa haya mawili, yani Tanzania na Rwanda.

Tanzania ili iweze kukua kiuchumi, inahitaji ushirikiano kutoka kwa majirani zake. Nchi hizi zinategemeana. Rwanda wanaihitaji Tanzania na Watanzania wanahitaji uwapo wa ndugu zao.

Sipendi kuona uhusiano mbaya kwa nchi za Tanzania na Rwanda unakua, nikiamini ni hatua isiyokuwa na faida zaidi ya hasara kwa mataifa haya mawili yanayopigania kujitawala wenyewe.

Katika hotuba yake aliyoitoa mwishoni mwa mwezi uliopita, Rais Kikwete alielezea mambo mengi dhidi ya Rwanda, akisititiza kuwa alinukuliwa vibaya na ushauri wake kupindishwa.

Rais Kikwete aliwatangazia umma kuwa hakuna sababu ya kugombana na Rwanda, japo alikiri kutukanwa na majirani zetu hao.

Haya ni matatizo makubwa kwa viongozi wa Afrika. Kagame, akiwa kama rais wa Rwanda, ni vyema akazingatia nidhamu katika utawala wake.

Kagame anapaswa kujua faida ya amani inavyoweza kuwafanya wananchi wake waishi vizuri. Wananchi wa Rwanda wasingependa kuona wapo viongozi wanaotamani kulifanya Taifa hilo liingie kwenye hatari.

Kadhia waliyoipata mwaka 1994 inatosha. Roho za Rwanda ziliangamia bila sababu. Kama hivyo ndivyo, nani anaweza kusimama hadharani akachochea vita, huku akijua kuwa hana faida navyo?

Nani anayeweza kuelezea faida ya vita, hasa kwa Tanzania na Rwanda, ambazo zenyewe zinahitaji kuishi kwa kutegemea wahisani, Mataifa makubwa?

Huu si wakati wa kujenga uhasama. Huu ni wakati wa viongozi wa nchi za Afrika kukaa pamoja na kusema kwa kauli moja namna ya kuyasaidia mataifa yao.
Mrwanda apinge kwa nguvu zote kama kuna chokochoko zinazofanywa, zinazotakiwa kufanywa na viongozi wao leo au kesho.

Mtanzania, Mkenya, Mburundi, Mkongo na wengine wote wapinge kama kuna anayetaka kumsumbua mwenzake kwa namna moja ama nyingine.

Inawezekana wakati mwingine kunatokea migongano ya kimaslahi, ila hakuna ugomvi usiokuwa na njia ya kusuluhishwa. Mazungumzo mara kadhaa huleta tija na kudumisha jamii bora.

Hakuna nchi iliyoendelea kwa kupenda vita, hasa hizi zinazoishi kwa misaada kutoka nchi za watu. Ukiacha roho za watu zinavyoangamia katika machafuko, pia nchi zinatumia gharama kubwa kujilinda au kujibu mashambulizi au kununua silaha kwa fedha za kujenga shule, vituo vya afya na huduma nyingine muhimu kwa wananchi wao.

Rais Kikwete ameyaona haya. Na kutokana na ustahimilivu wake, akabaini kuwa hakuna sababu ya maana ya kulumbana na Rwanda, sababu ikiwa kuwashauri kumaliza tofauti zao na waasi.

Kauli hii haikuungwa mkono na Kagame. Maneno ya kejeli yakaanza kushika kasi, sambamba na vijana wao, ikiwa ni njia ya kufikisha matusi kwa Watanzania kwa njia mbalimbali, ikiwamo mitandao ya kijamii.

Ukiingia katika mitandao mbalimbali na kufuatilia uhasama huu, utagundua kuwa umefikia wakati mbaya mno. Inahitaji moyo mno kujitangaza kuwa wewe ni Mtanzania mbele ya Mrwanda.

Hii si njia nzuri kwa mataifa haya. Nchi ya Tanzania amani ni jambo la lazima kwa wananchi wake. Ingawa ina makabila zaidi ya 120, ila yameishi kwa upendo wa hali ya juu.

Wanapokutana Wazigua na Wasukuma, huwezi ona tofauti yao. Wanaishi kama ndugu. Huwezi kuona malumbano kati ya Wangoni na Wachaga. Haya ni mambo ya kupongezwa na Watanzania wote.

Amani hii ni tunu kutoka kwa Mungu. Ingawa hatuna utajiri wa kupindukia, ila maisha yetu yamekuwa na furaha tele, jambo linalotangaza sisi ni nani.

Kwasababu hiyo, yoyote anayeona ana hamu ya kulichanganya Taifa hili, basi aangalie mara mbili. Japo uwezo wa kufanya lolote upo, lakini nini chanzo?

Chanzo kiwe hiki cha viongozi kushauriana? Kwani kuna ulazima kufuata ushauri ambao huutaki? Kwanini sasa ubabaike kwa kushauriwa?

Alipokuwa Tanzania katika ziara yake, Rais wa Marekani, Barrack Hussein Obama, aliulizwa juu ya machafuko yanayoendelea nchini Kongo.

Obama alijibu huku akionyesha kuwa rais wa Tanzania, Kikwete, ana uwezo wa kuyafanyia kazi hayo, maana yapo ndani ya uwezo wake.

Kauli hii sio tu imemjenga Kikwete nje ya mipaka yake, pia imeonyesha namna gani Watanzania wanaongozwa na rais mwenye mtazamo wa kina.

Haya yanapotokea, kwa rais asiyejitambua, rais mwenye ubinafsi na ubabe usiokuwa na tija, ana uwezo wa kuchukia kama inavyoonekana sasa.

Anawaza kwanini asiwe yeye? Na inapotokea mmoja wapo, ikiwamo Rwanda inaanzisha chokochoko, kama mmoja wao anakuwa hajitambui, uhasama huo utaongezeka.

Ni vyema wananchi wakapinga kwa nguvu zote kama viongozi wao wanataka kuwaingiza kwenye uhasama. Watu zaidi 500,000 waliripotiwa kupoteza maisha katika mauaji ya kimbari mwaka 1994.

Ni idadi kubwa mno. Sitarajii kuona vifo hivyo vimesahauliwa na wananchi sambamba na viongozi wao. Ndio maana nasema, suala la machafuko si la kuchekea.
Linazalisha vizazi tegemezi. Linazalilisha watu kwa kiasi kikubwa mno, hivyo halistahili kuchekewa. Watu wanazikimbia nchi zao bado wanazipenda.

Akina mama wajawazito na watoto ndio wanakuwa wahanga wakubwa katika hilo. Wengine wanapoteza maisha kutokana na njaa, shida ya maji na mengineyo.

Wengine wanaingiliwa kimwili bila lidhaa yao. Kama haya yanatokea, nani anaumia? Ni wakati sasa wa viongozi wa Afrika kudumisha umoja na mshikamano.

Hakuna Tanzania, Rwanda, Kongo, Burundi, Kenya, Msumbiji ama Uganda. Hizi nchi zote zinapaswa kuishi kwa upendo na kushirikiana kibiashara.

Hatuhitaji uhasama wa aina yoyote kutoka Rwanda, kama njia ya kukuza uchumi wa nchi hizi mbili. Wapo baadhi yao wanaochekea machafuko.

Hawa wameshindwa kung’amua machungu wanayokutana nayo wana jamii wengine kutokana na matokeo hayo. Mwisho kabisa, napongeza kwa nguvu zote kauli ya Rais Kikwete, nikiamini kuwa ni mwenye busara.

Pamoja na matusi yote anayotukanwa, akidhalilishwa, ila yeye anaona hakuna sababu ya kujibizana vibaya na majirani zao hao, japo uwezo huo upo.

Rwanda ni Taifa dogo mno. Kinguvu halina ubavu hata robo ya kupambana na ubavu wa Tanzania. Na wenyewe wanajua hilo. Hata hivyo hakuna sababu kubwa juu ya suala hilo.

Muhimu ni viongozi wa nchi zote za Afrika kupendana, kuhubiri amani katika vikao vyao, maana ndivyo vinavyoweza kuleta maendeleo kwa nchi zao.

Watanzania tunawapenda na kuwaheshimu majirani zetu, japo sio sababu ya kuonekana si lolote, maana tunajua uwezo tunao, tena mkubwa mno.
+255 712053949

No comments:

Post a Comment