Pages

Pages

Friday, August 09, 2013

TFF sasa waishangaa Yanga kuitisha mkutano wa dharula



Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
SHIRIKISHO la Soka nchini (TFF), limeshangazwa na uongozi wa Yanga kuitisha mkutano wa dharula ili watowe uamuzi wa kukubali udhamini wa Azam tv au wakatae.
Msemaji wa TFF, Boniface Wambura, pichani
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Msemaji wa TFF, Boniface Wambura, alisema Yanga inapoteza muda na kujitwisha mzigo wa bure katika kufikiria la kuonyeshwa mechi zao Azam TV.

Alisema viongozi wa Yanga walikutana na Kamati ya Ligi na TFF kwa ujumla katika mkutano, hivyo haina haja ya kulifikisha suala hilo kwa wanachama wao.

“Inashangaza mno, maana mambo mengine yanafaa kuamuliwa na uongozi tu, hivyo sijui kwanini hawa Yanga wanajitwisha mzigo mzito wa bure tu kwa huo mkutano wao wa Agosti 18, katika Ukumbi wa PTA Sabasaba, jijini Dar es Salaam.

“Sasa kuna haja gani kila suala linalohitaji viongozi kuacha kuamua jambo kwa ajili ya kulipeleka kwa wanachama wao bila sababu za msingi, ukizingatia kuwa wao ndio viongozi wa Yanga,” alisema.

Suala la Azam tv limeleta mkanganyiko kutoka kwa klabu ya Yanga, baada ya kugomea mechi zao kuonyeshwa kwenye Kampuni ya Azam TV, wakisema sheria hazijafuatwa wakati wa kutoa tenda hiyo kwa kampuni inayomiliki timu ambayo nayo inashiriki Ligi ya Tanzania Bara.

Klabu 13 zinazoshiriki ligi hiyo zimeafiki kuonyeshwa mechi zao katika Azam TV, isipokuwa Yanga inayoendelea kuweka msimamo wao juu ya ofa hiyo kutoka kwa Kampuni hiyo nchini.

No comments:

Post a Comment