Pages

Pages

Saturday, August 10, 2013

MAMBO FULANI MUHIMU:Umesahau nini kwa mpenzi wako wa zamani?



Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
IDDI Mubarak msomaji wangu mpendwa, huku nikiamini kuwa tutaendelea kuwa pamoja siku ya leo, kama ilivyokuwa kawaida yetu ya kukutana kwenye kona hii kujadili mambo mbalimbali ya uhusiano na maisha.
Raha kwenda mbele
Nakushukuru kama wewe ni miongoni mwa wasomaji wa ukurasa huu, unaokujia kila Jumamosi, huku wiki hii ikiangukia katika Sikukuu ya Idd, baada ya kipindi cha mwezi mzima ndani ya mfungo wa Ramadhan.

Ndugu msomaji wangu mpendwa, kuna vitendo vinavyoumiza kichwa, hivi ni kuona baadhi ya watu wanajenga ukaribu wa kupitiliza kwa wapenzi wao wa zamani kiasi cha kuzua hofu kwa wenzi wao.

Ukiacha wale waliopata mtoto katika kipindi cha uhusiano, au wanandoa walioachana huku wakiwa na mtoto, hao wanaruhusiwa kuwasiliana mara kwa mara kulea mtoto. Ubaya upo kwa wale walioachana, lakini muda wote wapo katika mawasiliano makubwa, huku wakiwa hawana chochote kinachowaunganisha.

Wakati mwingine hualikana chakula cha mchana au usiku, muda mwingine huchukuana na kwenda katika majumba ya starehe, kama vile bado wapo kwenye mapenzi kama ilivyokuwa awali.

Hii ni mbaya sana, maana kama mlishaachana huo ukaribu uliojenga kwa sasa ni ishara gani? Ndio kusema bado mnapendana? Kama hivyo ndivyo, kwanini mliachana?

Je, huoni sasa ni wakati wako kurudiana na huyo mpenzi wako wa zamani, ili kumuondolea jakamoyo mpenzi wako mpya? Haya ni maswali ambayo tunapaswa kujiuliza kila mara.

Kuna baadhi ya watu ambao baada ya kuachana na wapenzi wao wa zamani, hushindwa kujizuia na kutafuta mahala kwa kujiegemeza, ili watulize majonzi ya kuachwa.

Kwa bahati nzuri wakapata watu wanaowapenda kwa dhati, ambao wamekuwa wakiwajali kwa kila wanachokitaka katika suala zima la mapenzi wanayoyapata, wanatembea kifua mbele wakithaminiwa na wapenzi wao wapya.

Lakini kutokana na ujinga, anajikuta anaingia tena katika urafiki na yule aliyeachana naye kipindi cha nyuma, sasa unabaki unashangaa chanzo na mwelekeo wake.

Si kila mtu anahitaji kuona mchumba wake aliyekuwa naye ana ukaribu na mpenzi wake wa zamani, hakuna anayependa suala hilo. Ni wazi wapenzi wa zamani wanapokuwa na ukaribu wa kupitiliza, suala la ngono kwao ni lazima.

Kama watafanya ngono, si kweli kama wataogopana kiasi cha kuweza kujikinga katika suala hilo, zaidi wataingiliana kimwili bila tahadhari yoyote, matokeo yake ni kupeana maradhi.

Hapo ndipo utakuta cheni kubwa ya maambukizi, kwani wakishaambukizana maradhi huwapelekea wapenzi wao hao wapya, ukiwa ni mtindo usiokuwa na mashiko hata kidogo. Ni jukumu letu kujua hakuna ulazima wa kudumisha ukaribu na wapenzi wetu wa zamani.

Watu wabakie kulea watoto, kama katika hatua ya mapenzi yao walibahatika kupata zawadi hizo kutoka kwa Mungu. Na kama unaona kuna ulazima wa kuwa na ukaribu na mtu wako wa zamani, basi jaribuni kuzungumza namna ya kurudiana, ili usilete mkanganyiko kwa wengine.

Kuachana kupo, lakini pia kurudiana si jambo geni duniani, ukiona huwezi kukaa bila kumuona mpenzi wako wa zamani, kumpigia simu au kuwasiliana naye muda wowote, mpigie magoti mrudiane.

Kinyume na hapo, utasababisha maswali mengi kutoka ndani ya moyo wako na jamii kwa ujumla, utampa presha uliyekuwa naye, maana anaona ujinga wako, kimekushinda mwenyewe mwanzo na sasa unajirudisha kienyeji.

Katika jamii wapo watu wengi wenye tabia hizo, wanaachana na wapenzi wao lakini muda wote wapo pamoja. Baadaye wanaanzisha tena uhusiano na kuendelea na uchafu wao.

Wanasababisha presha kwa wengine, hivyo hakuna haja ya kujinyima kama kweli waliachana kwa bahati mbaya, basi rudisheni tena penzi lenu ili watu wajue moja, kuliko kusumbua wenzenu.

Huo ndio ukweli, maana wengi wamekuwa wakiwaza na kuumiza kichwa kuona waliokuwa nao, wana ukaribu wa kupitiliza na wapenzi wao wa zamani, hivyo kuwachanganya kisaikolojia.

Nimeandika makala haya kama majibu ya baadhi ya wasomaji wangu, waliohoji uhalali wa wapenzi wao, wachumba wao kuwa na ukaribu na wapenzi wa zamani, tena wengineo wakiandikiana hadi meseji za mapenzi.

Hii sio haki na kuna ulazima wa jamii, kutambua huo ni mpango mbaya na unaweza kudhalilisha watu wengine.

Tukutane wiki ijayo.
+255 712 053949


No comments:

Post a Comment