Pages

Pages

Wednesday, August 07, 2013

Maonyesho ya Elimu Expo na matarajio ya kukuza kiwango cha elimu Tanzania


Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
KUTOKANA na umuhimu mkubwa wa elimu duniani, Tanzania ni miongoni mwa Mataifa yanayoweka mkazo mkubwa katika suala hilo, kwa kutumia pia ushirikiano wa wadau mbalimbali.
 Kelvin Twissa kutoka Vodacom akizungumza jambo, akifuatiwa na Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Phillip Mulugo na muandaaji wa maonyesho hayo, Joel Njama.

Walimu, wazazi, wanafunzi pamoja na taasisi nyingi zimekuwa zikifanya majadiliano ya kila namna, hasa lengo likiwa kutafuta changamoto zinazoikabili Tanzania.

Makampuni ya kila aina yanaibuka kukarabati majengo ya shule za Msingi na sekondari, kununua vitabu na vitendea kazi vinavyoweza kumfanya mwalimu na mwanafunzi kupata urahisi katika suala zima la elimu.

Miongoni mwa Kampuni zinazojitokeza kusaidiana na serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni Masoko Agencies Tanzania Ltd, itakayoandaa maonyesho ya Elimu Expo, katika Viwanja vya Posta, Kijitonyama, jijini Dar es Salaam, kuanzia Agosti 30 mwaka huu.

Maonyesho hayo yataandaliwa kwa udhamini mkubwa wa Kampuni ya Simu za Mikononi ya Vodacom Tanzania, ambapo mapema wiki hii walitangaza mpango huo mbele ya Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Tanzania, Phillip Mulugo.

Katika mazungumzo yaliyofanyika wiki iliyopita, jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Masoko Agencies Tanzania Ltd, Joel Njama, ambaye ndio muaandaaji Mkuu wa maonyesho hayo, anasema kuwa lengo ni kuweka mpango wa kuwezesha masuala ya elimu Tanzania.

“Mji wa Dar es salaam umeandaliwa kuwa mwenyeji wa maonyesho ya elimu ya kwanza ya aina yake mwaka huu, katika uwanja utakaoruhusu muingiliano na majadiliano kati ya
watengenezaji wa sera, wapenda maendeleo, watunzi mbalimbali, wazazi, wanafunzi, na jamii kwa ujumla.

“Maonyesho haya yamepewa jina la Vodacom Elimu Expo yakiwa na lengo kuwahusisha wadau wote wa elimu katika kuangalia mianya iliyopo, kugundua changamoto na kutafutia suluhisho ili kukuza elimu Tanzania,” alisema.

Njama anasema kuwa Elimu Expo itafanyika kwa siku tatu kuanzia Agosti 30 mwaka huu, huku wasemaji mbalimbali kutoka mashirika na viwanda tofauti ambavyo kwa pamoja vitafanikisha maendeleo ya elimu hapa nchini.

Kuwa elimu ndio ufunguo wa maendeleo katika Taifa, hivyo kila mtu ana wajibu na haki ya kuweza kufanya mikakati ya kuendeleza sekta hiyo muhimu.

Kwa mujibu wa Njama, maonyesho hayo yatashirikisha wageni zaidi ya 150,000, huku dhamira ya dhati ikihusisha mbinu za kushirikiana kwa wadau wote, hasa serikali.

Mdau huyo wa elimu anasema kuwa Tanzania imekuwa ikikabiriwa na changamoto nyingi za kielimu, hivyo anaamini kwa kukutana katika maonyesho hayo, kila kitu kitafanikiwa.

Naye Mkuu wa Mawasiliano na Masoko wa Kampuni ya Simu za Mikononi ya Vodacom Tanzania, Kelvin Twissa, anasema kuwa wameamua kuingia kwenye tukio hilo la siku tatu kwa ajili ya kukuza harakati za kielimu.

Anasema Kampuni yao imekuwa ikipenda kuwekeza pia katika elimu, ikiamini ndio ilipokuwa watalaamu, madaktari, walimu na watu wengine muhimu.

Ukiacha kujenga au kukarabati shule nyingi za msingi na sekondari wanazojitolea kila wakati, pia wameruhusu kijiji chenye mnara wao wa simu kutumika kutoa umeme katika shule ya kijiji husika.

“Huu ni mpango kabambe ambao sisi Vodacom tunaamini kuwa tutafanikisha kukuza kiwango cha elimu hapa nchini kwa namna moja ama nyingine.

“Kuna baadhi ya vijiji ambavyo havina umeme, ila mnara wetu mmoja unaweza kutoa umeme masaa 24 bila kuzimika, hivyo tunaamini wanafunzi wanaosoma hasa nyakati za usiku wanaweza kufanikiwa,” alisema.

Akielezea matumaini yake juu ya Vodacom Elimu Expo, Twissa anasema kuwa kufanyika kwa maonyesho hayo pia kutasaidia kubainisha changamoto muhimu, ambapo wadau wote watajua na kusonga mbele.

Anasema moja ya changamoto hizo ni ile ya kulipa ada ya shule, ambalo limeonekana ni jambo la kuchosha na kupoteza muda kwenye mabenki mbalimbali.

“Ni jambo la kusikitisha kabisa kuchelewa kulipa ada ya shule kwa sababu ya foleni zilizopo katika benki
zetu.

“Kampuni ya mawasiliano ya Vodacom imekuja na njia ya kuitatua changamoto hii, hivyo kuna uwezekano wa kulipa ada ya shule kupitia M-Pesa,” alisema.

Naye Mulugo, Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, anasema kuwa serikali itaunga mkono maonyesho hayo ili yafanikiwe hapa nchini.

“Hii ni fursa kwa wale wote ambao wanajadili na kuja na suluhisho ambalo litapelekea elimu Tanzania kuendelea katika njia iliyo bora.

“Mafanikio yanayopatikana kutoka kwenye mikakati na juhudi za wadau mbalimbali ndio jambo la msingi ambalo kwa kiasi Fulani linakuza kiwango cha elimu hapa nchini, hivyo kuwafanya wazazi waone umuhimu wa kuwabakiza watoto wao ili wasome kwenye shule mbalimbali za Tanzania,” alisema Mulugo.

Waziri Mulugo anasema Taifa linahitaji mchango wa wadau mbalimbali, ndio maana inaona maonyesho hayo ya Agosti 30 yatakuwa na mashiko na kufanikisha kwa kiasi kikubwa juhudi za kukuza kiwango cha elimu Tanzania.

Mwisho

No comments:

Post a Comment