Pages

Pages

Friday, July 05, 2013

Twanga Pepeta yapata pigo, seneta wake Mathew Kiongozi atangaza leo kujiwekaa kando na bendi hiyo



Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
SIKU chache baada ya kuzindua albam yake 12, bendi ya Twanga Pepeta  imepata pigo kutokana na mdau wake mkubwa, ama ‘senator’ wake Mathew Kawogo maarufu kama ‘Mathew Kiongozi’ ametangaza kuachia nafasi hiyo na kuwataka wadau wa muziki wa dansi Tanzania waheshimu msimamo wake. 
Mathew Kiongozi, aliyekuwa seneta wa Twanga Pepeta
Mwanamuziki wa Twanga Pepeta, Luiza Mbutu
Bendi ya Twanga Pepeta, ilizundua albamu yake mwishoni mwa wiki iliyopita katika Viwanja vya Leaders Club, Kinondoni, iliyokwenda kwa jina la Nyumbani ni Nyumbani.


Akizungumza mapema leo mchana, Mathew Kiongozi alisema kuanzia leo yeye si seneta tena wa bendi ya Twanga Pepeta na kuamini kuwa nafasi yake itazibwa na wadau wengine wa muziki wa dansi hapa nchini na kuendeleza muziki wa dansi.

Alisema kuwa ameitumikia bendi hiyo kwa muda mrefu kwa kujitolea kwa hali na mali, ila sasa umefika wakati wa kujiweka pembeni na kuamini kuwa msimamo wako utakuwa mzuri kwake kwa ajili ya kujiweka huru zaidi.

“Nimekuwa karibu na Twanga Pepeta kwa muda mrefu mno sambamba na kushiriki harakati nyingi za kimaendeleo juu ya bendi hii, ila sasa naona nijiweke kando na kuwapisha wengine.

“Huu ni msimamo utakaoniweka huru na kuendelea kubaki shabiki wa kawaida wa bendi hii na nyinginezo zote zinazofanya muziki wa dansi Tanzania kwa ajili ya kukuza tasnia hiyo,” alisema Kiongozi.

Kutangaza kuachia nafasi yake, huenda ikawa pigo kwa bendi hiyo inayoendeshwa na Mkurugenzi wake, Asha Baraka, huku ikifanikiwa kukaa kileleni kwa kipindi kirefu tangu kuasisiwa kwake.

No comments:

Post a Comment