Pages

Pages

Saturday, August 10, 2013

AHMAD SALUM ‘MADY SALU’: Fundi ujenzi anayepigania ujiko Bongo Fleva



Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
MUZIKI wa kizazi kipya, ni moja ya vitu vinavyoleta maisha mazuri kwa wasanii mbalimbali hapa nchini.  Kila msanii anaingia katika tasnia hiyo, akiwa na lengo la kujitafutia maisha yake.

Vijana mbalimbali walioingia katika sanaa hiyo, wanajimudu kimaisha, kwa namna moja ama nyingine, jambo linaloonyesha kuwa sanaa ni kazi
inayolipa mno.
Ahmad Salum, Mady Salu akiwa kwenye picha mbalimbali.
Hata hivyo, wapo wasanii, ambao licha ya kufanya juhudi kubwa kujikomboa kisanaa, wanajikuta wakiendelea kusaga rhumba njiani, huku sanaa yao ikishindwa kuonekana mara moja.


Miongoni mwa wasanii wanaopigania maisha bora katika sekta hiyo ni Ahmad Salum, anayejulikana kwa jina la usanii la Mady Salu, kwenye tasnia hiyo.


Katika mazungumzo yaliyofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita, Mady Salu anasema Mungu bado hajafungua njia yake ya mafanikio kisanaa.

Anasema licha ya kupigania maendeleo ya muziki kwa miaka zaidi ya tisa, bado hajaona namna ya kujikomboa katika tasnia hiyo ya muziki wa
Bongo Fleva.

Mady Salu anasema mwaka 2005, aliweza kuachia wimbo wa Maisha Mihangaiko, akiwa ndani ya kundi la Ngovita Crew, lililokuwa na maskani
yake Tandale jijini Dar es Salaam.

Kundi hili lilikuwa na wasanii watano, akiwamo Fico Man, Kijino, Gungwa Man, Chiteni na yeye mwenyewe, ambaye hata hivyo wimbo huo
haujafanya vizuri sana.

“Huu wimbo ulikuwa ukipigwa katika vituo vya redio, ambapo pia haijakuwa njia ya sisi kujulikana zaidi uwezo wetu, jambo ambalo lilileta
mkanganyiko.

“Wimbo wa Maisha Mihangaiko ulirekodiwa katika Studio za G2, chini ya mtayarishaji wake Roy, ambaye kwa sasa ni marehemu, moja ya wadau wa
muziki wenye historia na Bongo Fleva,” alisema.

Mady Salu na kuongeza baada ya kuachia wimbo huo, waliingia tena mzigoni na kurekodi nyimbo iliyokwenda kwa jina la ‘Tusikate Tamaa’,
uliotengenezwa na Moze P.

Hata hivyo anasema wimbo huo ulikuwa na mkosi kwao, kwani mpaka sasa haujasambazwa kwenye vituo vya redio, pia kundi lao liliingia
mdudu na kugawanyika.

Anasema wote wanaendelea kuwasiliana, maana
hawajagombana, lakini wameshindwa kabisa kukutana na kufanya kazi ya muziki kwa
maendeleo.

Anasema kundi lao la Ngovita Clew ni kifupi cha maneno ya Ngome ya Vipaji Tanzania, lilikuwa na mipango kabambe lakini mambo yalikwenda vibaya.

Msanii huyo anasema baada ya kuona mambo yamekuwa magumu, hajakata tamaa kutokana na kuipenda sanaa ya muziki wa Bongo Fleva.
“Napenda sana muziki, ndio maana kila siku ya Mungu naona siwezi kuwa mbali na sekta hiyo kwa namna moja ama nyingine, nikiamini kuwa ipo
siku mambo yatakuwa poa.

“Kutunga nyimbo kwangu sio jambo gumu, hivyo naamini kuna siku milango yangu itafunguliwa na mimi kushika nafasi za juu, katika tasnia ya
muziki huo hapa nchini,” alisema Mady Salu.

Mady Salu anasema wakati akifanya muziki kwa kuingia studio kurekodi nyimbo mbalimbali, pia anajishughulisha na kazi ya ujenzi wa
nyumba maeneo mbalimbali.

Kijana huyo anasema kazi hiyo ya ujenzi wa nyumba, ameirithi kutoka kwa baba yake Mzee Salum, anayejishughulisha na kazi hiyo kwa miaka
mingi sasa.

Anasema kwa sasa ana uwezo wa kujenga nyumba za aina mbalimbali, kuanzia msingi hadi upangaji wa matofali, kazi inayompa ahueni ya
maisha ya msoto wa muziki.

“Bila kazi hii nisingeweza kufanya lolote, maana nikipata pesa
huku, natafuta studio kwa ajili ya kuhangaikia namna ya kutangaza kipaji changu
kisanaa,” anaeleza.
Mady Salu anasema mpaka sasa amesharekodi nyimbo zake tatu, anazotarajia kuzisambaza katika vituo vya redio, ambazo ni Kama Unanipenda,
Tatizo Wewe na Rudi Kwenu.

Nyimbo hizi zote amezirekodi katika Studio za BM Records, yenye maskani yake jijini Dar es Salaam.


No comments:

Post a Comment